HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 10, 2018

SERIKALI HAITOMVUMILIA KIONGOZI ATAKAYEKIUKA MAADILI-MAJALIWA

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuenzi misingi ya utawala bora haitamvumilia kiongozi yeyote wa umma atakayekiuka misingi hiyo na kutanguliza maslahi binafsi badala ya maslahi ya umma katika utendaji wake.

Amesema mgongano wa maslahi umechangia rasilimali za nchi kunufaisha watu wachache huku wananchi wengi kuendelea kuwa fukara, wakati wachache wakijitajirisha isivyo halali, hivyo Serikali itaendelea kuziba mianya, kwani ikiachiwa iendelee, itarudisha nyuma jitihada za Serikali katika kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema mmomonyoko wa maadili umechangia sana kutozingatiwa kwa sheria, kanuni na miongozo mbalimbali katika utumishi wa umma, tatizo ambalo limesababisha mgongano wa maslahi.

Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Desemba 10) kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu yaliyofanyika Kitaifa jijini Dodoma, ambapo ametumia Napenda fursa hiyo kuwaasa viongozi wote kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika utendaji wao kwani hiyo ndio njia pekee itakayoepusha mgongano wa maslahi.

Waziri Mkuu amesema mgongano wa maslahi ni miongoni mwa mambo yaliyochangia kuisababishia hasara Serikali kwa muda mrefu, tatizo ambalo lazima lidhibitiwe kwani mara kadhaa baadhi ya viongozi au watumishi wa umma wamekuwa wakifanya maamuzi kwa mambo wanayojua wazi kuwa wana maslahi binafsi nayo.

”Mathalan katika Halmashauri zetu wapo madiwani au watumishi wanaoshiriki kutoa maamuzi yanayohitimishwa kwa kumpatia kazi mkandarasi au mzabuni wakati kampuni husika inamilikiwa na mwenza, rafiki, ndugu wa karibu au mtoa rushwa.”

Amesema mgongano wa maslahi ambapo amesema kuwa huwa unatokea pale mahitaji, manufaa na faida (maslahi) binafsi ya kiongozi yanapokinzana na yale ya umma katika utendaji wake wa kazi, jambo ambalo ni kinyume na misingi ya utawala bora ambayo Taifa letu linaiamini na kuifuata tangu lilipoanzishwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.”

Amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli itaendelea kuunga mkono na kutekeleza Mikataba na Makubaliano ya Kimataifa ipasavyo. Mikataba hiyo ni pamoja na mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Makubaliano yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu.

”Sambamba na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi katika ibara ya 145 (a), ambapo tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, mojawapo ya agenda yetu ilikuwa ni kuendeleza jitihada za kukuza, kulinda na kuhifadhi haki za binadamu na utawala wa sheria katika ngazi zote za uongozi.

Jambo hili tumelifanya kwa nguvu kubwa na kwa sasa tumeona kuna mabadiliko makubwa sana miongoni mwa watumishi wa umma katika kutoa huduma kwa wananchi kwa nidhamu, bila upendeleo na kuepuka vitendo vya rushwa.”

Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha miaka mitatu yameshuhudiwa mafanikio makubwa nchini na kwamba hakuna muujiza uliofanyika kufikia hatua hiyo, bali ni usimamiaji wa nidhamu ya kazi, uadilifu na rasilimali za nchi.

Amesema kinachofanywa na Serikali ni kuchukua hatua stahiki dhidi ya vitendo vyote vinavyokiuka maadili na misingi ya utawala bora kadri inavyowezekana na sasa mafanikio ya jitihada hizo yanaonekana, ambapo baadhi ya watumishi wa umma waliishakuwa miungu watu  na  kusahau kabisa  kwamba  utumishi  wao  ni wa  kuwatumikia  Watanzania,

”Mafanikio ya hatua hizo ni kurejea kwa  nidhamu katika utumishi wa umma, kushuka kwa mfumuko wa bei za bidhaa, kuendelea kutekelezwa kwa miradi ya maendeleo na kuimarika kwa utamaduni wa kufanya kazi halali ili kupata kipato halali hivyo, kufuta maisha yaliyojaa ujanja ujanja.”

Hivyo, Waziri Mkuu amesema maadhimisho hayo ni muhimu kwa sababu yanatoa fursa ya Serikali kujitathmini kama imefanya juhudi za kutosha kuhakikisha maadili yamezingatiwa katika kila eneo na hivyo kupunguza vitendo vya rushwa, kuimarisha uwajibikaji katika kuutumikia Umma na misingi ya utawala bora kwa ujumla wake.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Spika wa Bunge Job Ndugai, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapteni MstaafuGeorge Mkuchika, Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Paramagamba Kabudi.

Wengine ni Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu Wakuu wa Taasisi zinazosimamia Maadili, Haki za Binadamu, Uwajibikaji na Mapambano dhidi ya Rushwa, Viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na Wawakilishi wa Washirika wa Maendeleo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Waziri Mkuu na Bunge), Maimuna Tarishi wakati alipowasili kwenye ukumbi wa LAPF jijini Dodoma kuzungumza na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Desemba 10, 2018. Wengine pichani kutoka kushoto ni Waziri wa Nchil Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavinde na kulia ni  Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu, Profesa, Faustine  Kamuzora. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad