Na Ramadhani Ali - Maelezo Zanzibar
Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dk. Fadhil Mohd Abdalla
amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuweka mikakati
ya kupunguza vifo vya watoto wachanga chini ya mwezi mmoja
vinavyotokana na maambukizi.
Aliitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuhakikisha huduma za maradhi
ya maambukizi yanayowasumbua watoto ndani ya wiki ya kwanza tokea
kuzaliwa zinatolewa katika vituo vyote vya afya badala Hospitali kuu
pekee.
Dk. Fadhil alitoa kauli hiyo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tano
ya madaktari wakufunzi kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati katika
Hoteli ya Golden Tulip Malindi.
Alisema Zanzibar imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vya watoto
wenye umri wa mwaka mmoja hadi mitatu lakini vifo vya watoto wachanga
wa siku saba za mwanzo tokea kuzaliwa bado imekuwa ni changamoto.
Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya alisema Wizara itaendelea kufundisha
Madaktari wa vituo vya ya afya msingi ili kuhakikisha kila kituo
kinaweza kutoa tiba ya maambukizi.
“Lengo ni kuhakikisha dawa za maambukizi zilizokuwa zikitolewa
Hospitali kuu sasa zinasambazwa katika vituo vya afya ili kupunguza
vifo vya watoto wachanga” alisisitiza Dk. Fadhil.
Mwakilishi wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) Ofisi ya Brazzaville
Congo, ambae ni mtaalamu wa afya ya watoto wachanga Dk. Assumpta
Muriizhi, alisema akinamama wanapitia kipindi kigumu katika kipindi
cha miaka miwili baada ya kujifungua kutokana na kupambana na afya ya
mtoto ambae hawezi kujieleza.
Alisema wapo baadhi ya wazazi hawaoni umuhimu wa kuwapeleka watoto wao
Hospitali wanapopata maambukizi jambo linapelekea kuathirika zaidi na
hatimae kupoteza maisha.
Aliwashauri akinamama wanapogundua watoto wao wachanga wanasumbuliwa
na maradhi kuwawahisha mapema vituo vya afya vya karibu kupata huduma
ya awali kabla ya kuwapelekwe Hospitali kuu iwapo matatizo
yataongezeka.
Alisema hakuna umuhimu mkubwa kwa watoto wachanga kuwaanzisha huduma
za afya katika Hospitali kuu hasa kwa Zanzibar ambapo vituo vya afya
vinapatikana kila sehemu.
Mkutano huo unahudhuriwa na Madaktari Wataalamu wa watoto wachanga
kutoka Zambia, Zimbabwe, Msumbiji, Kenya, Uganda, Tanzani Bara,
Zanzibar na Maafisa
Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa ya WHO na UNICEF.
Mwakilishi wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) Ofisi ya Brazzaville Congo Dk. Assumpta Muriizhi akizungumza na washiriki wa mafunzo ya madaktari wa watoto katika Hoteli ya Golden Tulip Malindi Mjini Zanzibar.
Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dk. Fadhil Mohd Abdalla akifungua Mafunzo ya siku tano ya madaktari wa watoto wachanga kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati katika Hoteli ya Golden Tulip Malindi Mjini Zanzibar.
Baadhi ya washiriki wa Mafunzo ya madaktari wa watoto wachanga kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati wakimskiliza Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dk. Fadhil Mohd Abdalla (hayupo pichani) alipokuwa akifungua mafunzo hayo.
Mshauri wa afya ya watoto wachanga Dk. Samira Aboubakar akijadiliana na baadhi ya washiri wa mafunzo ya watoto wachanga katika Hoteli ya Golden Tulip Malindi Mjini Unguja. 
Picha ya pamoja washiriki wa mafunzo ya siku tano ya
madaktari wakufunzi wa watotot wachanga kutoka nchi za Afrika
Mashariki na Kati na mgeni rasmin.
Picha na Makame Mshenga.
No comments:
Post a Comment