HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 19 November 2018

Huduma za kibingwa ni Mkombozi kwa wananchi- RC

 Mkuu wa Mkoa wa Katavi. Bw. Amos Makala akihutubia wananchi wakati wa uzinduzi wa mpango wa Madaktari Bingwa unaotekelezwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoani humo.
 Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu na Ushauri wa Kiufundi, Dkt. Aifena Mramba akitoa maelezo ya awali katika hafla ya uzinduzi wa Mpango wa Madaktari Bingwa Mkoani Katavi.
 Mkuu wa Mkoa wa Katavi. Bw. Amos Makala akipokea dawa na vitendanishi ambavyo vitatumika katika zoezi la kuwahudumia wananchi wa Mkoa wa Katavi kupitia Mpango wa Madaktari Bingwa.
 Madaktari Bingwa wakifuatilia tukio la uzinduzi wa kuwahudumia wananchi wa Mkoa wa Katavi.
Wananchi wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi.

 Wananchi wakifuatilia hotuba ya Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi.
  Mkuu wa Mkoa wa Katavi. Bw. Amos Makala na Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu na Ushauri wa Kiufundi wa NHIF, Dkt. Aifena Mramba wakisalimiana na wananchi waliofika kwenye uzinduzi wa huduma hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi. Bw. Amos Makala akimwangalia mtoto aliyeletwa hospitalini hapo kwa ajili ya huduma za Madaktari Bingwa.
Maofisa wa NHIF wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Katavi.

Na Grace Michael, Katavi
SERIKALI imepongeza jitihada za kusogeza huduma za matibabu zinazofanywa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kupitia mpango wake wa kupeleka Madaktari Bingwa katika mikoa mbalimbali nchini hususan yenye upungufu wa wataalam.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Bw. Amos Makala wakati akizindua huduma za Madaktari Bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo.

“Wazo la kuanzisha na kuendeleza mpango huu ni la manufaa makubwa kwa wananchi wetu kwani sio wananchi wote wanaweza kuzifikia huduma hizi za kitaalam huko zilipo hivyo kuleta huduma hizi hasa katika Mkoa huu jambo zuri na la kupongezwa sana,” alisema Bw. Makala.

Alisema kuwa kitendo cha NHIF kupeleka Madaktari hao kinapunguza gharama kwa wananchi na upotevu wa muda wa kufuata huduma hizo katika Hospitali kubwa lakini pia inasaidia kwa kiwango kikubwa kuimarisha huduma za matibabu katika hospitali wanazopeleka mpango huo.

Kutokana na umuhimu huo, alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi wote wenye uhitaji kujitokeza ili wanufaike na huduma hizo lakini pia kuhakikisha kila mwananchi anakuwa mlinzi wa huduma za Mfuko ili uweze kuimarika na kuendelea kuwahudumia Watanzania. 

“Mbali na kuleta wataalam hawa lakini pia wameleta na dawa na vitendanishi mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha wananchi hawakosi huduma walizofuata, tunawashukuru sana NHIF,” alisema Bw. Makala.

Akitoa maelezo ya awali, Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu na Ushauri wa Kitaalamu Dkt. Aifena Mramba alisema kuwa tangu mpango huu uanze mwaka 2013 umefikia mikoa  17 na imefanyika mara 22. Aliitaja Mikoa hiyo ni pamoja na Rukwa, Lindi, Kigoma, Katavi, Mara, Tabora, Manyara, Mtwara, Shinyanga, Simiyu, Kagera, Singida, Ruvuma, Iringa, Njombe, Geita ambapo jumla ya wagonjwa 18,133 walihudumiwa huku wagonjwa 734 wakifanyiwa upasuaji wa aina mbalimbali. 

Dkt. Mramba alisema kuwa mpango huu una lengo la kuhakikisha wanachama wa Mfuko na wananchi wengine wananufaika na huduma za kitaalam zinazopatikana katika maeneo mengine lakini pia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali kubwa ikiwemo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Bugando, KCMC na Benjamin Mkapa.

Akizungumzia huduma zingine kwa wanachama wa Mfuko, Dkt. Mramba alisema kuwa kwa sasa Mfuko umejipanga kuhakikisha unawafikia wananchi katika maeneo yote ili kuhakikisha kila mwananchi anatibiwa katika utaratibu wa Bima ya Afya.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad