HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 25, 2019

TANESCO yatenga Tshs. Bilioni 400 kupeleka umeme kwenye maeneo yaliyopitiwa na miundombinu

Na Teresia Mhagama, Dodoma
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetenga kiasi cha shilingi bilioni 400 kwa ajili ya kazi ya kusambaza umeme kwenye maeneo takribani 754 yaliyopitiwa na miundombinu ya umeme lakini hayana umeme.

Hayo yalisemwa tarehe 24 Juni, 2019 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu wakati wa Majumuisho ya Semina ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti iliyohusu utekelelezaji wa miradi ya umeme vijijini na mradi wa Kinyerezi 1 Extension (MW 185).

Semina hiyo ya siku moja ilihudhuriwa na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt.Hamisi Mwinyimvua, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Wakili Julius Kalolo, Menejimenti ya Wizara ya Nishati, REA na TANESCO.

“TANESCO imeshajipanga kufanya kazi hiyo na Wizara inaendelea kusimamia kazi hizi za usambazaji umeme ili kuhakikisha kuwa zinafanyika kwa ufanisi na tumeshafanya vikao mara kadhaa ili na wadau wanaohusika na usambazaji umeme wakiwemo Mameneja wa TANESCO nchi nzima lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata umeme.” Alisema Naibu Waziri.

Aliongeza kuwa, katika mwaka wa Fedha unaoanza mwezi wa Saba mwaka huu, kipaumbele kitakuwa ni usambazaji umeme katika maeneo mbalimbali nchini kwani kila siku kuna ziada ya umeme ya kiasi cha megawati 250 hadi 300 kwa siku.

Aidha kuhusu usambazaji umeme katika Taasisi za umma kwenye miradi ya umeme vijijini alisema kuwa, Serikali kupitia REA na TANESCO itaweka kipaumbele cha kupeleka umeme kwenye maeneo hayo ili uwepo wa nishati kwenye vijiji hivyo uwe na tija.

Katika Semina hiyo, wajumbe hao walielezwa mafanikio mbalimbali ya usambazaji umeme vijijini ambapo ilielezwa kuwa, hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Mei, 2019, jumla ya Vijiji 7,217 kati ya Vijiji 12,268 ambayo ni asilimia 58.9 ya Vijiji vyote vimefikiwa na miundombinu ya umeme.

Pia, hadi kufikia mwezi Juni 2020 jumla ya Vijiji 10,278 sawa na asilimia 84 ya Vijiji vyote vitakuwa vimepatiwa umeme.

Kuhusu utekelezaji wa mradi wa Kinyerezi I Extension (MW 185) ilielezwa kuwa, mradi huo utakamilika mwezi Agosti mwaka huu na mkandarasi ni kampuni ya Jacobsen Electro ya Norway.

Katika Semina hayo, Wajumbe hao walitoa maoni mbalimbali yatakayoboresha Sekta ya Nishati nchini ambayo Wizara ya Nishati kupitia Taasisi zake iliahidi kuyafanyia kazi.
 Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akizungumza wakati wa Majumuisho ya Semina ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti iliyohusu miradi ya umeme vijijini na Kinyerezi 1 Extension, iliyofanyika jijini Dodoma. Kushoto kwa Naibu Waziri ni, Mkurugenzi Msaidizi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Nishati, Maseke Mabiki.
 Wataalam kutoka Wizara ya Nishati, REA na TANESCO wakiwa kwenye Semina ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti iliyohusu miradi ya umeme vijijini na Kinyerezi 1 Extension, iliyofanyika jijini Dodoma.
 Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Viongozi wa Wizara ya Nishati, REA na TANESCO wakiwa kwenye Semina iliyohusu miradi ya umeme vijijini na Kinyerezi 1 Extension, iliyofanyika jijini Dodoma.
 Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, akizungumza wakati wa Semina ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti iliyohusu miradi ya umeme vijijini na Kinyerezi 1 Extension, iliyofanyika jijini Dodoma. Kulia kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Viongozi wa Wizara ya Nishati, REA na TANESCO wakiwa kwenye Semina iliyohusu miradi ya umeme vijijini na Kinyerezi 1 Extension, iliyofanyika jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad