HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, 6 January 2019

RAIS MAGUFULI ATUNUKIWA CHETI CHA UZALENDO NA AWAMATA

Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii
ASASI ya Uzalendo nchini (AWAMATA) imemtunuku cheti cha uzalendo Rais Dkt. John Magufuli kwa  kufanya vizuri katika kipengele cha uzalendo kwa mwaka 2018.

 Akizungumza katika  mkutano huo uliofanyika  katika ukumbi wa City Garden jijini Dar es salaam Mwenyekiti wa Asasi hiyo Chief Daudi   Mrindoko ameeleza kuwa Rais Magufuli amejitoa katika kupambana na rushwa pamoja na kuanzisha miradi mikubwa yenye lengo la kuboresha uchumi na hali ya wananchi wa kawaida, hivyo mchango wake unapaswa kutambuliwa, kuthaminiwa na kuheshimiwa. 

 Mrindoko amesema  kuwa mipango ya Asasi hiyo ipo  katika kueneza elimu ya uzalendo kwa kuanzisha chuo cha Uzalendo kitakachotoa Elimu ya Uzalendo, Ujasiriamali na kuwajengea vijana uwezo   wa kujitegemea na kuwa zao bora kwa taifa.

Pia Asasi hiyo imetoa picha maalumu ya miradi iliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli katika kipindi cha mwaka 2018 na kuelezwa kuwa kuwa kasi anayoenda na Mh. Rais ni kuleta neema kwa wananchi wengi.

Sambamba na hilo AWAMATA imetoa vyeti kwa baadhi ya  Watanzania wengine sita waliogusa wengi katika jamii kupitia  kazi zao za  kizalendo na hao ni pamoja na ; Naibu Waziri ofisi ya Makamu wa pili wa Rais Zanzibar, Juma Mihayo N’hunga ambaye mchango  umeonekana katika  kuimarisha Muungano wa Tanzania bara na visiwani.

Wengine waliopata vyeti kwa uzalendo kwa mwaka 2018 ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Homera ambaye mchango wake umetambulika katika kuboresha miundo mbinu ya Afya na elimu wilayani Tunduru hasa kwa kufanikisha ujenzi  zahanati na shule ya msingi nje ya bajeti ya serikali.

Aidha Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro amepata tuzo hiyo kutokana na mchango wake hasa kwa  kutatua matatizo ya muda mrefu ya Ardhi, pamoja na  kusaidia akina Mama kupata nyenzo na mradi wa mbuzi wilayani Arumeru.

Mkuu wa Wilaya ya Ulanga,  Ngollo Malenya aliyekuwa katibu mkuu wa Asasi kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ametunukiwa tuzo hiyo kutokana na kujitoa kwake kwa kipindi chote na kuhakikisha malengo na matarajio ya Asasi yanafanikiwa na hata  baada ya uteuzi wake bado ameendelea kuonesha kwa vitendo uzalendo kwa wananchi wa wilaya yake.

Pia tuzo nyingine imeenda kwa Mwenyekiti wa shirikisho la vyama vya walemavu Tanzania, Ummy Nderiananga ambaye amepata tuzo hiyo kutokana na  mchango wake wa kupeleka elimu ya kizalendo kwa vyama anavyoviongoza nchini kote.

Kwa upande wake msomi na  Mwanahistoria  Francis Daudi ametunukiwa tuzo hiyo kupitia makala zake za historia na uzalendo kupitia magazeti, vituo vya televisheni, Redio na katika mitandao ya kijamii ambapo makala hizo zimeonekana  kuinua moyo wa uzalendo miongoni mwa vijana wengi nchini.

 Francis Daudi ni mmoja kati ya watanzania waliowakilisha taifa kwenye mkutano mkuu wa vijana wa SADC nchini Namibia kwa mwaka 2018.

Mkutano Mkuu wa Asasi ya Wazalendo na Maendeleo nchini ulihitimishwa kwa  kumchagua  Pilly Kimario kuwa katibu mtendaji baada ya aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo  Ngollo Malenya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ulanga. 
 Cheti cha pongezi na kutambua mchango kupitia kipengele  cha uzalendo kwa mwaka 2018 kilichotolewa na taasisi ya uzalendo nchini kwa Rais Dkt.John Magufuli, jijini Dar es salaam.
 Mwenyekiti wa AWAMATA Chief Daudi Mwidadi Mrindoko (aliyeshika picha) na katibu wa taasisi hiyo Pilly Kimario(aliyeshika cheti kushoto) wakiwa kwenye picha ya Pamoja na wadau na washiriki wa mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam .
Mwenyekiti wa AMATA  Chief Daudi Mwidadi Mrindoko (aliyeketi kushoto) na katibu wa Asasi hiyo  Pilly Kimario(aliyeketi kulia)wakiwa Pamoja na wakurugenzi wapya wa Asasi waliotangazwa katika mkutano mkuu wa mwaka, jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad