HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, March 7, 2019

Azam FC kuwania pointi tatu dhidi ya JKT Tanzania

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
KLABU ya Azam FC, itaingia vitani kuwania pointi tatu muhimu kwa kuvaana na JKT Tanzania, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex kesho Ijumaa saa 1.00 usiku.

Mchezo huo wa raundi ya 30, unatarajia kuwa mkali na aina yake, kikosi cha Azam FC kikiwa kwenye hali nzuri kabisa hadi sasa kikiwa kimejikusanyia pointi 53 katika nafasi ya pili kikizidiwa pointi na 11 na kinara Yanga aliyekuwa nazo 64.

Wakati Azam FC ikitoka kuichapa African Lyon mabao 3-1 kwenye mchezo uliopita, JKT yenyewe ipo nafasi ya sita kwa pointi 36 baada ya mchezo uliopita kulazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Lyon, uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Azam FC ikiwa na makocha wake wa muda, Idd Nassor Cheche na Meja Mstaafu, Abdul Mingange, wameendelea kufanya kazi kubwa ya kukisuka kikosi hicho, ambacho kimeonekana kuimarika kadiri siku zinavyosogea.

Akizungumzia mchezo huo, Cheche alisema wachezaji wana ari kubwa na wamekuwa wakifanya vema katika mazoezi jambo ambalo linampa matumaini ya kuendelea kupata matokeo mazuri kwenye mtanange huo.

“Wachezaji wana ari kubwa kuelekea mchezo huo na wamekuwa wakifurahia mazoezi, jambo ambalo linanipa matumaini ya kupata matokeo mazuri zaidi, tunaiheshimu JKT ni timu nzuri ila tumejipanga kupata ushindi kwenye mechi zetu mbili zijazo za ligi kabla ya kucheza mechi ya FA dhidi ya Kagera Sugar,” alisema.

Mabingwa hao wa ligi msimu 2013/2014 bila kupoteza mchezo wowote, wataingia kwenye mchezo huo wakimkosa kiungo wake mshambuliaji, Tafadzwa Kutinyu, ambaye atakuwa akitumikia adhabu ya kukosa mechi moja kufuatia kukusanya kadi tatu za njano.

Katika mchezo wa raundi ya kwanza ya ligi, Azam FC iliichapa JKT bao 1-0 ugenini kwenye Uwanja wa Meja Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam, bao lililofungwa na aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Yahya Zayd, aliyetimkia Ismaily ya Misri, akimalizia pande safi alilopewa na Donald Ngoma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad