HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 19 December 2018

BENKI YA CBA NA VODACOM WAKABIDHI ZAWADI ZA BAJAJI 5 KWA WASHINDI WA PROMOSHENI YA SHINDA NA M- PAWA

Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii
BENKI ya CBA kwa kushirikiana kampuni ya simu ya Vodacom wamekabidhi zawadi kwa washindi wake wa promosheni ya shinda na M- pawa katika tawi la benki ya CBA kijitonyama jijini Dar es salaam, na hiyo ikiwa ni baada ya kudumu kwa promosheni hiyo kwa muda wa wiki 6.

Akizungumza katika makabidhiano hayo mwakilishi wa Mkurugenzi wa benki ya CBA Julius Konyani amesema kuwa  promosheni hiyo ililenga kuwafikia wananchi wasiofikiwa na huduma  za kibenki na kuwawekea mazingira ya kujiwekea akiba huku ikiwapa changamoto ya kurudisha mikopo yao kwa wakati pindi wanapochukua mikopo.

Konyani amesema kuwa; "Mikopo yetu ina riba ndogo sana kwani lengo la  kufanya promesheni hii  hasa ilikua ni kuwawezesha kiuchumi wateja wetu, pia promosheni hii ilikua na lengo la kutoa shukrani na kuwazawadia wateja  wetu katika msimu huu wa sikukuu na tumefurahi washindi wetu wamekuwa ishara ya mafanikio yetu katika lengo hili" Ameeleza Konyani.

Aidha amesema kuwa benki ya CBA kwa kushirikiana na Vodacom wataendelea kutoa na kuboresha huduma ya M-pawa na kuwafikia watanzania wengi zaidi wakiwemo wakulima na wajasiriamali ambao watapewa mikopo midogo hadi ya shilingi laki tano ili kuweza kuwapa nguvu katika shughuli zao za kiuchumi wanazozifanya.

Kwa upande wake Meneja masoko, huduma za kifedha kutoka kampuni ya Vodacom Noel Mazoya amewashukuru watumiaji wa Vodacom kupitia huduma ya M-Pawa  na kuahidi kuboresha zaidi huduma hiyo ili watanzania waweze kunufaika.

Mazoya amesema kuwa kwa kipindi cha promosheni pekee wamefanikiwa kuwapata wateja wapya zaidi ya milioni moja wa M-Pawa na amewapongeza washindi hao na kuwataka wakawe mabalozi wao kupitia huduma ya M-pawa.

Mmoja wa washindi hao Mariam Barawa, Mkazi wa Kibamba jijini Dar es salaam  ametoa wito kwa wateja wa vodacom kutumia huduma ya M-pawa ili waweze kupata zawadi kutoka CBA na amewashukuru kwa zawadi hiyo na kueleza kuwa itamsaidia katika kuingiza kipato chake.

Kampeni ya shinda na M-pawa ilifanyika kuanzia Novemba 8 na kufika tamati Desemba 13 ambapo jumla ya washindi 1296 walipatikana huku mshindi mkuu ambaye ni Sophia Sarapion (54) mkulima wa mihogo kutoka Bukoba alijishindia pesa taslimu shilingi milioni kumi ambazo atakabidhiwa mapema mwezi ujao.
Washindi wa bajaji kupitia promosheni ya shinda na M -pawa wakiwa pamoja na baadhi ya viongozi kutoka benki ya CBA na Kampuni ya simu ya Vodacom.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa benki ya CBA Julius Konyani (kushoto)akimkabidhi kadi ya bajaji bi. Mariam Barawa mmoja kati ya washindi watano waliojishindia bajaji hizo kupitia promosheni ya shinda na M- Pawa,  jijini Dar es salaam. Kulia ni meneja masoko wa huduma za kifedha kutoka kampuni ya Vodacom Noel Mazoya.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad