Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba
Pato la Taifa kwa Mwaka 2019 linatarajiwa kukua kwa kasi ya wastani wa
asilimia 7.8% itakayosababisha kuimarika zaidi kwa Uchumi wa Zanzibar
kutokana na ongezeko la Uwekezaji katika Sekta ndogo ya usafirishaji
na Uvuvi.
Alisema hali hiyo imesababisha kuongezeka kwa Pato la Mwananchi mmoja
mmoja kutoka Shilingi Milioni 2,104,000/- sawa na Dola za Kimarekani
Mia 944 na kufikia Shilingi za Kitanzania Milioni 2,323,000/- sawa na
Dola za Kimarekani Elfu 1.026.
Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nchi Ofisi
ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika Kibao cha Bajeti
2019/2020 kilichoanza Baraza la Wawakilishi Chukwani Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar tayari
imekaribia kufikia kiwango cha Nchi ya kipato ca Kati cha Dola za
Kimarekani Elfu 1,030 kwa mujibu wa vigezo vya Kimataifa.
Balozi Seif alisema Pato la Taifa kwa bei ya soko limefikia thamani ya
Shilingi Bilioni 3,663,000,000/- kwa Mwaka 2018 kutoka thamani ya
Shilingi Bilioni 3,228,000,000/- kwa Mwaka 2017 kulikosababishwa na
ongezeko la pato la Mwananchi.
Alisema kasi ya mfumko wa bei pia umeshuka hadi kufikia wastani wa
asilimia 3.9 Mwaka 2018 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 5.6
Mwaka 2017 baada ya kuchukuliwa hatua za udhitibi wa mfumko wa bei kwa
kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula.
Balozi Seif alisema hali hiyo inatokana na uwezeshwaji waliopatiwa
Wakulima kwa kupatiwa pembejeo na mafunzo ya kuongeza uzalishaji kwa
kutumia Teknolojia ya gharama nafuu iliyokwenda sambamba na utafiti
katika Sekta ya Kilimo uliosaidia kupata mbinu za kupiga vita
changamoto zinazoyakabili mazao ya matunda na mboga za majani.
Alieleza kwamba Muelekeo wa Hali ya Uchumi wa Zanzibar kwa Mwaka 2019
unategemewa kwenda sambamba na Utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya
2020, Mkakati wa Kukuza Uchumi Zanzibar {MKUZA 111} na ilani ya
Uchaguzi ya Chama cha Mapinduai ya Mwaka 2015 – 2020.
Balozi Seif alifahamisha kuwa mafanikio yote yaliyopatikana
yanatokana na jitihada kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar chini ya Uongozi mahiri wa Rais wa Zanzibar Dr. Ali
Mohamed Shein katika kuona hali ya uchumi na Kijamii ya Taifa na
Wananchi inazidi kuimarika kila kukicha.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba azma ya
Serikali kuu ni kuhakikisha kwamba inakamilisha Miradi yote mikubwa ya
Maendeleo kama ilivyoahidi katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha
Mapinduzi ya Mwaka 2015 – 2020.
Aliitaja Miradi hiyo kuwa ni pamoja na Ujenzi wa Jengo la Abiria
{Terminal 3} katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume
Zanzibar, Ujenzi wa Bandari ya Mpiga Duri iliyopo Maruhubi pamoja na
Ujenzi wa Hospitali Binguni iliyopo Wilaya ya Kati.
Alisema miradi hiyo inakwenda sambamba na mpango wa Taifa wa kuendelea
kuimarisha uzalishaji na usafirishaji wa zao la Karafuu kutokana na
matarajio ya msimu mkubwa wa zao hilo kwa Mwaka huu wa 2019 pamoja na
kupanuka kwa kiwango cha idadi ya Watalii kutokana na kupatikana kwa
masoko mapya ya sekta hiyo.
Balozi Seif alifafanua wazi kwamba Serikali tayari imeandaa mikakati
maalum ya kutafuta fedha kwa Nchi na Mashirika rafiki sambamba na
kutenga Fedha kutoka katika vianzio vyake vya ndani ili itapotokezea
kushindikana kupata msaada kutoka nje Serikali iendelee na
ukamilishaji wa Ujenzi wa Miradi hiyo.
Akizungumzia hali ya upatikanaji wa Mchanga, Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar alisema mchanga ni Rasilmali muhimu hapa Nchini kutokana na
matumizi makubwa katika Sekta ya Ujenzi.
Balozi Seif alisema kwa bahati mbaya eneo halisi linaloweza kuchimbwa
mchanga katika Visiwa vya Zanzibar ni dogo zaidi kwa kuwa baadhi ya
maeneo mengine tayari yameshachimbwa, wakati mwengine yanatumika kwa
matumizi ya Kibinaadamu ikiwemo Makaazi, Kilimo na Huduma za Kijamii.
Alisema kutokana na changamoto hiyo Serikali Kuu ililazimika kutangaza
utaratibu Mpya wa usimamizi wa uchimbaji, usafirishaji na uuzaji
Mchanga ulioanza Tarehe 3 Machi Mwaka 2017 kwa lengo la kujaribu
kudhibiti maeneo ya Ardhi na kuweza kutumika kwa shughuli nyengine
hasa Kilimo.
Alifahamisha kwamba tokea kuanza kwa utaratibu huo unaosimamiwa na
Serikali Kuu yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana ikiwemo gari
zinazobeba mchanga kupimwa ili kupata Takwimu na malipo sahihi ya
bidhaa hiyo, kupunguza msongamano wa Gari machimboni pamoja na uwepo
wa bei elekezi inayowazuia Wafanyabiashara kupandisha bei ya mchanga
kiholela ambayo huwaumiza Wananchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliweka wazi kwamba katika kipindi
cha kuanzia Mwezi Machi 2017 hadi Disemba 2018 chini ya usimamizi huo
jumla ya Tani Milioni 1,690,122 za Mchanga zilichimbwa Visiwani
Zanzibar.
Alisema kati ya Tani hizo Unguja ilichimbwa na kusafirishwa Tani
Milioni 1,605,517 na Pemba zilizchimbwa na kusafirishwa Tani 84,605
sawa na asilimia 5% ya uchimbaji unaofanyika katika Kisiwa cha Unguja.
“ Kwa Takwimu hizi ni wazi kwamba ipo kasi kubwa ya uchimbaji wa
mchanga katika Kisiwa cha Unguja ikilinganishwa na uchimbaji wa
Mchanga katika Kisiwa cha Pemba”. Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa Wananchi kwamba
Serikali haitamvumilia Mtu ye yote yule ambae atachimba na kusafirisha
mchanga kinyume na utaratibu uliowekwa au kuuza mchanga kinyume na bei
elekezi iliyowekwa na Serikali.
Kuhusu Sekta ya Elimu Balozi Seif alisema Serikali Kuu kupitia Wizara
inayosimamia Taaluma inaendelea kuchukuwa hatua kadhaa katika
kuhakikisha mazingira ya Elimu yanakuwa mazuri ili Watoto wa Visiwa
vya Zanzibar waweze kupata Haki yao ya Elimu bila ya Malipo.
Alisema inapendeza kuona asilimia ya Uandikishaji katika ngazi zote za
Elimu ya lazima imeongezeka ikilinganishwa na Mwaka wa Fedha wa
2017/2018 ambapo ngazi ya Maandalizi uandikishaji umefikia asilimia
69.4% Mwaka 2018 kutoka asilimia 66.1 Mwaka 2017.
Balozi Seif alieleza kwamba kasi hii ya uandikishaji inatokana na
upatikanaji wa nafasi, mwamko wa Jamii kuhusu Elimu na ushiriki mzuri
wa Wananchi katika kuleta Maendeleo kwenye Sekta ya Elimu.
Alieleza kwamba katika juhudi za kuimarisha Sekta hiyo muhimu kwa
Taifa lolote lile Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana
na Mfuko wa OPEC tayari imekamilisha ujenzi wa Skuli Tisa za Ghorofa
za Sekondari Unguja na Pemba.
Alisema Mradi huo mkubwa umekwenda sambamba na ujenzi wa Maabara,
Maktaba na vyumba vya Kompyuta kwa Skuli 24 za Sekondari kwa
mashirikiano na Benki ya Dunia.
Balozi Seif alifahamisha kwamba katika kuimarisha Elimu ya Sekondari
Serikali imegawa vifaa vya Maabara na Kemikali kwa Skuli zote za
Sekondari za Unguja na Pemba zenye Kidato cha Nne na cha Sita ili
kuwawezesha Wanafunzi kusoma kwa vitendo na kujiandaa vyema na
Mitihani yao.
Akigusia kadhia ya uvujaji wa Mitihani ya Darasa la Kumi iliyofanyika
Disemba Mwaka 2018 na kupelekea Serikali kupitia Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya amali kufuta Mitihani hiyo Serikali tayari imeshachukuwa
hatua za kuwasimamisha kazi Watendaji wote waliohusika kutoka Wizara
ya Elimu pamoja na Wizara ya Habari kwa mujibu wa Sheria za Utumishi
wa Umma.
Balozi Seif alisema kadhia hiyo isiyovumilika imepelekea Serikali
kuiagiza Kamati ya Taifa ya Ulinzi na Usalama kufanya uchunguzi wa
kina na kujua chanzo chake ambapo tayari imeshakamilisha kazi yake
iliyoagizwa na kuwasilisha rasmi Taarifa hiyo Serikalini.
Alisema Taarifa hiyo ya uchunguzi imebaini baadhi ya Watendaji wa
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar pamoja na baadhi ya
Watendaji wa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale kubainika
kuhusiaka na kadhia hiyo iliyolitia aibu Taifa.
Balozi Seif alisema kwa mnasaba huo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
tayari imeshalitaka Jeshi la Polisi Nchini kuwachukulia hatua za
Kisheria kwa mujibu wa Makosa waliyofanya wale wote waliohusika na
tukio hilo lililoleta hasara kubwa ya Fedha za Umma.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameliomba
Baraza la Wawakilishi liidhinishe jumla ya Shilingi Bilioni Hamsini na
Saba, Mia Tisa na Kumi na Moja Milioni, Laki Tatu na Arubaini na Tisa
Elfu { 57,911,349,000/- } kwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar na Taasisi zake kwa ajili ya kutekeleza Program 11 kwa Mwaka
wa Fedha wa 2019/2020.
Alisema katika mchanganuo huo Shilingi Bilioni Arubaini na Nane Kumi
na Tatu Milioni na Laki Nne { 48,013,400,000/- } ni kwa Kazi za
kawaida na Shilingi Bilioni Tisa, Mia Nane na Tisini na Saba Milioni,
Laki Tisa na Arubaini na Tisa Elfu { 9,897,949,000/- } ni kwa kazi za
Maendeleo.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwasilisha Hotuba ya
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake ya Nchi Ofisi ya Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika kikao cha Bajeti kilichoanza rasmi
Mwaka huu wa Fedha wa 2019/2020.
Baadhi
ya Manaibu Mawaziri wa Wizara za Serikali wakifuatilia hotuba ya
Makadirio ya Mapato na Matumizi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar.
Baadhi
ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakifuatilia hotuba ya Makadirio ya
Mapato na Matumizi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Baadhi
ya Viongozi Waandamizi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
wakiongozwa na Katibu Mkuu wake Nd. Shaaban Seif Mohamed wa pili kutoka
Kulia Mstari wa chini.
Baadhi
ya Watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar wakifuatilia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar iliyowasilishwa na Balozi
Seif.
Baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar wakisikiliza hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi Ofisi
ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar iliyowasilishwa na Balozi Seif. Picha na – OMPR – ZNZ.
No comments:
Post a Comment