Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii
UBALOZI wa Sweden nchini umesaini makubaliano na shirika la Femina Hip ikiwa ni msaada wa kutekeleza mpango mkakati wa Femina Hip kwa mwaka 2018/2020. Katika makubaliano hayo jumla ya shilingi bilioni 4.5 zimetolewa kwa shirika hilo ili kuendelea kukuza elimu ya afya ya uzazi, haki, uwezeshaji kiuchumi na uraia kwa vijana nchini. Makubaliano hayo yametiwa saini na Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Ubalozi wa Sweden nchini Ulf Kallstig na mwanzilishi na Mkurugenzi mtendaji wa Femina Hip Dkt. Minou Fuglesang katika ofisi za ubalozi wa Sweden leo jijini Dar es salaam.
Akizungumza na vyombo vya habari wakati wa makubaliano hayo Ulf Kallstig amesema kuwa mchango wa Sweden utaboresha mipango ya Femina Hip inayolenga kuwawezesha vijana kutoka kona zote nchini hasa katika kuwajengea juhudi za kuwawezesha, kuboresha maisha ya vijana nchini na kuwajengea tabia ya uwajibikaji.
Aidha amesema kuwa, "Vijana wana jukumu muhimu katika kuiendesha Tanzania kuelekea taifa la uchumi wa kati wa viwanda na ni muhimu kwetu kuzishirikisha sauti za vijana katika mijadala ya kimaendeleo inayolenga kuhakikisha malengo ya maendeleo endelevu yanafanikiwa pamoja na ari ya ushirikishwaji na ustawi wa Tanzania" ameeleza Ulf.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Femina Hip Dkt. Minou Fuglesang amesema kuwa, " Femina Hip inashukuru kwa ushirikiano na ubalozi wa Sweden, tutaendelea kuchangia kazi zinazofanywa na serikali ya Tanzania katika kuhakikisha kwamba katika kizazi hiki cha vijana hususani wasichana wanalindwa na kusaidiwa kuwa raia wema wenye kuwajibika ipasavyo" ameeleza Dkt. Minou.
Dkt. Minou amesema kuwa, asasi za kiraia ni chombo muhimu na zina nafasi ya kipekee katika kuwapa sauti wananchi na kwa Femina kwa miaka mingi imekuwa chombo kinachoaminiwa kwa kuimarisha kitengo cha uhamasishaji na ushirikiano kwenye mitandao ya shule za sekondari na mashirika ya ndani katika kufikisha ujuzi muhimu vijana kila kona nchini.
Mkurugenzi wa habari wa Femina Amabilis Batamula amesema kuwa, wakielekea miaka 20 ya Femina wanaishukuru sana serikali ya Tanzania na Sweden kwa kuwaunga mkono na hadi sasa wanawafikia watu Milioni 15 kwa mwaka na kuna zaidi ya klabu 2340 za Fema kwa katika shule za sekondari kote nchini.
Aidha Batamula ameishukuru serikali kwa kuruhusu na kutambua mchango wa asasi za kiraia ikiwepo Femina katika kuwajenga vijana katika ujenzi wa taifa.
Pia amesema kuwa katika wiki ya vijana iliyohitimishwa kitaifa Mkoani Tanga, mgeni rasmi Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Ummy Mwalimu alipendekeza uwepo wa Klabu za Fema katika shule zote za serikali na binafsi nchini na wao wanasubiri mwitiko kutoka kwa vijana katika shule mbalimbali nchini.
Mwisho ameushukuru ubalozi wa Sweden kwa kuwa marafiki wazuri kwa Serikali na Femina na kwa msaada walioupata leo utawasaidia sana vijana.
Mkurugenzi mtendaji wa Femina Hip Dkt. Minou Fuglesang akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam ambapo ametoa shukurani kwa ubalozi wa Sweden kwa kuonyesha ushirikiano ambao utaiwezesha shirika la Femina kuendekeza juhudi za kuwawezesha kuboresha Maisha ya vijana wa Tanzania na kuwajengea tabia ya uwajibikaji.
Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Ubalozi wa Sweden Ulf Kallstig pamoja na Mkurugenzi mtendaji wa Femina Hip Dkt.Minou Fuglesang leo Jijini Dar es Salaam katika ubalozi wa Sweden wakisaini mkataba wa makubaliano Mapya ya shilingi bilioni 4.5 za Kitanzania na shirika la Femina Kwa kipindi cha mwaka 2018-2020 ili kuboresha mipango ya shirika hilo.
Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Ubalozi wa Sweden Ulf Kallstig wakikabidhiana mkataba huo na Mkurugenzi mtendaji wa Femina Dkt Minou Fuglesang pamoja na Mkurugenzi wa habari wa shirika hilo Amabili Batamula baada ya zoezi la utiaji saini kumalizika leo Jijini Dar es Salaam katika ubalozi wa Sweden.
No comments:
Post a Comment