HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, March 21, 2019

NAIBU MEYA ILALA AZINDUA MRADI WA MAJI VINGUNGUTI

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
NAIBU Meya wa Manispaa ya Ilala Omar Kumbilamoto amezindua mradi wa maji Mtaa wa Majengo Kata ya Vingunguti utakaohudumia wananchi 1440 kwa siku.

Mradi huo uliogharimu milioni 28 kuanzia uchimbaji wa kisima, ujengaji wa Vizimba vya kuchotea maji na tanki utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita 4800 kwa siku  na kuondoa kero ya maji kwa kwa wananchi wa mtaa wa Majengo.

Akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Kumbilamoto amesema pongezi kubwa zinaenda kwa Mhandisi wa Maji Manispaa ya Ilala kwa jitihada kubwa alizofanya za kuwezesha kupatikana kwa mradi huo na kumalizika kwa wakati.

Amesema, baada ya kukamilika kwa mradi huu ambao ulikuwa unasubiriwa na wananchi kwa muda mrefu, jumuiya ya watumia maji wajiongeze kwa kuweza kusimamia mradi huu kwa uweledi na uweze kujiendesha ikiwemo kuzalisha miradi mingine.

“Tunajua kunakuwa na changamoto hususani kwenye jumuiya za maji kwa kushindwa kusimamia miradi iliyopo kwenye mitaa ila napenda kuwaambia kuwa jumuiya mjiongeze kwa kusimamia miradi hii ili iweze kujiendesha yenyewe na kuzalisha mingine kwani visima vya watu binafsi vimekuwa na maendeleo mazuri kuliko vya serikali,”amesema Kumbilamoto.

Kumbilato amewataka Manispaa kuangalia beinza maji na kuweka utofauti kati ya bei ya visima vya watu binafsi na vya serikali ili wananchi wengi wapate maji safi na salama.

“Wananchi pia watunze miundo mbinu ya maji ili iweze kudumu na wapate maji safi na salama kwani lengo la serikali ya awamu ya tano kama inavyoanishwa na makamu wa Rais Samia Suluhu ni kumtua mama ndoo Kichwani,”amesema Kumbilamoto.

Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Mhandisi Upendo Lugongo amesema eneo lililojengwa mradi huo litasaidia wananchi 1440 na maji yatapatikana kwa saa 24.

Aidha, ameeleza kuwa sheria mpya iliyopotishwa ni kuwa watumishi wote wa maji katika manispaa pamoja na miradi ya maji ya Halmashauri na mitaa kwa sasa itaungana na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Mkoa wa Dar es Salaam (DAWASA).

Upendo amewaomba wananchi kuendelea kulinda miundo mbinu pamoja na kutumia maji hayo kwa manufaa yao wote.

Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Majengo Chande Msoke ameishukuru serikali pamoja na Kamati ya Utendaji kwa kupitisha bajeti na kufanikiwa kwa kumalizika kwa mradi huo ndani ya wakati na kuwa kwa sasa kero ya maji kwenye mtaa wake umemalizika.

Katika kusherehekea wiki ya maji iliyoanza Machi 16 na kumalizika Machi 22, miradi mbalimbali ya maji imezinduliwa ikiwa ni mikakati ya kuhakikisha kufiki 2020 asilimia 95 ya wananchi wanapata maji safi na salama kwa mjini na asilimia 85 kwa upande wa vijijini.
Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala Omar Kumbilamoto akizundua mradi wa maji mtaa wa Majengo Vingunguti leo Jijini Dar es Salaam utakaohudumia wananchi 1440 kwa siku ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya maji iliyoanza Machi 16-22.
 Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala Omar Kumbilamoto akimtua mama ndoo kichwani baada ya kuzindua mradi wa maji mtaa wa Majengo Vingunguti leo Jijini Dar es Salaam utakaohudumia wananchi 1440 kwa siku ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya maji iliyoanza Machi 16-22.
 Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala Omar Kumbilamoto akifungua bomba la maji kuashiria uzinduzi wa mradi wa maji mtaa wa Majengo Vingunguti leo Jijini Dar es Salaam utakaohudumia wananchi 1440 kwa siku ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya maji iliyoanza Machi 16-22.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad