HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, January 25, 2019

MAWAZIRI UGANDA NA TANZANIA KUJADILI BOMBA LA MAFUTA GHAFI

Kikao cha Nne cha Mawaziri mbalimbali kutoka Uganda na Tanzania wanaohusika na utekelezaji wa mradi wa bomba la Mafuta ghafi kutoka Hoima Uganda hadi Tanga Tanzania kinatarajiwa kufanyika leo jijini Kampala ambapo Mawaziri hao wanatarajiwa kupata taarifa za majadiliano yaliyokuwa yakifanyika kati ya Timu ya Kitaifa ya Majadiliano (GNT) ya Tanzania na Uganda ambayo yalianza Januari 21, 2019.

Kutoka Tanzania Mawaziri watakaohudhuria kikao hicho ni Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba.

Aidha Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Nishati, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pia watahudhuria kikao hicho, hii ni baada ya kufanya kikao jana na Makatibu Wakuu kutoka Wizara mbalimbali nchini Uganda wanaohusika na utekelezaji wa mradi huo hivyo Makatibu Wakuu hao ndio wataokawasilisha taarifa  kwa Mawaziri kuhusu majadiliano ya wataalam wa pande zote.

Kabla ya kufanya kikao na Mawaziri wa Uganda, Mawaziri hao kutoka Tanzania mapema leo walifanya kikao  na wataalam kutoka Taasisi mbalimbali nchini Tanzania walio katika  Timu ya Kitaifa ya Majadiliano ya Mradi huo ili kupata taarifa ya awali ya hatua ya majadiliano.

Baada ya kupata taarifa ya hatua ya majadiliano yaliyofikiwa kati ya pande hizo mbili, Mawaziri hao watajadili taarifa hiyo na endapo wataiafiki, hatua nyingine za majadiliano zitaendelea  ambazo  sasa zitahusisha Serikali ya Uganda na Tanzania na wawekezaji wa mradi ambao ni kampuni ya Total E&P  ya Ufaransa, Tullow Oil ya Uingereza, CNOOC ya China na kampuni za Mafuta za Taifa za Tanzania na Uganda.

Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima Uganda hadi Tanga Tanzania litakuwa na urefu wa kilometa 1445.
 Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati), Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi ( wa pili kushoto), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ( wa pili kulia) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba (wa kwanza kulia) wakiwa katika kikao na wataalam wa Tanzania (hawapo pichani) wanaohusika na majadiliano ya mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania.
 Wataalam kutoka Taasisi mbalimbali nchini Tanzania walio katika Timu ya Kitaifa ya Majadiliano (GNT) ya Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania wakiwa katika kikao na Mawaziri kutoka Tanzania (hawapo pichani) wanaohudhuria mkutano kuhusu mradi huo unaofanyika jijini Kampala-Uganda.
 Kikao kati ya Mawaziri  na Wataalam mbalimbali kutoka Tanzania  waliohudhuria Mkutano kuhusu mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi unaofanyika jijini Kampala-Uganda.
 Watendaji mbalimbali kutoka Tanzania wakiwa katika kikao na Mawaziri kutoka Tanzania wanaohudhuria Mkutano kuhusu mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi unaofanyika jijini Kampala Uganda.
Watendaji mbalimbali kutoka Tanzania wakiwa katika kikao na Mawaziri kutoka Tanzania wanaohudhuria Mkutano  kuhusu mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi unaofanyika jijini Kampala Uganda.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad