HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, December 1, 2018

Kituo cha Pamoja cha Ukaguzi Namanga Kuiingizia Tanzania Bil. 58 Mwaka Huu wa Fedha

Na: Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma.
Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli amesema kituo kipya cha ukaguzi Namanga kinatarajia kuingizia Tanzania Shilingi Bil. 58 mwaka huu wa fedha, 2018/2019. Rais Magufuli ameyasema hayo leo Namanga, Jijini  Arusha wakati wa ufunguzi wa kituo hicho uliofanyika mpakani mwa Tanzania na Kenya.

Rais Magufuli amesema, kukamilika kwa kituo hicho kumeongeza mapato kutoka wastani wa shilingi Bil. 3 kwa mwezi hadi shilingi Bil. 4.5 kwa mwezi ambapo kwa mwaka huu wa fedha Serikali ya Tanzania inatarajia kukusanya jumla ya shilingi Bil. 58 kutoka katika kituo hicho.

"Ujenzi wa vituo vya huduma za pamoja mipakani vimerahisha huduma za usafiri na kupunguza gharama za muda.Zamani watu walikuwa wakitumia siku nzima kuvuka mpaka, lakini sasa hivi mtu anatumia dakika 15 tu kuvuka mpaka huo," amesema Rais Magufuli.

Amesema, kituo hicho kitawawezesha wafanyabiashara kuvusha bidhaa zao zaidi ya mara  Kumi kwa mwezi tofauti na ilivyokuwa mwanzo ambapo ilikuwa nadra kwa mfanyabiashara kuvuka mpaka huo hata mara Nne kwa mwezi.

Aidha amesema, kituo hicho kitaimarisha shughuli za biashara na utalii kwa nchi zote mbili kutokana na kurahisishwa kwa huduma ya usafiri pamoja na miundombinu mingine katika kituo hicho.

Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta amesema ni jukumu lao viongozi kuhakikisha wananchi wanafanyabiashara bila kupingwa na waweze kuimarisha biashara kati ya nchi hizo mbili. Amesema dhumuni la ujenzi wa kituo hicho ni kuwarahisishia wafanyabiashara wadogo na wakubwa kufanya biashara zao kwa urahisi, ili kila mwana jumuiya wa Afrika Mashariki aweze kunufaika na umoja huo.

Aidha amewataka wale wote waliopewa jukumu la kusimamia kituo hicho basi wajue kazi yao sio kumnyanyasa mwananchi bali kumsaidia mwananchi afanye biashara yake. Pia wananchi wajue kuwa wakisaidiwa kufanya biashara hawajaambiwa kufanya biashara ya madawa ya kulevya, kuua wanyama au biashara ya magendo bali wanatakiwa kufanya biashara ya haki ili mtu apate fedha yake ya haki.

Nae, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe Balozi Dkt. Augustine Mahige amesema, kuwa na kituo kimoja cha forodha na uhamiaji kinaboresha soko la pamoja la Afrika Mashariki. Vile vile amesema, baada ya soko la pamoja, Jumuiya ya Afrika Mashariki inajiandaa kuwa na sarafu moja ifikapo 2020.

Kituo cha pamoja Namanga kimejengwa kwa ufadhili wa nchi ya Japani kupitia Shirika la Maendeleo la JICA ambapo kwa upande wa Tazania jumla ya shilingi Bil. 18.6 zimegharamiwa . Aidha Benki ya Maendeleo ya Afrika imefadhili kiasi cha Dola za Marekani 117,000 kwa ajili ya kuweka vifaa vya ofisi kwa upande wa Tanzania na Kenya.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia wanachi wa Kenya na Tanzania katika eneo la Mpakani Namanga mara baada ya hafla ya ufunguzi wa Kituo cha Kutoa huduma kwa pamoja mpakani Namanga One Stop Border Post (OSBP) upande wa Tanzania na Kenya.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad