HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 17, 2019

SERIKALI KUPITIA UPYA MASHAMBA YALIYOFUTWA KILOSA

Na Munir Shemweta, KILOSA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema wizara yake itapitia upya mashamba yote yaliyofutwa na Raisi katika wilaya ya Kilosa mkoa wa Morogoro.

Lukuvi amesema hayo tarehe 16 Mei 2019 katika kata ya Chanzulu tarafa ya Kimamba wilaya ya Kilosa mkoa wa Morogoro alipozungumza na wananchi wa kata hiyo wakati alipokwenda kutatua mgogoro wa Ardhi katika wilaya hiyo ikiwa ni jitihada za wizara kumaliza migogoro ya ardhi nchini.

Waziri Lukuvi alisema, katika maeneo mbalimbali yapo mashamba yaliyofutwa na Raisi lakini hayajawekewa utaratibu wa kuyatumia na hivyo kutoa fursa kwa wajanja wachache kujigawiwa na mengine kuyauza kwa wananchi bila kufuata utaratibu.

Alisema, katika kuhakikisha mashamba yote yaliyofutwa na Rais katika wilaya ya Kilosa na kuzua mgogoro baina ya wananchi na wamiliki wizara yake imeamua kupeleka timu kutoka wizarani kwa ajili ya kuyafanyia uhakiki mashamba yote yaliyofutwa katika wilaya ya Kilosa.

Kwa mujibu wa Lukuvi timu hiyo inajumuisha Kamishna wa ardhi nchini Mary Makondo, Kaimu Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Samweli Katambi, Mthamini Mkuu wa Serikali Evalyne Mugasha, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Kati Ezekiel Kitlya na Wataalamu kutoka idara za Mipango Miji Wizarani.

Alisema, uamuzi wa kwenda na timu kutoka Wizarani unalenga kumaliza kabisa migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo hasa baada ya kubaini ofisi za wilaya na mkoa wa Morogoro kushindwa kutatua mgogoro huku viongozi wa wake wakituhumiwa.

Waziri wa Ardhi alitaja kazi kubwa itakayofanya timu hiyo kuwa ni kupitia mashamba 15 yaliyofutwa na raisi sambamba na kufufua mipaka ya mashamba hayo na kazi hiyo itafanywa kwa na ushirikiano wa ngazi za wilaya.

" Tutayapitia mashamba yote yaliyofutwa na Raisi na kujua kilichomo ndani yake na timu ya uhakiki niliyokuja nayo itanilitea mapendekezo ya namna ya kutumia mashamba na mengine watapewa wanaostahili na si kila mtu atapewa" alisema Lukuvi

Huku akishangiliwa na wananchi wa Chanzulu Lukuvi alisema, wale wote waliojimilikisha mashamba yaliyofutwa na Rais watanyang'anywa na kupatiwa wanaostahili na mengine yatatolewa kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa ajili ya kupatiwa wawekezaji.

Mkuu wa Idara ya Ardhi, Maliasili na Mazingira katika halmashauri ya Kilosa Ibrahim Mndembo alisema, Jumla ya mashamba 25 yenye ukubwa wa ekari 23,596 kwenye maeneo ya Msowero, Magole na Chanzulu katika wilaya ya Kilosa yamebatilishwa umiliki baada ya wamiliki wake kushindwa kuyaendeleza ambapo kati ya mashamba hayo mashamba 15 yalibatilishwa miliki zake katika kipindi cha uongozi wa serikali ya awamu ya tano.

Mashamba yenye mgogoro na wananchi katika wilaya ya Kilosa ni Noble Agriculture Enterprises, Magereza dhidi ya wananchi wa Mabane, Mbigiri na Mabwegere, Chadulu Estate, Shamba la Swai dhidi ya wananchi wa Ilonga na shamba la Mauzi Estate Malangali.
 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na wananchi wa Chanzulu Kilosa mkoani Morogoro alipokwenda kutatua migogoro ya ardhi ikiwa ni jitihada za Wizara ya Ardhi kumaliza migogoro ya ardhi nchini.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na viongozi wa wilaya ya Kilosa alipokwenda kutatua migogoro ya Ardhi katika wilaya hiyo ikiwa ni jitihada za wizara ya Ardhi kumaliza migogoro ya ardhi nchini. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad