HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, November 27, 2018

WALIOVAMIA ARDHI YA BAKWATA MWANZA WATAKIWA KUONDOKA KWA HIARI

Na Baltazar Mashaka, Mwanza
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza linakusudia kujenga hospitali itakayowahudumia waumini wa dini hiyo na jamii. Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Alhaji Sheikh Hassan Musa Kabeke alisema jana wakati akizungumza na waandishi wa habari pamoja na waumini wa dini hiyo baada ya kufanya usafi kwenye Msikiti wa Nyegezi Kijiweni katika Wilaya ya Nyamagana.

Alisema baadhi ya wananchi wamevamia na kujenga kwenye maeneo yanayomilikiwana taasisi hiyo ya dini likiwemo eneo la msikiti wa Nyegezi Kijiweni wanalotaka kujenga kituo cha afya na baadaye hospitali na hivyo wote waliovamia maeneo yake waondoke wenyewe. Sheikh Kabeke alifafanua kuwa wamebaini maeneo ya BAKWATA mkoani Mwanza likiwemo eneo la msikiti wa Nyegezi ambao ulichomwa moto na watu wasiojulikana, yamevamiwa na kuwataka walioingia na kufanya ujenzi wajitathmini na wachukue uamuzi sahihi kwa maslahi ya Waislamu na jamii ya Watanzania.

Alisema waliojenga kwenye ardhi ya maeneo ya baraza hilo la Waislamu ni vema wakaondoka wenyewe badala ya viongozi wa kiroho kuingia kwenye mgogoro na misuguano isiyo ya lazima na waumini wake ama jamii inayowazunguka.Kaimu sheikh huyo wa mkoa alisema; “ Katika utaratibu wa BAKWATA wa kukagua na kuhakiki mali zake wamebaini baadhi ya maeneo yao yamevamiwa na kujengwa nyumba za kudumu.Waliovamia waje tukae mezani kwa mazungumzo ili wapishe kwa hiari badala ya kuingia kwenye migogoro na marumbano.”

Sheikh Kabeke aliongeza; “Kilio cha Waislamu hapa Mwanza ni hospitali itakayowahudumia kwa pamoja na jamii, tutaijenga kwenye eneo letu la Nyegezi kwa maendeleo yao.Lakini wapo watu wameingia na kujenga nyumba za makazi kwenye eneo la baraza, hivyo wajitathmini na wajiondoe wenyewe na kurejesha ardhi hiyo kwa BAKWATA.” Alieleza kuwa, kwa kuwa waislamu wanahamasisha amani na utulivu, hawana ugomvi na waliojenga kwenye ardhi ya eneo la msikiti na anaamini waliongia na kujenga nyumba za makazi wataitunza amani hiyo ikizingatiwa vitabu vya dini vinakataza dhuluma.

Sheikh Kabeke ambaye pia ni Mwenyekiti mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa dini Mkoa wa Mwanza aliongeza kuwa wakati wanamilikishwa eneo hilo kulikuwa na nyumba tatu za asili lakini sasa mbali na hizo zimeongezeka nyingine saba, hivyo kwa nia ya kutunza na kulinda amani na usalama kwenye jamii watu hao wakae wazungumze na BAKWATA. Aidha, msikiti wa Nyegezi eneo ambalo wanataka kuliendeleza kujenga hospitali ulichomwa moto na watu wasiofahamika  mwaka jana.
 Katibu wa BAKWATA Kata ya Nyegezi akifafanua jambo kwa Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Alhaji Sheikh Hassan Musa Kabeke wakati wakikagua mipaka ya eneo la taasisi hiyo Nyegezi Kijiweni jana. 
 Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Alhaji Sheikh Hassan Musa Kabeke akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu wakiwemo waandishi wa habari (hawapo pichani) baada ya kumaliza kufanya usafi kwenye Msikiti wa Nyegezi Kijiweni katika Wilaya ya Nyamagana. Wa pili kutoka kulia ni Kaimu Katibu wa BAKWATA mkoani humu, Sina Mohamed Mwagalazi.
 Ustadhi Khatibu Imani akizungumza na waandishi wa habari (hawapo picha) kuhusu uvamizi wa ardhi ya BAKWATA ulipojengwa Msikiti wa Nyegezi Kijiweni. Picha zote na Baltazar Mashaka

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad