HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 25, 2019

Muhimbili yaboresha huduma za ICU kutoka vitanda 25 hadi 78

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeongeza idadi ya vitanda katika wodi za wagonjwa wanaohitaji huduma za uangalizi maalum (ICU) kutoka 25 hadi 78 ikiwa ni sehemu ya mkakati wa hospitali wa kuboresha miundombinu ya kutoa huduma kwa wagonjwa.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kina mama wa MNH, Dkt. Vicenti Tarimo amesema lengo la kuboresha miundombinu inayotumika kutoa huduma ni kupunguza vifo vya kina mama wanaofariki dunia kutokana na kifafa cha mimba.

“Hospitali imetengeneza chumba cha kina mama wanaohitaji huduma ya uangalizi maalum (MAICU) chenye vitanda 10, pia imeweka mashine tano za kusaidia kupumua na ultrasound. Hivi sasa, huduma hii inapatikana kwenye jengo lao ukilinganisha na zamani ambapo mama alipaswa kupelekwa ICU ya kawaida ambayo ipo umbali wa mita 150. Hali hii ya upatikanaji wa huduma ilikuwa inahatarisha uhai wa mama na mtoto. Maisha ya kina mama wengi yameokolewa kupitia MAICU,” amesema Dkt. Tarimo. 

Dkt. Tarimo amefafanua kwamba kuwapo kwa huduma ya MAICU kumesaidia  kupunguza vifo vya kina mama kutoka 125 mwaka 2017/2018 hadi kufikia vifo 86 Julai 2018 hadi Juni 2019.  

Amesema uboreshaji wa huduma MNH ni sehemu ya kutekeleza malengo ya Serikali pamoja na malengo ya milenia ya kupunguza vifo vya kina mama.

“Hatua hii inaifanya MNH kuwa Hospitali ya kwanza ya umma hapa nchini kuwa na ICU ya kina mama wajawazito wenye kuhitaji uangalizi maalumu,” amesema Dkt. Tarimo.

Dkt. Tarimo amebainisha pia MNH ina ICU ya watoto wachanga (NICU) yenye vitanda 18, PICU ya watoto wenye umri wa kuanzia mwezi yenye vitanda 12, wodi ya wagonjwa wa tiba (MICU) ambayo ina vitanda 15, wodi ya wagonjwa wa upasuaji wanaohitaji uangalizi maalum (SICU) yenye vitanda 18, wodi ya wagonjwa wanaopandikizwa figo wanaohitaji uangalizi maalum ambayo ina vitanda 5 na ICU ya kina mama wajawazito (MAICU) ambayo ina vitanda 10.

“Shirika la Afya Duniani (WHO) linazitaka Hospitali kuwa na asilimia 10 ya vitanda vya ICU. MNH ina vitanda 1,550 hivyo inatakiwa kuwapo kwa vitanda 155 vya ICU. Hivi sasa MNH ina vitanda 78 sawa na asilimia 50 ya takwa la WHO. Hizi ni jitihada kubwa za uboreshaji huduma kwa wananchi,” amesema.

Dkt. Tarimo amesema kwamba uwapo wa miundombinu ya ICU, imesadia watalaam kutoka hospitali nyingine nchini kuja kujifunza namna bora ya kuanzisha na kuendesha vyumba vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum kwa makundi mbalimbali.

“Baadhi ya hospitali za rufaa za mikoa zimeanza kuleta watalaam wake kujifunza jinsi ya kutoa huduma kwenye ICU. Vilevile huduma hizi zitasaidia katika utafiti wa mahitaji halisi ya huduma za ICU pamoja na gharama zake na hivyo kusaidia Wizara ya Afya na Serikali kwa ujumla katika kuweka mipango ya upanuzi wa huduma hii hapa nchini,” amesema Dkt. Tarimo.

Katika hatua nyingine, Hospitali imefanya ukarabati mkubwa katika wodi 3 hadi 6 za Mwaisela na kuweka mfumo wa oxygen pamoja na vitanda 7 kila wodi sawa na vitanda 28 vya kutoa huduma kwa wagonjwa maalum (HDU). Uboreshaji huu utawasaidia wagonjwa wa kiharusi kuonwa kitalaam zaidi na kuwa  kwenye uangalizi wa karibu ikilinganishwa na awali walikuwa wakilazwa katika wodi za kawaida.
 Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kina mama wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Vicenti Tarimo akizungumza na waandishi wa habari juu ya uboreshaji wa wodi zinazolaza wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU). Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Ukunga na Uzazi wa MNH, Bi. Mugara Mahungururo akiwa kwenye mkutano leo.
Meneja wa Jengo la Wazazi namba Moja wa MNH, Suzana Ndambala akitoa ufafanuzi katika kuhusu  huduma inayopatikana katika ICU ya kina mama wajawazito (MAICU) ina vitanda 10.
 Pichani ni waandishi wa habari wakimsikiliza Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kina mama wa MNH, Dkt. Tarimo kuhusu uboreshaji wa miundimbinu inayotumika kutoa huduma kwa wagonjwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad