HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, February 7, 2019

Balozi Seif afanya mazungumzo na Rais wa Taasisi inyosimamia mazungira kutoka UN

Rais wa Taasisi inayosimamia mazingira ya Umoja wa Mataifa Bwana Siim Valmar Kiislar amesema wakati umefika kwa Mataifa yote Ulimwenguni kuwa na mfumo Mmoja unaoeleweka wa utunzaji wa Mazingira utakaosaidia kuifanya Dunia iendelee kubakia salama.

Alisema tabia ya baadhi ya Mataifa kuendelea kukwepa mikataba na baadhi ya kanuni zinazowekwa Kimataifa pamoja na kuweka vikwazo vyenye nia ya kulinda maslahi yao binafsi vitapelekea kuongezeka kwa wasi wasi utakaoifanya Dunia hii ibakie katika mazingira hatarishi.

Bwana Siim Valmar Kiislar alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika Ofisi yake iliyomo ndani ya Jengo la Baraza la Wawakilishi liliopo Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Rais huyo akiuongoza Ujumbe mzito wa Taasisi hiyo ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa amekuja kushuhudia uzinduzi wa Kampeni ya Kidunia ya uzinduzi wa usafi wa Mazingira katika Fukwe ya Forodhani Visiwani Zanzibar ulioambatana na ujio la Mashua ya Mazingira iliyotengenezwa kutokana na malighafi ya Plastiki kutoka Nchini Kenya.

Bwana Siim Valmar ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Wananchi wake kwa umakini wao wa kusimamia masuala ya Mazingia katika kuitikia kampeni ya Kimataifa ya kupambana na mabadiliko ya Tabia Nchi.

Alisema kitendo cha Zanzibar kufanikiwa katika mapambano yake ya kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya Plastiki mbali ya kuwa mfano kwa Mataifa ya Ukanda wa Afrika Mashariki na kusini mwa Afrika, lakini pia kimeleta faraja kwa Umoja wa Mataifa kupitia Taasisi yake hiyo  inayosimamia masuala ya Mazingira.

Naye Mratibu Mkaazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayofanya kazi Nchini Tanzania Bwana Alvaro Rodriguez alisema bado Mataifa Ulimwenguni yana wajibu wa kushirikiana katika mapambano yake dhidi ya uchafuzi wa Mazingira.

Bwana Alvaro alisema ustawi wa Jamii pamoja na viumbe vilivyomo  ndani ya Dunia vitaendelea kuishi kwa amani bila ya vikwao endapo ushirikiano huo utaimarishwa na kuendelea kuwa wa kudumu kama inavyoonekana katika baadhi ya maeneo.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar bado inaendelea kuathirika na mabadiliko ya Tabia Nchi akatolea mfano ufukwe wa Bahari ya Msuka uliopo kaskazini mwa Kisiwa cha Pemba ambao tayari umeshaliwa na mawimbi ya Bahari kwa sehemu kubwa.

Balozi Seif aliueleza Ujumbe huo wa Taasisi ya Umoja wa Mataifa unaosimamia Mazingira kwamba Zanzibar imeanza mikakati ya kupiga marufuku matumizi na uingizwaji wa Mifuko ya Plastiki tokea mwanzoni mwa Miaka ya 90 na kufanikiwa vyema katika azma yake ya kulinda mazingira.

Alisema ujio wa mashua ya Mazingira katika Visiwa vya Unguja na Pemba utasaidia mfano wa Darasa kwa Wananchi waliowengi kuwa na muelekeo wa jitihada za mapambano dhidi ya mabadiliko ya Tabia Nchi yanayoikumbwa Dunia hivi sasa na kuleta athari kubwa ya Kimazingira.
 Rais wa Taasisi inayosimamia mazingira ya Umoja wa Mataifa Bwana Siim Valmar Kiislar kiipongeza Zanzibar kwa mapambano yake ya kusimamia vyema mazingira alipokuwa akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye Jengo la Baraza la Wawakilishi Chukwani.
 Balozi Seif Ali Iddi Kulia akisisitiza jambo wakati akizaungumza na  Bwana Siim Valmar Kiislar aliyewasili Zanzibar kushuhudia Uzinduzi wa usafi wa mazingira Kidunia katika Fukwe ya Forodhani.
 Balozi Seif Kulia na Mgeni wake Rais wa Taasisi inayosimamia mazingira ya Umoja wa Mataifa Bwana Siim Valmar Kiislar wakitoa nje ya Ofisi baada ya kumaliza mazungumzo yao.
 Bwana Siim Valmar Kiislar kati kati  akibadilishana mawazo na Balozi Seif baada ya mazungumzo yao huku Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed akishuhudia.
 Balozi Seif  wa Nne kutoka Kulia akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Uongozi wa Juu wa Taasisi ya Umoja wa Mataifa inayosimamia Mazingira nje ya Jengo la Baraza la Wawakilishi baada ya kumaliza mazungumzo yao. Kulia ya Balozi Seif ni Rais wa Taasisi hiyo Bwana Siim Valmar Kiislar, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed, Mratibu Mkaazi wa Mashirika ya Umoja wa Mtaifa Nchini Tanzania Bw. Bwana Alvaro Rodriguez na Ofisa wa Uratibu katika masuala ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania Bibi Clara Makenya. Kutoka Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Zanzibar Bibi Farhat Farhat Ali Mbarouk na Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mohamed Haji Hamza. Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad