HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 3 April 2019

VODACOM, TALA WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUISABABISHIA HASARA SERIKALI

Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii.

MKURUGENZI Mtendaji wa kampuni ya simu za mkononi, Vodacom Tanzania, 
Hisham Hendi raia wa Misri , wafanyakazi wake wanne, raia wawili wa Kenya na wenzao,  wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi  ya uhujumu uchumi, likiwemo  shtaka la kuisababishia Serikali hasara ya bilioni 5.2

Mkurugenzi huyo na wenzake wameunganishwa na washtakiwa Ahmed Issa ambaye ni Meneja uwendeshaji wa biashara wa kampuni ya Inventure Mob Tanzania Ltd, na raia wa Kenya,  Brian Lusiola ambaye ni mtaalami wa IT,  ambao walisomewa mashtaka sita wiki iliyopita.
  Mbali na Hend ambaye ni raia wa Misri, washitakiwa wengine ni Mkuu wa Kitengo cha Mapato wa Vodacom PLC, Joseph Nderitu ambaye ni raia wa Kenya, Mkurugenzi wa Sheria wa kampuni hiyo, Olaf Mumburi Mkazi wa Victoria Kinondoni.

Wengine ni Mkuu wa Kitengo cha Mauzo wa kampuni hiyo, Joseph Muhere, Meneja wa Uhasibu, Ibrahim Bonzo wa Kampuni ya Vodacom iliyopo Ursino Estate barabara ya Bagamoyo.

Akisoma hati ya mashtaka  Wakili wa Serikali Mwandamizi, Jackline Nyantori amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi kuwa, kati ya Januari 2018 na Machi 2019 huko katika jengo la Tanzanite Park, lililopo Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, washtakiwa Ngasa, Lusiola na kampuni ya Tala Tanzania waliongoza genge la uhalifu  na kuisababishia serikali kupitia TCRA, hasara ya Sh bilioni 5.8.

Katika shtaka la pili, washtakiwa hao hao  wanadaiwa, katika tarehe isiyofahamika kati ya Januari Mosi na Desemba 31, 2018, waliingiza kifaa cha mawasiliano kinachoitwa Proliant MLI GEN 9 Server (PABX Virtual Mashine yenye serial number 76520D88838129_425) bila kuwa na leseni kutoka TCRA.

Washtakiwa wanadaiwa pia kusimika kifaa hicho na kuendesha mtambo huo wa mawasiliano bila kuwa na leseni inayotolewa na TCRA.

Aidha  washtakiwa wanadaiwa, kutoka Januari 2 hadi  Machi 11,2019 waliendesha kifaa hicho cha kieletroniki cha mawasiliano kwa kuruhusu simu za kimataifa zilizoingia nchini bila kibali cha TCRA. Pia imedaiwa kati ya Aprili 17, mwaka jana na Machi 11, washtakiwa waliendesha mitambo hiyo kwa kupokea na kusambaza upokeaji wa simu za kimataifa bila kuwa na leseni hiyo.

Katika shtaka la tano, inadaiwa kati ya Aprili 17, mwaka jana na Machi 11, mwaka huu, washtakiwa walikwepa kodi ya kupokea na kusambaza huduma ya upokeaji wa simu za kimataifa kwa kusambaza mawasiliano kwa kutumia mfumo huo.

Washitakiwa hao pia wanadaiwa Aprili 17, mwaka jana na Machi 11, mwaka huu kinyume na sheria, washtakiwa walitumia vifaa vya mawasiliano kuunganisha  huduma ya kieletroniki ya mawasiliano kwa lengo la kupokea na kusambaza mfumo wa mawasiliano bila kupata kibali cha TCRA.

Imeendelea kudaiwa kuwa, katika tarehe hizo, maeneo ya Tanzanite Park Building Kinondoni, Ngassa, Lusiola na Kampuni ya Tala, walitumia namba 813 za Vodacom ambazo ni namba maalum bila kupewa na TCRA.

Ngassa, Lusiola na Tala, pia wanadaiwa katika tarehe hizo, waliisababishia TCRA hasara ya Sh Milioni 642.2.

Katika shtaka la Tisa, Wakili Wankyo Simon amedai kuwa Hendi, Nderitu, Mumburi, Muhere, Bonzo na Kampuni ya Vodacom, kati ya Aprili 17, mwaka jana na Machi 11, mwaka huu maeneo ya jengo la Vodacom, lililopo Ursino Estate barabara ya Bagamoyo, Dar es Salaam, waliwaruhusu  Ngassa, Lusiola na Tala kutumia namba 813 za Vodacom bila kuzipata kutoka TCRA.

Pia Simon alidai washitakiwa hao kutoka Vodaom katika tarehe hizo, kwa pamoja waliisababishia serikali na TCRA hasara ya Sh 5,250,237,000.

Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mhakamani hapo kwa kuwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi ispokuwa kwa kibali kutoka kwa DPP. Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na imeahirishwa hadi  Aprili 17, 2019 kwa kutajwa

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad