Balozi wa Kenya nchini Tanzania Dan Kazungu amewaomba wawekezaji
kutoka kila pande ya dunia kujitokeza kwa wingi kuwekeza kwa kujenga
hoteli na nyumba za kupumzikia wageni katika eneo linalozunguka
maporomoko ya Kalambo (Kalambo Falls) yaliyopo katika Wilaya ya
Kalambo Mkoani Rukwa.
Amesema kuwa eneo hilo ni zuri kwa wanafamilia kulitumia katika siku
za mapumziko, siku za sikukuu na pia kujitokeza ili kuyaona maajabu
hayo ambayo yametambuliwa na Shirika la umoja wa mataifa la Elimu,
Sayansi, na Utamaduni (UNESCO) kuwa ni urithi wa dunia.
“Tunaomba wawekezaji waje hapa kwa wingi, hapa kuna kivutio ambacho
kimejulikana na umoja wa mataifa UNESCO kama hifadhi ya urithi wa
dunia, mje wawekezaji hapa, pahali ambapo siku za mwisho wa wiki watu
wanaweza kuja kujipumzisha ama siku za sikukuu kuja na familia yao
kwaajili ya “picnic”, wanajenga “lodges” lakini tunaomba “lodges”
zijengwe nyingi zaidi za hadhi ya ubora wa juu zaidi ili tufurahie na
familia zetu,” Alisema.
Balozi Kazungu ameyasema hayo alipotembelea maporomoko ya kalambo
katika ziara yake ya siku moja Mkoani Rukwa iliyolenga kutafuta fursa
za uwekezaji katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huku akitembelea kiwanda
cha Nyama cha SAAFI pamoja na ujenzi wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa
Sumbawanga.
Aidha, Balozi Kazungu alitoa ushauri kwa wakala wa misitu Tanzania
wanaoshughulika na uhifadhi wa msitu wa Kalambo pamoja na kuimarisha
miundombinu ya maporomopko hayo kuona uwezekazo wa kuweka nyaya pamoja
na vigari vitakavyopita kwenye nyaya hizo ili watalii waweze kuyaona
maporomoko hayo vizuri zaidi pamoja na msitu huo.
Wakati akisoma taarifa ya maporomoko hayo ya Kalambo, Kaimu Meneja wa
Wakala wa Misitu Wilaya ya Kalambo Helman Ndanzi amesema kuwa pindi
ujenzi wa ngazi za kushukukia kutoka maporomoko yanapoanzia hadi
kufikia sehemu maji yanapodondokea utakapokamilika, ngazi hizo
zitakuwa na urefu wa mita 1277 na kugharimu shilingi 852,789,066.70.
“Changamoto zilizopo ni kutotangazwa vya kutosha maporomoko hayo hali
inayopelekea kutojitokeza kwa wawekezaji katika eneo hilo ambalo
mawasiliano ya simu pia bado ni tatizo na hivyo tunaiomba mitandano
mbalimbali ya simu kujitokeza kuweka minara katika maeneo haya ili
mawasiliano yawe rahisi,” Alisema.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo
alimhakikishia Balozi huyo kuwa mkoa umejipanga kuhakikisha
unakamilisha miundombinu inayohitajika ili kuwarahisishia wawekezaji
kutekeleza shughuli zao kwa urahisi na hatimae kuinua uchumi wa
wananchi katika mkoa lakini pia uchumi Tanzania kwa ujumla.
“Sisi tupo kwenye mpango ule wa viwanja vya ndege vile vinne, kuna
kiwanja hiki cha Sumbawanga, Tabora, Shinyanga pamoja na Kigoma,
karibu kila kitu kipo tayari kimazingira, vitu vyote vinavyotakiwa
kufanyika kabla ya kuanza upanuzi wa uwanja tayari vimekwishafanyika,
mhandisi mshauri yupo, mkandarasi yupo, mikataba tayari, fidia kwa
wananchi waliohusika nae neo la upanuzi tayari, kila kitu kipo tayari,
bado serikali haijaruhu lakini bila ya shaka wakati wowote ruhusa
itatoka,” Alisisitiza.
Maporomoko ya Kalambo ni maporomoko ya pili kwa urefu kutoka maji
yanapoanzia kumwagika hadi yanapodondokea kwa mita 235 na upana wa
mita kuanzia 3.6 hadi mita 18 (single drop waterfall) ambapo
maporomoko ya kwanza ni ya TUGELA yaliyopo Afrika ya Kusini yenye
urefu wa mita 947.
Balozi wa Kenya Nchini Tanzania Dan Kazungu akitoa ushauri kwa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wilaya ya Kalambo juu ya kuboresha eneo hilo la Maporomoko.
Balozi wa Kenya Nchini Tanzania Dan Kazungu (mbele kulia) akiongozana na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (mbele kushoto) wakati wakiteremka ngazi za kuelekea kwenye kina cha maporomoko ya Kalambo. (Kalambo Falls)
Balozi wa Kenya Nchini Tanzania Dan Kazungu baada ya kufika eneo ambalo unaweza kuyaona maporomoko hayo vizuri.
Sehemu ya Maporomoko ya Kalambo (Kalambo Falls)
No comments:
Post a Comment