HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 18 March 2019

KATIBU MKUU UVCCM AWATAKA VIJANA KUTUMIA VYEMA FURSA ZA UONGOZI

*Awataka kutokuwa wabeba pochi na mikoba bali wagombee nafasi za uongozi na kulitumikia taifa

Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii
KATIBU Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha  Mapinduzi (Uvccm) Mwalimu Raymond Mwangwala amewataka vijana nchini kuacha tabia ya kuwa wabeba pochi za watu kwa kusindikiza safari za uongozi kwa watu wengine  na kuwataka kuomba nafasi za uongozi kuanzia ngazi za Serikali za mitaa ambazo zipo mbioni kuelekea kwenye uchaguzi utakaofanyika  mapema mwaka huu 2019.

 Akizungumza wakati wa Uzinduzi wa Kampeni ya Dar ya Kijani yenye lengo la kutoa hamasa kwa vijana wa UVCCM kushiriki kikamilifu katika kugombea nafasi za uongozi na kurudisha mitaa yote ya Jiji la Dar es Salaam kwenye himaya yao,  Mwalimu amesema kuwa Dar lazima iwe mfano na vijana wajitokeze na kuwa sehemu ya historia ya ujenzi wa Taifa la Tanzania chini ya Jemedari mkuu na Mzalendo, Rais Dkt. John Joseph Magufuli.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na  vijana toka wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam, Mwangwala ametoa rai kwa Mikoa yote nchini  kuiga kampeni za namna hiyo zinazolenga zinazojenga Ari, hamasa na moyo wa kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi.

Aidha amewakumbusha Vijana kutumia vizuri mitandao ya kijamii kwa kuendesha kampeni mbalimbali lakini kujibia upotoshwaji unaofanywa  na upinzani. Amewataka Vijana kufanya tafiti ili kusaidia kupata ufumbuzi wa matatizo mbalimbali ili kuzidi kuendeleza taifa zaidi.

Pia ameomba kamati za maadili kuwafukuza wanachama wa CCM wanaoendekeza siasa za makundi na kuchafuana ndani ya Chama.

Mwalimu ametoa salamu za Mwenyekiti za UVCCM Taifa, Kheri James kwa wanachama hao na  kueleza kuwa kiongozi huyo mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi anavyofanya kazi usiku na mchana ili kuifanya UVCCM kubaki na heshima iliyojijengea.


Awali, akimkaribisha katibu mkuu, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dar Es Salaam, Musa Kilakala ameeleza kuwa Umoja huo umejipanga kuchukua mitaa yote ya jijini Dar es salaam kupitia kampeni hiyo ya Dar ya Kijani ambayo  itatoa majibu kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019.

Kongamano la "Ifanye Dar iwe Kijani" limeendeshwa na UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa Chuo kikuu cha Dar es salaam tawi la Elimu (DUCE.)
 Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mwalimu Raymond Mangwala akizungumza na vijana wa umoja huo kanda ya Dar es salaam katika kongamono la  Dar ya kijani, na kuwataka vijana hao kulitumikia taifa kwa kugombea nafasi za uongozi, leo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya vijana wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wakifuatilia mada katika kongamano la Dar ya kijani ambalo viongozi wa umoja huo kwa kushirikiana na wanachama hao wamejizatiti kuzitumikia vyema nafasi za uongozi katika kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. John Joseph Magufuli katika kujenga taifa, leo jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad