Na Mwandishi Wetu, Kibaha Pwani
WATU wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kwa tuhuma za uvunjaji wa nyumba usiku na kuiba katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani ambapo jumla ya mali zote zilizokamatwa zina thamani kiasi cha Shilingi Mil. 18,800,000.
Watuhumiwa hao wamekamatwa kufuatia msako mkali ulioendeshwa na makachero wa kupambana na makundi yanayojihusisha na matukio ya uvunjaji na kuiba mali za watu katika nyakati za usiku na mchana.
Yamesemwa hayo na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani ACP Nyigesa Wankyo amesema kuwa majina ya watuhumiwa yamehifadhiwa kwa ajili ya uchunguzi na kufanikisha kuukamata mtandao wote wa walioshirikiana nao katika matukio ya uvunjaji.
RPC Wankyo alisema kuwa katika msako huo wamefanikiwa kukamata vitu mbalimbali amabvyo ni luninga kumi za aina mbalimbali ( zote Flat Screen) , jenereta kubwa mbili zenye thamani ya sh.6, 500,000, jenereta hizo ni aina ya Euro Power EP.6500E na Boss BG-2500.
Vitu vingine vilivyokamatwa katika msako huo ni pamoja na deki mbili,ving'amuzi viwili, spika mbili music system mbili, home theatre, rimoti sita, speaker twiter mbili, flash moja, kapeti za chini ya sakafu mbili, stendi moja ya vyombo na extention moja.
Aidha Kamanda amesema kuwa wamemkamata mtuhumiwa mmoja akiwa na lita 200 za mafuta ya dizeli ambapo alikutwa na madumu kumi yenye ujazo wa lita 20 mafuta hayo alikua ameiba katika karakana ya mradi wa reli ya kisasa (Standard Gauge) iliyopo eneo la Soga Wilaya ya Kipolisi Mlandizi.
Pia amewaasa wale wote wanaohujumu mradi wa mkubwa wa ujenzi wa reli ya kisasa kwa kuiba mafuta kuacha mara moja tabia hiyo kwani Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani hawatakuwa na muhali nao na mtu yeyote atakayejaribu kujihusisha na vitendo vya wizi tutawakamata na kuwafikisha mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
"Mtuhumiwa huyo alikamatwa katika kijiji cha Mperamumbi akiwa amepakia mafuta hayo kwenye pikipiki aina ya SANLG namba MC.197BJD.Mtuhumiwa anashikiliwa kwa mahojiano zaidi kwa lengo la kubaini walem wote ambao amekuwa akishirikiana nao katika wizi huo wa mafuta na atafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma hizo mbili zinazomkabili" alisema Wankyo.
Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limekamata bhangi kiroba kimoja kilichokua kinasafirishwa kwenda kuuzwa, katika tukio hulo mmiliki wa pikipiki yenye namba za usajiliMC951 BSA anaombwa kujisalimisha kwenye kituo chochote cha Polisi ndani ya siku tatu vinginevyo atasakwa popote pale aliko ili kujibu tuhuma za kusafirisha bangi ambayo aliitelekeza ikiwa kwenye pikipiki hiyo baada ya kugundua anafuatiliwa na askari wa jeshi la polisi.
"Kutokana na matukio haya Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani tunatoa wito kwa wananchi kuwa wabia katika suala zima la ulinzi shirikishi kwenye maeneo tao ili kuweza kukabiliana na matukio ya uvunjaji wa sheria..Pia tunatoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Pwani kuwafichua wale wote wanaoshirikiana na wahalifu kwenye maeneo yao kwani haiwezekani mahali pakavunjwa katika mtaa bila ya kuwepi na wenyeji wanaowafahamu alisema RPC Wankyo.
"Natoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kununua vitu vya mikononi bila kupewa risiti ya kile wanachokinunua, wale wote ambao watakutwa na mali ya wizi nao tutawachukulia hatua kali za kisheria ili iwe mfano kwa wengine"alisema Kamanda huyo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani ACP Nyigesa Wankyo akiwa na baadhi ya maofisa wa Jeshi la Polisi akizungumza na waandishi wa habari
No comments:
Post a Comment