HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, December 18, 2018

Tume yatangaza Uchaguzi mdogo katika Kata za Biturana, Kibondo na Mwanahina Meatu

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo wa kata mbili utakaofanyika tarehe 19 Januari 2019 sanjari na uchaguzi mdogo wa Jimbo la Temeke na Kata 46 za Tanzania Bara uliotangazwa awali.

Akitoa taarifa kwa umma Jijini Dar es Salaam leo (Jumanne), Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji (Rufaa) Mbarouk Salim Mbarouk amezitaja kata hizo kuwa ni pamoja  na Mwanahina iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Mkoani Shinyanga  na Kata ya Biturana katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma. 

“Fomu za Uteuzi wa Wagombea zitatolewa kati ya  tarehe  21  hadi tarehe 27, Disemba mwaka huu. Uteuzi wa Wagombea utafanyika tarehe  27, Disemba mwaka huu. Kampeni za Uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 28, Disemba mwaka huu hadi tarehe 18 Januari 2019  na Siku ya Uchaguzi itakuwa ni tarehe 19  Januari 2019,” alisema Jaji Mbarouk.

Jaji Mbarouk aliongeza kwamba Uchaguzi wa Kata hizo ambao unafanyika kutokana na kujiuzulu uanachama kwa madiwani waliokuwepo awali utafanyika pamoja na uchaguzi wa Jimbo la Temeke na Kata 46 za Tanzania Bara, kama ilivyotangazwa hapo awali.

Akitoa wito kwa vyama vya siasa, Jaji Mbarouk alisema “Tume inapenda kuvikumbusha Vyama vya Siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na maelekezo yanayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa kipindi chote cha Uchaguzi huu mdogo”.

Alisema Tume imetangaza nafasi hizo wazi baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa ambaye kwa kutumia mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, aliitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi za Madiwani katika Kata hizo.

“Kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatoa taarifa kwa Umma kuhusu uwepo wa Uchaguzi mdogo wa Udiwani katika Kata tajwa zilizopo katika Halmashauri za Meatu na Kibondo,” Jaji Mbarouk alisema.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad