HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 23 November 2018

Muhimbili yahudumia wagonjwa zaidi ya 1476 Ligula

Madaktari Bingwa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili pamoja na watalaam wengine wa afya leo wamehitimisha utoaji wa huduma za afya katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Mtwara -Ligula- kwa kuhudumia wagonjwa 1476.

Kati ya hao, upasuaji mkubwa umefanyika kwa wagonjwa 54 na mdogo kwa wagonjwa 81. Baadhi ya upasuaji mkubwa uliofanyika ni kutoa uvimbe kwenye mfuko wa uzazi, kutoa matezi ya koo na matezi ya nyama ya pua (mafindofindo, kutoa tezi dume pamojan na kutoa mtoto wa jicho. Maeneo ambayo wataalam wa Muhimbili kwa kushirikiana na wataalam wa Hospitali ya Ligula wamehudumia ni magonjwa ya dharura, Radiolojia magonjwa ya ndani, afya ya kinywa na meno,watoto ,magonjwa ya pua,koo na masikio, magonjwa ya kike na uzazi pamoja na mfumo wa mkojo.

Utoaji wa huduma za afya umeenda sambamba na kuwajengea uwezo wataalam wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mtwara ili waweze kutoa huduma bora za afya na kupunguza rufaa za kwenda Muhimbili. Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Ligula Dkt. Lobikieki Kissambu amewashukuru wataalam wa Muhimbili kwa kutoa huduma za afya katika hospitali hiyo na kueleza kuwa hospitali hiyo ina Daktari Bingwa mmoja tu hivyo ujio wa watalaam hao umewawezesha wananchi kupata huduma za kibingwa.

Utoaji wa huduma za afya kwa njia ya mkoba ni sehemu ya mpango mkakati wa Hospitali ya Taifa Muhimbili ya kuhakikisha inatembelea Hospitali za Rufaa za Mikoa nchini ili kushirikiana nao na kuwajengea uwezo katika kutoa huduma ili kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa Muhimbili.
Wataalam wa afya wa Hospitali ya Rufaa mkoa wa Mtwara-Ligula- wakiwahudumia wagonjwa wa macho kwa kutumia mashine maalum ya kupimia macho.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya kinywa na meno kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Frank Kessy (kulia) akishirikiana na Dkt. Dickson Sahini kumfanyia upasuaji mgonjwa mwenye uvimbe aina ya jipu lililotokana na magonjwa ya kinywa na meno.
Daktari Bingwa wa watoto Apansia Ndossa (kushoto) pamoja na muuguzi Dorcas Ndedya wakimuhudumia mtoto mchanga ambaye hakupumua vizuri baada ya kuzaliwa.
Daktari wa magonjwa ya dharura kutoka Muhimbili (kulia) akitoa maelekezo kwa watoa huduma wa kitengo cha magonjwa ya dharura katika Hospitali ya Ligula jinsi ya kumpatia huduma mgonjwa mwenye shida ya kupumua.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya ndani wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Henrika Kimambo (kushoto) akimuhudumia mgonjwa mapema hii leo.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad