HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 3, 2018

BENKI YAELEZA ILIVYOJIPANGA KATIKA KUFANIKISHA KWA VITENDO UJENZI WA TANZANIA YA VIWANDA

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
WAKATI Serikali ya Awamu ya Tano chini Rais Dk.John Magufuli ikihimiza ujenzi wa viwanda ili kufikia uchumi wa kati, uongozi wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imesema imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kujenga uchumi imara utakaotokana na viwanda.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam na wahariri wa habari za uchumi na biashara kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini , Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Theobard Sabi amesema wanatambua Serikali imedhamiria kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na kuifikisha Tanzania kuwa nchi yenye hadhi ya kipato cha kati na kuondokana na umaskini kufikia mwaka 2025.
"NBC inaunga mkono dhamira hiyo kwa kuwawezesha wafanyabiashara katika sekta mbalimbali na mitaji ya kifedha. Kama mnavyofahamu kwamba NBC ni moja ya benki yenye mtaji mkubwa wa kuwawezesha wafanyabiashara wa kitanzania. Hivyo tutahakikisha tunashiriki kikamilifu katika kuwajengea uwezo wa Tanzania ili washiriki kwenye kujenga uchumi kupitia viwanda na hayo ndio moja ya malengo yetu kama benki yenye uwezo mkubwa kifedha,"amesema Sabi.
Kuhusu vipaumbele vya benki hiyo, amesema kuwa wameweka vipaumbele vitano na namna ya kufanikisha.Amesema kipaumbele chao cha kwanza ni mteja kuwa namba moja na safari ya kumuweka mtaja kuwa wa kwanza itakazia kwenye mabadiliko ya kitamaduni ya benki yao na kuelekea kwenye utoaji hasa katika maeneo ya malipo, ufunguaji na ufufuaji wa akanti, chaneli za kidigiti pamoja na ututatuzi wa malalamiko.
Pia kipaumbele namba tatu ni kuwa karibu na wateja wao kwani NBC inaamini kwamba bila ya wateja na wao hatutakuwepo. "Hivyo tutajikita katika kuhakikisha tunakuwa karibu na wateja wetu. Tutaboresha muonekano wa matawi yetu inayoendana na matakwa na mahitaji yao.
Tumeanza na tawi letu la Dodoma ambalo lina muonekano mpya na wa kisasa unaokidhi mahitaji ya wateja wetu. Tumeanza na ukarabati wa tawi letu la Dodoma kwa sasa, lakini mengine yatafuata,"amesema Sabi.
Wakati kipaumbele namba mbili ni kuboresha huduma za malipo ambapo wanaangalia upya na kwa undani zaidi taratibu zao za malipo ilikupunguza muda wa miamala ya malipo yanayotoka matawini na ya Makao Makuu. Eneo la malipo ni eneo muhimu sana kwa wateja wao na ndio maana wanataka kuimarisha eneo hilo lifikie viwango vya kimataifa kwa mantiki ya muda unaochukuliwa kukamilisha miamala ya malipo.
Sabi amesema kipaumbele namba nne ni kujenga benki ya kidijiti ambapo mkakati huo una umuhimu wa kipekee kwa NBC kwa maana kwamba utarahisisha maisha kwa wateja wao na tayari wameanza kuwekeza kwenye mifumo mipya inayobeba huduma za kidijiti zinazokidhi mahitaji ya wateja kwa kuokoa muda, gharama, na usumbufu na hivyo kurahisisha maisha ya wateja wetu kwa kufanya miamala yao mahala popote na wakati wowote.
Ameongeza jambo la pili, ni kutekeleza mpango wa kukutana mara kwa mara na wateja wao kupitia vikao ilituweze kupata mrejesho wa huduma na bidhaa zetu kutoka kwao. Mrejesho wa wateja wetu utatupatia taarifa muhimu za kuboresha huduma zetu zilizopo na ambazo tunatarajia kupeleka sokoni. Vile vile kukutana huko kutaimarisha uhusiano wa kindugu na kibiashara uliopo kwani biashara ya benki hujengwa na uaminifu.
"Huduma hii ni faraja kubwa kwa vikundi kwani wanalazimika kukutana na kusaini hundi au hati za malipo ndipo mnufaika aende benki kuchukua fedha zake. Hilo sasa ni historia kwani mnufaika anawezakutumiwa fedha zake moja kwa moja benki au akatumiwa kwenye simu yake ya mkononi.Huduma nilizotaja ni baadhi tu na tunaendelea kubuni huduma zingine za kidijiti kuokoa gharama na kuboresha utoaji wetu wa huduma,"amesema Sabi.
Ametoa mfano kuwa wamerahisisha miamala ya malipo kwa wateja wao wakubwa kupitia mfumo wa IFEC. Wateja hao wanaweza kufanya miamala ya malipo bila kuja benki na kujaza makaratasi. "Kwa wanachama wa vikundi vya kiuchumi vilivyo rasmi na visiyo rasmi, wanaweza kuidhinisha malipo kwa wanachama wanaokopa kupitia simu zao za mkononi na vile vile wanaweza kupata taarifa fupi ya salio ya akaunti yao bila ya kuwa na haja ya kwenda benki.
Ametaja kipaumbele namba tano ni kukuza hisa zao kwenye soko ambapo benki hiyo imedhamiria kukuza mapato yake katika kipindi kijacho kwa kazia kwenye mifumo mipya, bidhaa mpya, utoaji wa huduma bora, na kuwekeza kwenye huduma za kidijiti katika maeneo matatu makuu.
Pia amekumbusha kuwa NBC inamilikiwa kwa asilimia 30 na Serikali ya Tanzania, hivyo wanawajibika kulinda maslahi ya mwanahisa wa NBC huku akifafanua benki hiyo ni moja ya benki chache zilizoaminiwa na Serikali kujiunga na mfumo wa malipo Serikalini (GePG) ilikukusanya maduhuli ya Serikali.
Amesema pamoja na mipango mkakati ambayo ameibainisha yote itawezekana kwa kuzingatia sera, miongozo na taratibu za kibenki walizojiwekea wenyewe. "Lakini kubwa zaidi ni ushirikishwaji wa wafanyakazi wa NBC katika kutengeneze mikakati yetu, maana uongozi wa NBC ni shirkishi (inclusive) na anuai (diverse). Mafanikio yetu yanategemea sana wafanyakazi wetu na ndio maana ni muhimu kuwashirikisha ili kuwepo na uelewa wa pamoja kutoka chini hadi juu".
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi akielezea mpango makakati wa miaka mitano wa benki hiyo  wenye lengo la kuboresha kwa kiwango kikubwa huduma za benki hiyo kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC,  Theobald Sabi (kushoto),  akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam kuelezea mpango mkakati wa miaka mitano wa benki  hiyo wenye lengo la kufanya maboresho makubwa kwenye huduma zake. Kushoto kwake ni jopo zima la wakurugenzi wa benki hiyo.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC,  Theobald Sabi (mbele),  akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam kuelezea mpango mkakati wa miaka mitano wa benki  hiyo wenye lengo la kufanya maboresho makubwa kwenye huduma zake. Walioketi ni baadhi ya wakurugenzi wa NBC.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad