HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, December 1, 2018

UJENZI WA KAMPASI BOKO KUONGEZA IDADI YA KOZI HKMU

Na Karama Kenyunko, Blogu ya jamii
CHUO Kikuu cha kumbukumbu ya Hubert Kairuki cha jijini Dar es Salaam, kipo mbioni kujenga kampasi mpya katika eneo la Boko, mradi ambao utaanza mapema mwakani baada ya kukamilika kwa hatua za mwisho za kupata mkopo kutoka katika taasisi ya Norweigian Gurantee Export Credits (GIEK.)

Akizungumza wakati wa mahafali ya 16 katika ngazi mbalimbali za uuguzi na udaktari yaliyofanyika leo Desemba Mosi ,2018 katika viwanja vya chuo hicho jijini Dar es Salaam Makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa  Charles Mgone amesema kuwa ujenzi wa Kampasi hiyo mpya utaongeza idadi ya wadahiliwa pamoja na kuongeza idadi ya kozi zitakazotolewa. Aidha amesema kuwa  kwa mwaka huu jumla ya wanafunzi 230 wamehitimu na kutunukiwa shahada mbalimbali na kati ya hao wanaume 104 na wanawake 126 ambao wametunukiwa astashahada, stashahada na shahada.

Amesema kuwa kwa Astashahada ya uuguzi wapo wahitimu 11, stashahada ya uuguzi wahitimu 21, shahada ya udaktari wa binadamu wahitimu 153, shahada ya uuguzi wahitimu 32, shahada ya uzalimili  ya ustawi wa jamii wahitimu 3, shahada ya uzamili wa sayansi ya afya ya jamii wahitimu 2, shahada ya uzamili ya magonjwa na afya za watoto wahitimu 5 na shahada ya uzamili ya Magonjwa ya akina mama wahitimu 3. Mgone amesema kuwa  na kwa mwaka huu wa masomo 2018/2019 wamedahili wanafunzi wapya 293 na chuo kimeendelea kufadhili masomo kwa walimu ngazi ya uzamili na uzamivu na hadi sasa wana walimu 4 wanaosomea shahada ya uzamivu na 3 shahada ya uzamili katika fani mbalimbali.

Kuhusiana na mafanikio ya chuo hicho Mgone amesema kuwa mpango wa ujenzi wa kampasi mpya ni moja ya jambo wanalojivunia pamoja na kuunganishwa na huduma ya intaneti bure bila malipo kupitia mtandao wa Uhuru One ambao husaidia wanafunzi kusoma kisasa na wahadhiri kutoa mafunzo kwa kutumia teknolojia, pia ameeleza kuwa wanajivunia heshima iliyoletwa na mwanafunzi wa uuguzi chuoni hapo Grace Msemwa kwa kutunukiwa tuzo ya Malkia kutoka Clouds Media Group na hiyo ni baada ya kuwasaidia akina mama kujifungua salama na kuanzisha kampeni ijilikanayo Mkunga Nyumbani Kwako.

Pia amewataka wahitimu kuwa na nidhamu, utayari na kujali maadili ya taaluma zao na amewasihi kutumia vyema mafunzo waliyoyapata chuoni hapo na kuwa mabalozi wazuri  kwa kuwahudumia na kujenga taifa kwa weledi na ujali watu watakaowahudumia. Mkuu wa wa chuo Dkt. Salim Mohames Salim amewatunuku shahada wahitimu 230 na amewapongeza wahitimu kwa kufanya vizuri katika masomo yao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho John Ulanga amesema, juhudi kubwa zinazofanywa na bodi ya wakurugenzi wa shirika la Afya na Elimu la Kairuki(KHEN) wajumbe wa bodi na wajumbe wa baraza la huo zimekuwa ni chachu na kufanya ongezeko endelevu la udahili wa wanafunzi. Amesema, juhudi za chuo hicho zitaboreshwa zaidi na kufanya chuo hicho kuendelea kuwa bora nchini na hata Afrika nzima kwa ujumla.

Aidha Ulanga  ameshukuru mchango Mkubwa wanaopata kutoka kwa Serikali, Taasisi, walezi, Wazazi na wadau wote wanaochangia maendeleo katika chuo hicho na kufanya ubora wake katika ngazi zote za elimu kuongezeka.

Aidha amezishukuru taasisi za Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Taasisi za Umma, Binafsi na wadau wengine wa maendeleo kwa michango yao mbali mbali katika kuhakikisha wanasimamia ubora wa elimu hapa nchini na mwaka hui chuo kimeweza kutambulika na baraza la Vyuo Vikuu ya Afrika Mashariki ( IUCEA)  ambacho kimechagua chuo cha HKMU kuwa mwakilishi wa vyuo binafsi kwenye baraza la vyuo Vikuu Afrika Mashariki kwa miaka miwili.
 Mwenyekiti wa baraza la chuo kikuu cha kumbukumbu ya Hubert Kairuki, John Ulanga akizungumza wakati wa mahafali ya 16 katika ngazi mbali mbali za uuguzi na udaktari yaliyofanyika leo Desemba Mosi, 2018 katika viwanja vya chuo hicho jijini Dar es Salaam.
 Makamu mkuu wa Chuo kikuu cha kumbukumbu ya Hubert Kairuki Profesa Charles Mgone, akizungumza wakati wa kuhudhurisha na kutunuku wahitimu 230 waliohitimu mwaka huu ambapo ameeleza kuwa wana mpango wa kujenga kampasi mpya itakayoongeza idadi ya wanafunzi na kozi zitakazotolewa wakati wa mahafali ya 16 katika ngazi mbali mbali za uuguzi na udaktari yaliyofanyika leo Desemba Mosi, 2018 katika viwanja vya chuo hicho jijini Dar es Salaam. (Picha na Bakari Madjeshi, Blogu ya jamii)
 Mkuu wa chuo kikuu cha kumbukumbu ya Hubert Kairuki Dkt. Salim Mohamed Salim (kulia) akiteta jambo na Makamu mkuu wa hicho hicho Profesa Charles Mgone wakati wa mahafali ya 16 katika ngazi mbalimbali za uuguzi na udaktari yaliyofanyika leo Desemba Mosi, 2018 katika viwanja vya chuo hicho jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya wahitimu waliotunukiwa astashahada, stashahada, shahada za awali na shahada za uzamili kutoka chuo kikuu cha kumbukumbu ya Hubert Kairuki wakati wa mahafali ya 16 katika ngazi mbalimbali za uuguzi na udaktari yaliyofanyika leo Desemba Mosi, 2018 katika viwanja vya chuo hicho jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad