Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akiteta
jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bwana Bernard Konga katika
mkutano wa hadhara Halmashauri ya Wilaya ya Nanyamba Mkoani Mtwara wakati wa
uhamasishaji wa wananchi kujiunga na NHIF, kupitia Mpango wa Ushirika Afya.
Na Grace Michael
Wananchi Mkoani Mtwara wametakiwa kufanya uwekezaji kwenye afya zao
kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili wawe na uhakika wa kupata
huduma za matibabu wakati wowote. Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akizungumza na wananchi katika
Halmashauri ya Mji wa Nanyamba mkoani Mtwara.
Amesema kuwa ili kila mwananchi aweze kuwa na uhakika wa kufanya
shughuli zingine za maendeleo na uwekezaji mwingine lazima awe na
uhakika na afya yake kwa kuwa na uhakika wa kupata matibabu.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akikagua
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara.
“Nawaomba sana wananchi wa Mtwara wekezeni kwenye eneo la afya
zenu na uwekezaji mzuri ni kuwa na Bima ya Afya kupitia NHIF ili
iwawezeshe kupata huduma zote za matibabu kwa ngazi mbalimbali za
vituo vya kutolea huduma kuanzia ngazi ya Zahanati hadi Hospitali ya
Taifa,” alisema Mhe. Ummy.
Alisema kuwa Serikali imeweka utaratibu mzuri wenye gharama nafuu wa
kupata huduma za matibabu kupitia NHIF, utaratibu ambao unamtaka
mwananchi kujiunga kabla ya kuugua ili aweze kunufaika na huduma za
matibabu wakati wowote anapopatwa na maradhi.
“Wengi wetu hapa mmeuza mazao yenu na mnalipwa fedha nyingi, kati ya
fedha mnazopata hakikisheni mnatenga shilingi 76,800 tu kwa ajili ya
kukata kadi ya bima ya afya ambayo itakusaidia kupata huduma mahali
popote ndani ya nchi kwenye zaidi ya vituo 7000 vilivyosajiliwa na NHIF,”
alisema Mhe. Ummy wakati akizungumza na wananchi wa Nanyamba
Mkoani Mtwara.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu
akimhamasisha mmoja wa akina mama kumwandikisha mtoto wake na mpango wa Toto Afya
Kadi ili awe na uhakika wa kupata matibabu.
Aliwahakikishia wananchi upatikanaji wa huduma za matibabu katika
hospitali zote nchini kutokana na maboresho makubwa yaliyofanyika chini
ya Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imeongeza kwa kiasi kikubwa bajeti
ya afya hususan bajeti ya dawa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya,
Bwana Bernard Konga alisema kuwa, Mfuko umejipanga kuhakikisha
unawafikia wananchi wote katika maeneo yao na kuwasajili ili waweze
kuwa kwenye utaratibu rahisi wa kupata huduma za matibabu.
“Tumeweka mazingira rahisi ya upatikanaji wa huduma za matibabu, tunao
wigo mpana wa vituo vya kutoa huduma kwa wanachama wetu hivyo
tumejipanga kuwafikia katika maeneo yenu ili tuwasajili na muanze
kunufaika na huduma zetu ambazo unaweza ukazipata wakati wowote hata
ambao hauna fedha,” alisema Bw. Konga.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akiendelea
na uhamasishaji wa wananchi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Bw. Evod Mmanda aliupongeza Mfuko
kwa kuanzisha mpango wa Ushirika Afya ambao unawawezesha wakulima
kunufaika na huduma za matibabu kwa gharama nafuu.
Mheshimiwa Waziri Ummy yuko mkoani Mtwara kwa ziara ya siku tatu,
ambapo mbali na kutembelea vituo vya kutolewa huduma atazungumza na
wananchi na kuwahamasisha kujiunga na Bima ya Afya ili kila mwananchi
awe na uhakika wa kupata matibabu.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu
akiwaeleza wananchi umuhimu wa kujiunga na NHIF.
Viongozi wa Vyama vya Ushirika katika Halmashauri ya Nanyamba wakimsikiliza Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu juu ya kujiunga na NHIF,
kupitia Mpango wa Ushirika Afya.
Ufafanuzi wa masuala ya namna ya kujiunga na huduma za NHIF ukiendelea.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu na
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga wakijibu maswali ya wananchi juu ya huduma za
NHIF.
No comments:
Post a Comment