HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 5 December 2018

Operesheni Nzagamba Awamu ya Pili yaondoa watumishi wazembe Kibaha

                        Na Frank Mvungi- MAELEZO
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina ameagiza Kuondolewa mara moja kwa watumishi wa Wanaosimamia Kituo cha Ukaguzi Kibaha Mkoani Pwani kwa kushindwa kusimamia rasilimali za Sekta ya Mifugo na Uvuvi. Akizungumza leo Jijini Dodoma wakati  wa kikao cha Tathmini ya Operesheni Nzagamba Awamu ya Pili iliyofanyika  kati ya mwezi Oktoba na Novemba 2018 ikilenga Kuinua mchango wa Sekta ya Mifugo katika Pato la Taifa Waziri Mpina amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali yatokanayo na biashara ya Mifugo na Mazao yake.

“ Watumishi wote walioshiriki katika Operesheni Nzagamba Awamu ya Pili wamefanya kazi kubwa na kwa uzalendo mkubwa hivyo nawapongeza kwa kuwa mmeonesha kuwa tunao uwezo wa kusimamia rasilimali zetu ili zitoe mchango stahiki katika pato la Taifa”.Alisisitiza Mhe. Mpina. Akifafanua amesema watumishi wasio waadilfu na wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao hawana nafasi katika Wizara hiyo ndio maana ameagiza kuondolewa mara moja kwa watumishi wanaofanya kazi ya ukaguzi wa rasilimali hizo katika kituo cha Kibaha.
Aliongeza kuwa Operesheni Nzagamba awamu ya Pili, 2018 imedhihirisha kwamba usimamizi thabiti wa Sheria, Kanuni na Taratibu katika Sekta ya Mifugo unaweza kuleta tija kwa kuongeza uzalishaji bora wa mazao ya mifugo ambayo ni malighafi ya Viwanda na hivyo kuchangia ipasavyo katika kuendeleza uchumi wa Viwanda.

“ Ni mategemeo yangu kuwa wananchi mtakuwa wazalendo kwa nchi yetu kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za Kufanya biashara ya mifugo pia kutoa taarifa pale mnapobaini utoroshaji wa mifugo kwenda nchi jirani bila kulipiwa ushuru na tozo stahiki ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya watu hao”. Alibainisha Mhe. Mpina. Pia aliwaasa Watumishi wa Wizara hiyo na wale wa Halmashauri kuhakikisha kuwa wanasimamia kwa makini utekelezaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu zote zinazosimamia biashara ya Mifugo na Mazao yake hususan mabadiliko ya Kanuni mpya iliyotolewa mwezi Agosti, 2018.

Katika kuhakikisha minada yote ya awali na ile ya Upili pamaoja na ile ya mipakani inatoa matokea chanya, Waziri Mpina amesema kuwa  usimamizi utaendelea kuimarishwa ili kuwezesha biashara ya mifugo kufanyika kwa ufanisi na hivyo kurahisisha ukusanyaji wa maduhuli, tozo na ushuru wa Serikali. Alizitaka Mamlaka zinazotoa Leseni kwa wafanyabishara wanaosafirisha Mifugo nje ya nchi kuweka utaratibu rafiki utakaosaidia  kundi hilo kutoa mchango wake katika ujenzi wa Taifa na kuondoa au kupunguza vitendo vya biashara ya magendo. Aidha Waziri Mpina aliagiza kufunguliwa kwa Ofisi za Kanda ili kuimarisha usimamizi wa rasilimali za mazao ya mifugo hapa nchini.

Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kuwa Operesheni hiyo ilishirikisha watendaji 152 waliogawanyika katika timu 14 zilizofanya kazi katika nchi nzima. Akizungumzia mafanikio ya Operesheni hiyo amesema kuwa kwa mfano katika Mji wa Bunda zilikuwa zikikusanywa shilingi milioni mbili na nusu  (2.5) hapo awali ambapo kwa sasa baada ya kuimarisha ukusanyaji mapato katika eneo hilo yamefikia milioni nane  (8)kwa siku.

Udhibiti wa Biashara ya Mifugo na Mazao yake uliofanyika kupitia Operesheni Nzagamba II kuanzia tarehe 11 Oktoba, 2018 hadi tarehe 30 Novemba, 2018 (siku 50) umeiwezesha Wizara yangu kupitia Sekta ya Mifugo kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 5,773,074,768. Makusanyo haya yanapelekea Wizara hiyo katika sekta ya Mifugo tu kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 9,764,241,926.28 kwa kipindi cha Julai hadi Novemba, 2018 sawa na asilimia 52.87 ya lengo lililowekwa na Wizara ya Fedha.
 Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Luhaga Mpina akifuatilia uwasilishwaji wa Taarifa ya Tathmini ya Matokeo ya Operesheni Nzagamba awamu ya pili  leo Jijini Dodoma.Kulia kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof Elisante Ole Gabriel,Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi Mhe.Abdallah Ulega na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Prof Siza Tumbo.     
 Baadhi ya Maafisa wa Polisi walioshiriki  Operesheni Nzagamba awamu ya pili  wakifuatilia kwa makini Hotuba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Luhaga Mpina (hayupo          
     Viongozi mbalimbali wa "Comand Post" zilizotumika kuongoza Operesheni Nzagamba awamu ya pili  (Mstari wa mbele) wakifuatilia uwasilishwaji wa Taarifa ya Tathmini ya Matokeo ya Operesheni kutoka kwa Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko Dk Felix Nandonde kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi(hayupo Pichani) katika Ukumbi wa St.Gasper  Jijini Dodoma.
 Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Luhaga Mpina akiwa pamoja na Naibu Waziri wa  Mifugo na Uvuvi Mhe.Abdallah Ulega na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof Elisante Ole Gabriel wakati wa uwasilishwaji wa Taarifa ya Tathmini ya Matokeo ya Operesheni Nzagamba awamu ya pili  leo Jijini Dodoma.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof Elisante Ole Gabriel akizungumza wakati wa uwasilishwaji wa Taarifa ya Tathmini ya Matokeo ya Operesheni Nzagamba awamu ya pili  katika ukumbi wa St.Gasper Leo Jijini Dodoma. 
  Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko Dk Felix Nandonde kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi akiwasilisha Taarifa ya Tathmini ya Matokeo ya Operesheni Nzagamba awamu ya pili  leo Jijini Dodoma.
 Viongozi  14  wa timu zilizokuwa zinaongoza utekelezaji wa Operesheni Nzagamba awamu ya pili  wakieleza makusanyo waliyofikia mara baada ya Operesheni hiyo kuisha, leo katika ukumbi wa St.Gasper leo  Jijini Dodoma. 
 Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Luhaga Mpina akizungumza wakati wa uwasilishwaji wa Taarifa ya Tathmini ya Matokeo ya Operesheni Nzagamba awamu ya pili leo Jijini Dodoma.
Picha na MAELEZO.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad