Afisa mtendaji mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja ametoa ahadi ya kupeleka maji Bonyokwa wakati wa ziara ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof. Makame Mbarawa.
Prof Mbarawa amefanya ziara ya kusikiliza kero za wananchi kuhusiana na huduma ya Maji katika eneo hilo.
Mhandisi Luhemeja ameeleza kuwa eneo hilo limekosa huduma ya Maji kwa muda mrefu kutokana na kukosa chanzo cha Maji cha Karibu na hivyo DAWASA imeamua kulaza bomba kubwa litakalo chukua Maji kutoka mtambo wa uzalishaji Maji wa Ruvu juu ili kuhudumia wakazi wa eneo hilo.
“Sisi DAWASA tutaleta huduma ya Maji hapa Bonyokwa kwa kuwa ni muda mrefu mmeteseka na tatizo kubwa la eneo hili ni kukosa chanzo cha Maji cha kuhudumia hapa kutokana na jiografia yake ila sasa tumeamua kutoa Maji kutoka mtambo wa Ruvu juu na kuyaleta hapa, tayari pia baadhi ya vifaa vimefika hapa na kuanzia Siku ya Jumatatu tutaanza kazi rasmi ya kulaza mabomba hivyo wananchi mjitokeze kwa ajira uchimbaji mitaro” alisema mhandisi Luhemeja.
Aidha Prof. Makame Mbarawa katika mkutano huo amewatoa wasiwasi wakazi wa eneo hilo kwa kuwaeleza kuwa atahakikisha DAWASA inafikisha huduma ya Maji kwa wakati na kumuagiza meneja wa DAWASA Mkoa wa Tabata kusimamia hilo.
Pia amebainisha kuwa lengo la serikali ni kufikisha huduma ya Maji safi kwa asilimia tisini na tano kwa maeneo yaliyopo mijini kufika 2020.
Kwa niaba ya wakazi wa eneo hilo Meya wa Ilala na Diwani wa eneo hilo Charles Kwiyeko ameshukuru jitihada za serikali pamoja na DAWASA zakutaka kufikisha huduma ya Maji kwa kuwa ni kero kubwa na ya muda mrefu kwa wananchi wake.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof Makame Mbarawa akizungumza na wananchi wa Bonyokwa na kuwaondoa hofu na kuwahakikishia watapata maji kwenye maeneo yote yaliyokuwa hayana maji.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja akiwa anatembelea maeneo ya Bonyokwa akiwa ameambatana na Meneja wa DAWASA Tabata na Diwani wa kata hiyo.
Wananchi mbalimbali waliofika katika mkutano huo.
No comments:
Post a Comment