HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 24, 2019

SETH ARUHUSIWA NA MAHAKAMA KUONANA NA WAKILI WAKE AKIWA MAGEREZA

Na Karama Kenyunko Michuzi TV

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewaamuru maofisa wa Magereza anapokaa mshitakiwa Harbinder Seth anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, kumruhusu kuonana na wakili wake kwa sababu ni haki yake ya masingi.

Amri hiyo imetolewa Mei 23, 2019 baada ya mshtakiwa Seth kudai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa ana miezi sita hajaonana na wakili wake kwa sababu maofisa wa magereza wanamkatalia kufanya hivyo.

Seth amedai,  anataka kuonana na wakili wake ili waweze kuzungumzia masuala ya kesi hiyo hivyo anaomba kibali cha mahakama aweze kuruhusiwa kuonana na wakili wake.

Mapema kabla ya kutolewa kwa amri hiyo, wakili wa Serikali, Wankyo Simon alidai  kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi bado haujakamilika hivyo ameomba tarehe nyingine kwa ya kutajwa.

Kufuatia hayo, Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 10, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa wamerudishwa rumande.

Mbali na Seth mshitakiwa mwengine ni mfanyabiashara  James Rugemalira ambapo wote kwa  pamoja wanaokabiliwa na mashtaka 12 yakiwemo ya utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27 kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani hapo Juni 19, 2017. 

Washitakiwa hao wanadaiwa kuwa Oktoba 18, 2011 na Machi 19 , 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ili kutenda kosa.

Aidha, inadaiwa katika mashitaka ya kujipatia fedha kwamba  kati ya  Novemba 28 na 29, 2011 na Januari 23,2014 katika Makao makuu ya Benki ya Stanbic Kinondoni  na Benki ya Mkombozi tawi la Mtakatifu Joseph,  kwa ulaghai washitakiwa hao walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Dola za Marekani  22,198,544.60 na Sh 309, 461,300,158.27.  

Pia washitakiwa wote wanadaiwa kuisababishia serikali hasara ambapo inadaiwa walitenda makosa hayo Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la  kati kinondoni, kwa vitendo vyao waliisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani 22, 198, 544.60 na Sh. 309,461,300,158.27.

Kati ya Novemba 29,2013 na Januari 23, 2014 maeneo tofauti Dar es Salaam kwa pamoja walitenda kosa la kutakatisha fedha kwa kuchukua fedha kutoka BoT ambazo ni dola za Marekani milioni 22.1 na Sh bilioni 309.4  wakati wakijua fedha hizo ni zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Washitakiwa hao wapo rumande kwa kuwa mashitaka hayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad