HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 3 December 2018

WAZIRI MKUU MAJALIWA AFUNGUA MAFUNZO KWA WAKUU WA MIKOA NA MAKATIBU TAWALA WA MIKOA JIJINI DODOMA

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akifungua Mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kwenye ukumbi wa Hazina jijni Dodoma, Desemba 3, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
  Baadhi ya Makatibu  Tawala wa Mikoa wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  wakati alipofungua Mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kwenye Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Desemba 3, 2018. 
  Baadhi ya Wakuu wa Mikoa wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua  Mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kwenye Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Desemba 3, 2018.
 Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Mikoa baada ya kufungua Mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kwenye Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Desemba 3, 2018. 
 Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Makatibu Tawala wa Mikoa baada ya kufungua Mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kwenye Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Desemba 3, 2018. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda baada ya kufungau Mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala  wa Mikoa  kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Desemba  3, 2018. Wengine  pichani kutoka kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemani Jafo,  Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Profesa Joseph Semboja, Waziri Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma  na Utawala Bora, Kapt. (Mst.), George Mkuchika na Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Josephat Kandege.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU AFUNGUA MAFUNZO KWA WAKUU WA MIKOA NA MA’RAS

*Mfunzo hayo yatawasaidia kusimamia utumishi na kuzingatia miiko ya uongozi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefungua mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa, ambapo amesema  baada ya mafunzo hayo Serikali inatarajia watasimamia kikamilifu nidhamu katika utumishi wa umma na wao wenyewe watakuwa kioo katika kuzingatia miiko ya utumishi wa umma.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema viongozi hao wa mikoa watazingatia kikamilifu mipaka ya madaraka yao na kwamba hatua watakazozichukua katika uongozi na utendaji wao zitazingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo nchini.

Waziri Mkuu amefungua mafunzo hayo yanayoendeshwa na Taasisi ya Uongozi leo (Jumatatu, Desemba 3, 2018) katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine amewataka wakasimamie kikamilifu mapambano dhidi ya madawa ya kulevya.

“Mkadumishe uhusiano mwema baina yenu na watumishi walio chini yenu, kwa kuzingatia kuwa kila mtumishi anao mchango katika kuboresha utendaji kwenye kituo chake cha kazi. Nina matarajio makubwa kuwa mtadumisha uhusiano mzuri kikazi na viongozi wa juu na pia uhusiano wa diplomasia ya heshima na viongozi wengine ndani ya mihimili yetu mitatu.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao wahakikishe kila mmoja wao anaandaa mpango kazi unaoainisha shughuli zake za kila siku. “Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi na Wakuu wa Idara wote na Watumishi wote wawe na mpango kazi wa utekelezaji wa majukumu yao.”

Amesema viongozi hao wanatakiwa wasimamie nidhamu kazini na uwajibikaji wa watumishi kwa wananchi, ambapo pia amewasihi watende haki kwa wananchi na watumishi walio chini yao. Pia lazima watumishi wa Serikali wawapokee na kuwahudumia wananchi kwa staha, wawasikilize kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.

Waziri Mkuu amesema viongozi hao wanatakiwa waendelee kusimamia amani na utulivu kwenye mikoa yao ili watu waendelee kufanya shughuli zao bila wasiwasi wowote kwani  amani na utulivu ndiyo itawawezesha nchi iendelee kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje.

“Tunakumbushwa sisi viongozi tuhakikishe tunaziendeleza rasilimali za nchi hii kwa faida ya Watanzania wote bila kubagua jinsia, kabila, dini, rangi ya ngozi, mtu atokako ndani ya nchi

ilimradi hajavunja sheria; wala ubaguzi mwingine wa aina yoyote.  Tunaaswa tuwahudumie Watanzania wote kwa usawa.”

Kuhusu mada zitakazowasilishwa kwenye mafunzo hayo, Waziri Mkuu amesema zitawawezesha viongozi hao kupata fursa ya kutafakari na kujitathmini kuhusu hatua za kujiimarisha zaidi kiuongozi na kiutendaji. “Hatua hizo ni lazima ziwe pamoja na kubadilika kwa mtazamo na kujirekebisha endapo mtabaini maeneo mliyokuwa mkikosea tangu mlipokabidhiwa ofisi hadi sasa.”

Waziri Mkuu amesema mada zitakazowasilishwa kwenye mafunzo hayo zinahusu majukumu na mipaka ya kazi,ambapo watajifunza namna ya kufanya kazi bila mikwaruzano isiyo na tija baina yao na viongozi wa mihimili mingine ya dola, viongozi wa kisiasa na watendaji wengine Serikalini.

Amesema mada nyingine inahusuuongozi, hisia na mahusiano mahali pa kazi, ambapo itawawezesha kujiimarisha katika mbinu za kuwaongoza watumishi walio chini yao kwa kujenga na kudumisha mshikamano na ushirikiano wa pamoja.

“Mada itafafanua pia namna mnavyotegemeana na watumishi wa kada na ngazi mbalimbali katika kutimiza majukumu yenu. Ni muhimu sana kufanya kazi kama timu moja ili muweze kuyafikia malengo ya taasisi kwa upana wake na si malengo ya mtu au kiongozi mmoja.”

Amesema kwenye mada inayohusu muundo wa Serikali na namna inavyofanya kazi watauelewa vizuri zaidi muundo wa Serikali ulivyo na jinsi unavyofanya kazi. Pia wataielewa vizuri zaidi itifaki na kuheshimiana kwa ngazi mbalimbali kutoka Waziri, Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Makatibu Tawala, Wakurugenzi, Wakuu wa Idara hadi Wananchi.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Profesa Joseph Semboja amesema  mafunzo hayo ya wiki moja yatajikita katika maeneo makuu matatu ambayo ni kuimarisha uwezo wa washiriki katika kufanya maamuzi ya kimkakati yanayozingatia mahitaji na manufaa mapana ya sasa na ya baadae kwa jamii.

Ametaja eneo la pili kuwa ni kuimarisha uwezo wa washiriki katika kuongoza rasilimali watu na kusimamia rasilimali nyingine ili kutekeleza kikamilifu na kwa mafanikio maamuzi ya kimkakati waliyoyafanya katika kipengele cha kwanza.

“Eneo la tatu ni la kuimarisha uwezo wa washiriki katika kujijengea sifa binafsi za uongozi ili awe na ushawishi kwa wananchi anaowaongoza. Hili ni jambo la msingi, kiongozi mwenyewe awe mfano bora wa kuigwa. Awe muadilifu, mtenda haki, mfuata sheria na taratibu pamoja na kufahamu na kuheshimu miiko ya uongozi.”

Mafunzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu, George Mkuchika, Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge na Naibu Waziri  Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Josephat Kandege pamoja na maafisa wengine wa Serikali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad