HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, December 18, 2018

SERENGETI BOYS KUSHIRIKI MASHINDANO NCHINI UTURUKI

TIMU ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys inatarajia kushiriki mashindano maalumu ya maandalizi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) U17 mjini Antalya nchini Uturuki Februari mwakani.


Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka Miguu Afrika (CAF) kwa ushirikiano na Shirikisho la Soka Ulaya UEFA yataanza Februari 22 hadi Machi 2, mwakani na yatashirikisha jumla ya timu 12 kutoka Afrika na Ulaya.

Mbali na Serengeti Boys nchi nyingine za Afrika zitakazoshiriki katika mashindano hayo ni pamoja na Angola, Morocco, Cameroon, Uganda, Nigeria, Senegal na Guinea ambazo zitaungana na timu 4 kutoka Bara la Ulaya.



‬Serengeti Boys itakwenda kwenye michuano hiyo ikitoka kutwaa ubingwa wa michuano ya U17 Kusini mwa Afrika (COSAFA) baada ya ushindi wa penalti 6-5 dhidi ya Angola kufuatia sare ya bao 1-1, kwenye mchezo wa fainali juzi mjini Gaborone nchini Botswana.

Katika dakika 120 za mchezo huo, Angola walitangulia kwa bao la Morais kabla ya Tanzania kusawazisha kupitia kwa Kelvin Pius dakika ya 78.Na baada ya mchezo huo, Nahodha wa Tanzania, Michael Morice alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa mechi.

Tanzania iliyo chini ya kocha Oscar Milambo ilifika hatua hii kwa ushindi wa matuta pia, ikiitoa Zambia kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 1-1 pia. 

Awali, katika mechi za Kundi B, Serengeti Boys ilizifunga Malawi 2-1 na Afrika Kusini 2-0 baada ya kufungwa 2-0 na Angola, hivyo kufanikiwa kuingia Nusu Fainali.
Kikosi cha Serengeti Boys kinachojiandaa kwa fainali za Afrika za U17 Mei mwakani ambazo watakuwa wenyeji katika Jiji la Dar es Salaam.
Nahodha wa timu ya Vijana Serengeti Boys Michael Morice akikabidhi kombe kwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe baada ya kutwaa ubingwa wa michuano ya U17 Kusini mwa Afrika (COSAFA) walipowasili Uwanja wa ndege jana.
Wachezaji  Michael Morice na Kelvin John wakiwa na tuzo zao.










No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad