HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, March 29, 2019

MAKAMU WA RAIS AZINDUA JENGO NA MASHINE ZA TIBA ZA LINAC KATIKA TAASISI YA SARATANI OCEAN ROAD

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema tatizo la saratani kwa Watanzania linaweza kupungua ama kuondokana nalo endapo kutakuwa na tabia ya kupima afya zetu mara kwa mara.

Makamu wa Rais ameyasema hayo leo kwenye uzinduzi wa jengo na mashine mpya za tiba ya mionzi LINAC ambazo ni za kisasa kabisa na kwa Afrika, Tanzania inakuwa nchi ya kwanza kuwa nazo.

“tunaweza kujikinga kwa kufuata kanuni za afya zinavyotuelekeza kula chakula bora, kufanya mazoezi mara kwa mara, na kuepuka kunywa pombe kupita kiasi na kuepuka matumizi ya tumbaku”alisema Makamu wa Rais.

Mradi wa ununuzi na ufungaji wa mashine mpya za kisasa za tiba ya mionzi umegharamiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo shilingi bilioni 9.5 zimetumika.

Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha huduma za saratani hasa huduma za Kinga, Uchunguzi na Matibabu ya awali ikiwemo kuongeza vituo vya upimaji wa dalili za awali za Saratani ya mlango wa kizazi na matiti ambapo jumla ya vituo 650 vinatoa huduma hii kwa wakati.

Makamu wa Rais amewataka  wananchi wote hasa wanawake kufika katika vituo ili kufanyiwa uchunguzi  kwani zikigundulika dalili za awali mgonjwa atatibiwa na kupona.

Pia Makamu wa Rais amesisitiza wanaume waanze kuchukua mwamko wa kupima afya  zao hasa kupima saratani ya tezi dume.

“Nashukuru Wizara kwa kuanzisha kampeni ya upimaji wa virusi vya ukimwi kwa wanaume, kwa kauli mbiu ya Furaha Yangu na ingefaa suala hili liende pia kwa upimaji wa Saratani ya Tezi Dume” alisisitiza Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais ameupongeza mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kuingiza matibabu ya Saratani katika huduma ambazo wanagharimia“Ningependa kuwaagiza mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuhakikisha wanagharimia huduma hii ya tiba ya mionzi kwa LINAC.”

Wakati huohuo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema katika kipindi kifupi cha miaka mitatu sekta ya Afya imepata mafanikio makubwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo  chanjo kwa watoto zimefikia asilimia 98%, upatikanaji wa dawa muhimu ni asilimia 95%, vifaa na vifaa tiba, huduma za mama na mtoto ikiwemo ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya.

“Tumekusudia  kuleta watalii wa matibabu”alisema Waziri Ummy.  
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (kulia) wakati wa hafla ya uzinduzi wa Jengo na mashine za tiba ya saratani katika taasisi ya Saratani Ocean Road. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
 Kijana Rashid Juma Kapungu mwenye umri wa miaka 29, akitoa ushuhuda wa mafanikio baada ya kupata tiba ya mionzi katika Taasisi ya Saratani Ocean Road wakati wa hafla ya uzinduzi wa Jengo na mashine za tiba ya saratani. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa hafla ya uzinduzi wa Jengo na mashine za tiba ya saratani. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Jengo na mashine za tiba ya saratani. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipata maelezo juu ya mashine ya kisasa ya tiba ya saratani kwa mionzi kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji  wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt. Julius Maiselage wakati hafla ya uzinduzi wa Jengo na mashine za tiba ya saratani. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
 Mashine mpya za kisasa za tiba ya saratani za Linac ( Linear Accelerator) ambazo zimezinduliwa leo katika Taasisi ya Saratani Ocean Road. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad