HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, December 21, 2018

WAKURUGENZI WA SERA NA MIPANGO NA MAAFISA UTUMISHI WAANDAMIZI WAJENGEWA UWEZO WA MASUALA YA WATU WENYE ULEMAVU

Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na SHIVYAWATA wametoa mafunzo ya kuwajengea uwezo Wakurugenzi wa Sera na Mipango na Maafisa Utumishi Waandamizi juu ya masuala ya Watu wenye Ulemavu.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Bw. Peter Kalonga amesema kuwa masuala ya Watu wenye Ulemavu ni mtambuka, hivyo ili kuifikia jamii jumuishi ni vyema kuhakikisha masuala ya wenye Ulemavu yanajumuishwa vyema katika mipango mkakati wa kila sekta.

“Sera ya Taifa ya huduma na maendeleo kwa Watu wenye Ulemavu pamoja na Sheria ya Watu wenye Ulemavu zinasisitiza ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika nyanja mbalimbali za kijamii.” Alisema Kalonga. Aliongeza kuwa, Nchi yetu iliridhia Mkataba wa Kimataifa wa haki za Watu wenye Ulemavu wa mwaka 2006 unaotoa tafsiri ya mambo mbalimbali kuhusu haki za Watu wenye Ulemavu na kupelekea kutungwa Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010 ili kufanikisha utekelezaji wa mkataba huo na kukuza haki za watu wenye ulemavu nchini.

Aidha alitoa wito kwa Wakurugenzi na Maafisa Utumishi kuzingatia na kuyapa uzito unaostahili masuala ya Watu wenye Ulemavu ili kufanikisha ukondoishaji wa wenye Ulemavu katika sekta mbalimbali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) Bi. Ummy Nderiananga alisema kuwa ushirikiano baina na vyama vya watu wenye ulemavu na wadau mbalimbali umeleta mafanikio makubwa nchini hususan kwenye elimu, ajira, afya, uchumi, miundombinu na ushirikishwaji wa Watu wenye Ulemavu katika nyadhifa mbalimbali.

“Miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia mabadiliko chanya katika masuala ya Watu wenye Ulemavu na yanaleta matumaini kutokana na upatikanaji wa haki za Watu wenye Ulemavu nchini.” alisema Nderiananga.

Lengo la mkutano la mkutano huo ni kuwajengea uwezo Wakurugenzi na Maafisa Utumishi Waandamizi ngazi ya Wizara juu ya Sera, Sheria na Miongozo ya masuala mbalimbali yanayohusu Watu wenye Ulemavu, Kuweka mkakati wa kufanyakazi pamoja na kupata taarifa za mipango ya utekelezaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu kutoka sekta zinazotekeleza afua mbalimbali kwa Watu wenye Ulemavu.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bw. Peter Kalonga akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo wakati wa mkutano wa kuwajengea uelewa Wakurugenzi na Maafisa Utumishi Waandamizi ngazi ya Wizara juu ya masuala ya Watu wenye Ulemavu yaliyofanyika Disemba 21 na 22, 2018 Jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) Bi. Ummy Nderiananga akiwasilisha mada juu ya ujumuishwaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu.
Afisa Ustawi wa Jamii Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bi. Josephine Lyengi akelezea jambo kuhusu ukondoishwaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu.
Baadhi ya washiriki wakimsikiliza hotuba ya Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bw. Peter Kalonga (hayupo pichani).
Baadhi ya washiriki wakifuatilia mada zilizokuwa zinawasilishwa wakati wa mkutano huo uliofanyika katika hoteli ya Nashera, Jijini Dodoma.
Mjumbe kutoka SHIVYAWATA, Bw. Felician Mkude akiwasilisha mada kwa Wakurugenzi na Maafisa Utumishi Waandamizi ngazi ya Wizara juu ya masuala ya Watu wenye Ulemavu.
Afisa Uchumi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bi. Fatuma Urari akichangia mada wakati wa mkutano huo uliowakutanisha kujadili ukondoishaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu.
Mkurugenzi Msaidizi wa Sera kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bi. Graceana Shirima akichangia mada wakati wa mkutano huo.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bw. Peter Kalonga (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wakurugenzi wa Sera na Mipango, Maafisa Utumishi Waandamizi na Wawakilishi kutoka Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu (SHIVYAWATA). PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad