Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu
akionyesha kitambulisho cha matibabu kupitia mpango wa Ushirika Afya kabla ya kukabidhi kwa
wanachama waliojiunga kwenye kampeni ya uhamasishaji aliyoifanya katika Mkutano wa
hadhara katika eneo la Kitangali Wilaya ya Newala.
Na Grace Michael, Tandahimba
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umesema unaanza rasmi kampeni
ya uandikishaji ya kijiji kwa kijiji katika Mikoa ya Mtwara na Lindi ili
kuwawezesha wananchi hao kuwa kwenye utaratibu mzuri wa kupata
huduma za matibabu.
Imeelezwa kuwa, wananchi wamekuwa wakiingia katika umasikini mkubwa
kwa kulazimika kuuza mali za familia kwa lengo la kupata fedha za
kugharamia huduma za matibabu.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga
wilayani Tandahimba ambaye alikuwa miongoni mwa watendaji
walioambatana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu katika ziara yake ya kutembelea vituo vya
huduma na uhamasishaji wa wakulima kujiunga na NHIF, kupitia Mpango
wa Ushirika Afya.
“Nikuhakikishie Mheshimiwa Waziri na wananchi wote walioko hapa, timu
yangu inaanza rasmi kampeni ya kijiji kwa kijini kuanzia wiki ijayo kwa
lengo la kumfikia kila mkulima aliyeko katika Mkoa wa Mtwara na Lindi ili
wananchi hawa wawe kwenye mfumo bora wa kupata huduma za
matibabu wakati wowote,” alisema Bw. Konga.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akitoa
ufafanuzi wa huduma za matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Tandahimba.
Alisema kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wote wako kwenye sekta ya
kilimo hususan maeneo ya vijijini na kwa kutambua umuhimu wa kulitunza
kiafya kundi hili, Mfuko ulianzisha mpango maalum unaojulikana kwa jina la
Ushirika Afya unaowawezesha kujiunga na huduma za NHIF kwa gharama
nafuu.
Akizungumzia upatikanaji wa huduma za matibabu, Mhe. Waziri Ummy,
alisema kuwa Serikali imetengeneza utaratibu rahisi kwa wananchi wake
juu ya upatikanaji wa huduma za uhakika za matibabu kupitia Mfuko wa
Taifa wa Bima ya Afya ambao una jukumu la kugharamia matibabu kwa
wanachama wake.
Wananchi wa Kitangali wilayani Newala wakiwa katika mkutano wa uhamasishaji wa kujiunga na
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
“Hakuna sababu yoyote kwa sasa ya kushindwa kujiunga na NHIF, Serikali
ya Awamu ya Tano imeboresha huduma na upatikanaji wa dawa kwa sasa
ni mkubwa ambao unamwezesha kila mgonjwa kupata huduma
anazozihitaji hivyo nawaomba wananchi wote mjiunge na NHIF ili muwe na
uhakika wa kupata matibabu wakati wowote hata ambao hamna fedha,”
alisema Mhe. Ummy.
Alisema kuwa suala la kulinda afya za wananchi ni suala muhimu kutokana
na ukweli kwamba bila ya afya njema ama uhakika wa matibabu hakuna
shughuli zozote za maendeleo zinazoweza kufanyika.
Kwa upande wa wananchi wamemhakikishia Mhe. Waziri kuwa wako tayari
kujiunga na NHIF na kuunga juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya
Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Walitumia nafasi hiyo kumuomba Mhe. Waziri kufikisha salaam zao kwa
Mhe. Rais Magufuli kuwa wanaridhishwa na utendaji kazi wake hivyo wako
tayari kuhakikisha ndoto zake za kuifanya Tanzania kuwa na Uchumi wa
Kati zinafikiwa.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akiwa
kwenye picha ya pamoja na viongozi wa vyama vya Ushirika katika Wilaya ya Tandahimba.
Sehemu ya wananchi waliojitokeza katika mkutano wa uhamasishaji wa kujiunga na huduma za
NHIF.
Sehemu ya viongozi wa vyama vya ushirika wakifuatilia maelezo ya namna ya kujiunga na NHIF,
kupitia Ushirika Afya.
No comments:
Post a Comment