Na Teresia Mhagama, Kigoma
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amefanya ziara ya kikazi katika
Wilaya ya Kasulu, Kigoma Vijijini na Buhigwe mkoani Kigoma kwa lengo
la kukagua mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu (REA
III) ambapo pia aliwasha umeme katika baadhi ya Vijiji.
Akiwa wilayani Kasulu, Dkt Kalemani alikagua kazi zinazofanywa na
mkandarasi katika Kijiji cha Ruhita ambapo alikuta Kijiji hicho bado
hakijaunganishwa umeme na kumuagiza Mkandarasi, kampuni ya CCCE Etern
kufikisha umeme kijijini hapo baada ya siku 15.
Aidha, alimtaka Meneja wa TANESCO, Wilaya ya Kasulu kuhakikisha kuwa,
anasimamia suala ya uchoraji wa ramani za kuingiza umeme ndani ya
nyumba za wananchi kwani kuna baadhi ya watu binafsi wanaofanya kazi
hizo wamekuwa wakiwatoza wananchi gharama kubwa bila kujali tofauti ya
ukubwa au udogo wa kazi.
Vilevile, Dkt Kalemani alimtaka Meneja huyo kuhakikisha kuwa watu
wanaofanya kazi za kufunga nyaya za umeme ndani ya nyumba za wananchi
wanatambulika na TANESCO ili kuepusha utapeli na kufanya kazi chini ya
viwango vinavyotakiwa.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Simon Anange alimweleza Dkt
Kalemani kuwa, wananchi wa Kijiji hicho wamesubiri umeme kwa muda
mrefu baada ya kupata ahadi ya kupelekewa nishati hiyo, hivyo wanaomba
Mkandarasi akamilishe kazi hiyo mapema ili waweze kufanya shughuli
mbalimbali ikiwemo za kiuchumi.
Akizungumzia suala hilo, Dkt Kalemani alisema kuwa, Mkandarasi ambaye
ni kampuni ya CCCE Etern ameanza kazi mwezi Januari mwaka huu tofauti
na wanandarasi wa umeme katika maeneo mengine nchini ambao walianza
kazi mwaka jana, hii ni kwa sababu ya masuala ya kisheria
yaliyojitokeza hapo awali lakini sasa Mkandarasi huyo anaendelea na
kazi.
Akiwa wilayani Buhigwe, Dkt Kalemani alikagua miundombinu ya umeme
katika Kijiji cha Bulimanyi ambacho tayari kimeshafikishiwa umeme na
kaya zaidi ya Kumi zimeshaunganishwa na nishati hiyo na kumuagiza
Mkandarasi kupeleka umeme katika Vijiji vyote vya Wilaya hiyo.
Dkt. Kalemani pia alikagua miundombinu ya umeme katika Kijiji cha
Mkigo wilayani Kigoma Vijijini, ambapo pamoja na kuzungumza na
wananchi, aliwasha umeme katika Kijiji hicho.
Moja Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Mpigo wilayani Kigoma Vijijini mkoa wa Kigoma kabla ya kuwasha umeme katika Kijiji hicho.
Wananchi katika Kijiji cha Bulimanyi wilayani Buhigwe, Mkoa wa Kigoma
wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani)
wakati alipofika kijijini hapo kukagua miundombinu ya usambazaji
umeme.
No comments:
Post a Comment