HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 22 November 2018

WAZIRI KAIRUKI AAGIZA RITA KUVUNJA BODI YA UONGOZI WA MFUKO WA UDHAMINI WA NORTH MARA

Na Asteria Muhozya, Mara
Waziri wa Madini Angellah Kairuki ameuagiza Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kuvunja uongozi wa Mfuko wa Udhamini wa North Mara ( Bodi ya Wadhamini na Menejimenti) kwa kuwa umeshindwa  kusimamia  uendeshaji wa Mfuko kwa tija na kuandaa utaratibu mzuri  wa usimamizi  wa Mfuko huo ambao utakuwa na  manufaa kwa Taifa .

Aidha, Waziri Kairuki amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Tarime kuruhusu fedha za Keng'anya Enterprises Ltd ( KEL) kuendelea kulipwa  hadi hapo vyombo vya uchunguzi vitakakapobaini na kuelekeza vinginevyo, huku Mkuu wa Mkoa wa Mara akitakiwa kusimamia utekelezaji wa agizo hilo.

“Kwa kuwa Keng'anya Enterprises iliomba kupata PL 303/95 kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia Sekta ya Madini, hivyo malipo ya mrabaha wa asilimia moja yanayopokelewa kutoka kwenye mgodi kwa mujibu wa mkataba wake ni halali,” alisisitiza Kairuki.

Waziri Kairuki  alitoa  maagizo hayo Novemba 21, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ambaye alielekeza kufanyika uchunguzi wa Mfuko wa North Mara Community Trust  Fund, baada  ya baadhi ya wananchi wa Nyamongo Wilayani  Tarime kulalamika juu ya jamii kutofaidika na mfuko huo na badala yake kunufaisha baadhi ya watu wachache.

Rais Magufuli alitoa maelekezo ya kufanyika kwa uchunguzi wa mfuko huo wakati wa ziara yake Mkoani Mara tarehe 4 hadi 8 Septemba, 2018.

Mbali na agizo la kuuvunja uongozi wa mfuko, Waziri Kairuki aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwachunguza na kuwachukulia hatua za kisheria wajumbe wa bodi ya wadhamini, menejimenti ya mfuko na yeyote atakayethbitika kujihusisha na ufujaji na matumizi mabaya ya fedha za mfuko.

Pia, aliiagiza serikali ya Mkoa kukaa na wamiliki wote wa leseni zilizopo ndani ya Mgodi ambao wanalipwa mrabaha wa asilimia 1 kuangalia mfumo bora ili nao wachangie kwenye mfuko sehemu ya fedha wanazopokea kwa ajili ya maendeleo ya vijiji vnavyozunguka Mgodi wa North Mara.

Vilevile, aliigiza TAKUKURU kuchunguza na kuwachukulia hatua za kisheria watumishi wote watakaobainika kufanya ufujaji na ubadhirifu wa fedha za umma shilingi 214,000,000.
Maagizo ya Waziri Kairuki yanatokana na yaliyobainika katika kamati iliyoundwa na Wizara ya Madini baada ya kutolewa maelekezo ya kuchunguzwa kwa mfuko huo na Rais Magufuli.
Waziri Kairuki alisema miongoni  mwa mambo iliyoyabaini  kamati hiyo ni pamoja na Kampuni Tanzu ya North Mara Commercial Business Ltd tarehe 20 Aprili, kutoa kiasi cha shilingi milioni 214,000,000 kwenda kwa DAS Tarime kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo cha miwa, ambapo katika taarifa yake, Waziri Kairuki alisema kuwa, fedha hizo zilitokana na maombi yaliyowasilishwa na  Mkuu wa wilaya ya Tarime, ambazo hata hivyo, hazikuzingatia utaratibu wa fedha za umma na manunuzi.
“ Kampuni Tanzu ilifunguliwa mwaka 2017 ambayo wana hisa wake ni North Mara Community Trust Fund asilimia 99 na Bw., Robin Motengi Marwa asilimia 1,” alisema Kairuki
Aliongeza kuwa, pia ilibainika kuwa, wajumbe wa bodi  ya wadhamini wamekuwa wakikopeshwa  fedha za mfuko kinyume na malengo ya uanzishwaji wa mfuko huo.
Pia, kamati hiyo ilibaini kwamba, kati ya Mwaka 1990 hadi 1998, vijiji vya Nyangoto, Karende, Kewanja, Genkuru na Nyamwanga viliwahi kumiliki leseni tano za uchimbaji (CTs). Mwaka 1996, vijiji hivyo vilibadili leseni hizo kwa hiari yao na kuwa leseni ya utafiti PL 370/96 na kisha kuihamishia kwenye Kampuni ya East African Gold Mining Ltd (EAGM) na kisha kubadilishwa kuwa leseni ya uchimbaji wa kati (ML 17/96).
Halikadhalika, Waziri Kairuki alisema kamati ilibaini kuwa,  North Mara Community Trust Fund ilianzishwa kwa makubaliano kati ya Mgodi  na kampuni ya KEL ya Mwaka 2004. Mfuko huo ulisajiliwa Mwaka 2013 na kuanza kazi Mwaka 2015. Aliongeza kuwa, wachangiaji pekee wa Mfulo huo ni KEL na Mgodi kwa kiwango cha sawa cha asilimia 0.1 ya uzalishaji katika eneo la KEL.
“ Mfuko huo unaendeshwa na wajumbe wa bodi inayoundwa na pande zote tatu yaani Mgodi, KEL na vijiji, bodi inatakiwa kuwa na wajumbe wasiopungua watano.
Akizungumza kuhusu malengo ya kuundwa mfuko huo, alisema kamati ilibaini kwamba mfuko ulianzishwa kwa lengo l kutafuta shughuli zenye manufaa kwa jamii, kuhamasisha, kusaidia na kuwezesha program na shughuli kwenye maeneo ya elimu, mafunzo, afya, uwezo kilimo , maji na kupunguza umaskini kwa ujumla kadri ya wadhamini watakavyoona inafaa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima, alisema kazi hiyo ilifanyika kwa kipidi cha miezi miwili na hivyo kumshukuru waziri na wote walioshiriki kukamilika  maagizo hayp hayo ya kufanyika uchunguzi, yaliyotolewa na Rais Magufuli.
Waziri wa Madini Angellah Kairuki akieleza jambo. Kulia ni Mkuu wa MKoa wa Mara, Adam Malima na kushoto ni Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko
Waziri wa Madini Angellah Kairuki akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima (kulia)
Sehemu ya Watendaji kutoka Wizara ya Madini, Uongozi wa Mkoa  wa Mara wakifuatilia kikao hicho.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad