HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, 6 November 2018

POLISI BINGWA TAEKWONDO KENYA YA PILI, RPC AWAITA OFISINI

Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Mashindano ya ya Nane Nane Taekwondo Clubs Championship yamemalizika jana jioni kwa timu ya Polisi Arusha Taekwondo Club kuibuka mshindi baada ya kuzipiku timu zote zilizoshiriki kwa siku mbili katika ukumbi wa Tripple “A” uliopo jijini hapa.

Timu hiyo ambayo inajumuisha wachezaji wa kike na wa kiume pamoja na watoto wadogo wanaoanzia umri wa miaka mitano iliweza kuibuka na ushindi huo baada ya kupata jumla ya medali 27 toka katika makundi yote matatu ambapo watoto wa umri wa miaka 5, 8 na 13 walipata Gold Moja na Silver Mbili, huku askari pekee wa kike Ester Yohana akipata Gold na wanaume wakipata Gold 6, Silver 5 na Bronze 12.

Mashindano hayo ambayo yana umuhimu mkubwa katika kupima uwezo wa kila mchezaji yalishirikisha jumla ya timu kumi ambazo ni Polisi Arusha,Kijenge, Kili, Edmund Rise School,Perfect, Tripple A, Naura zote za Tanzania na Kilifi, Regional  A na Regional B zote toka nchini Kenya.

Katika mashindano hayo timu ya Polisi Arusha ilijinyakulia medali 8 zilikuwa za Gold, 7 za Silver na 12 za Bronze huku nafasi ya pili ilishikwa na timu ya Chuo Kikuu cha Kilifi toka Kenya ambayo ilipata medali 15 ambapo za Gold zilikuwa 4, Silver  5 na Bronze 6 , wakati nafasi ya tatu ilikwenda kwa kwa timu ya Regional.

Mara baada ya kupata taarifa hiyo Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng’anzi ambaye ndio mlezi wa timu hiyo alitikisa kichwa juu na chini kama ishara ya kufurahia ushindi huo na kuialika timu hiyo bingwa ofisini kwake siku ya Jumamosi.

Kufuatia ushindi huo baadhi ya wachezaji wa Kenya Joy Ludoro na Charity Manga wote kwa pamoja walitoa pongezi kwa timu ya Polisi Arusha kwa kushika nafasi ya kwanza na kuahidi katika mashindano yajayo wanaamini watafanya vizuri zaidi na kushika nafasi ya kwanza.

“Mashindano haya yametuongezea hari ya kuongeza juhudi zaidi ili mashindano yajayo tushike nafasi ya kwanza kama walivyofanya Polisi safari hii” Alisema Joy Ludoro mchezaji wa timu ya Kilifi ya nchini Kenya.

Kwa upande wa Charity Manga alisema Arusha ina wachezaji wa kike wachache hivyo alishauri viongozi wanaosimamia mchezo huo watoe hamasa kubwa kwa wanawake hali ambayo hata katika mashindano hayo huo wakose washindani wa uzito wao.

Naye kocha wa timu bingwa ya Polisi Arusha Taekwondo Club, Master Shija Shija alisema abweteki na ushindi alioupata bali atazidi kuongeza mazoezi na mbinu mbalimbali kwa wachezaji wake na kutoa wito kwa watanzania kuwa, wajitokeze kushiriki mchezo huo utakaowawezesha kuimarisha afya zao pamoja na kujilinda wao wenyewe.
 Mchezaji mwenye umri mdogo toka Kenya akiwa ameuangushwa chini baada ya kupigwa teke na mchezaji wa timu ya Taekwondo ya Polisi Arusha katika mchezo wa mashindano ya Nane Nane yaliyofanyika jana katika ukumbi wa Tripple A uliopo jijini hapa na Polisi kuibuka mshindi. (Picha na Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha) 
 Wachezaji wa timu ya Polisi Arusha Taekwondo wakimpongeza mmoja wa wachezaji wao mwenye umri mdogo mara baada ya kushinda mchezo wake dhidi ya mpinzani wake toka Kenya katika pambano la Nane Nane Taekwondo Clubs Championship lililofanyika ukumbi wa Tripple A uliopo jijini Arusha. (Picha na Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha)
 Wachezaji wa timu ya Polisi Arusha Taekwondo ambao ni mabingwa wa michuano ya Nane Nane Taekwondo Clubs Championship wakiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa timu za Kilifi na Regional toka nchini Kenya mara baada ya mashindano hayo kumalizika jana. (Picha na Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad