HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 5 October 2018

NAJUA TUUMEJIFUNZA AJALI YA MV NYERERE, SASA TUJADILI MWENDO KASI NA TRENI DAR…

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii

KABLA yakuendelea naomba msomaji wangu alau kwa dakika moja fumba macho. Kisha wewe na mimi tumuombe Mwenyezi Mungu azipumzishe roho za ndugu zetu 226 mahala pema peponi Amina.

Ni ndugu zetu  ambao wamepoteza uhai wao baada ya Kivuko cha MV. Nyerere kupinduka Septamba 20 mwaka huu katika Kisiwa cha Ukara mkoani Ukewere mkoani Mwanza. Ni moja ya ajali mbaya kuwahi kutokea ndani ya nchi yetu. Ni ajali ambayo sitaki hata kuisikia ikizungumzwa au kujadiliwa.

Ni ajali ambayo inasikitisha, inahuzunisha na inaumiza moyo. Huo ndio ukweli. Watanzania 226 kupoteza maisha kwa siku moja si jambo ambalo linaweza kusahaulika kwenye maisha yetu.

Waliopona katika ajali hiyo ni watu 41 tu. Inaumiza kwa kweli. Wakati naendelea kukusanya nguvu ili kueleza kile ambacho nimekikusudia naomba nitumie nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli kwa namna ambavyo wameshughulikia tukio hilo.
Rais Magufuli pamoja na walio chini yake walihakikisha wanafuatilia hatua kwa hatua kuhusu ajali hiyo. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amezungumza mara kadhaa namna ambavyo alikuwa anapigiwa simu na Rais.

Kwa ujinga wangu na akili zangu fupi ambazo zinashindwa kuwaza mbali, baada ya kutokea ajali hiyo nikawa najiuliza maswali mengi lakini sikuwa na majibu yake. Sitaki kujiuliza tena maana najua sitaweza kujijibu mwenyewe. Acha nikae kimya huenda ninayojiuliza kuna watu wenye akili nyingi na maarifa nao wanajiuliza kama mimi. Lakini Najua watakuwa na majibu.
Kwa mfano swali la kwanza kujiuliza ndani ya Kivuko kulikuwa na watu wangapi? Nilijiuliza swali hili zaidi ya mara 100 sikuwa na majibu. Hata hivyo jibu nikajakulipata baadae kwamba idadi ya watu waliokuwa kwenye Kivuko hicho siku ya tukio walikuwa zaidi ya 265.

Baada ya kufahamu idadi ya watu...nikajiuliza tena wakati wanaingia walipita wapi? Walipita njia sahihi au? Wahusika wa Kivuko hicho wanajua idadi halisi ya waliokuwa wanatakiwa kubebwa na Kivuko? Kama walikuwa wanajua kwanini waliacha watu wote wakaingia?

Ulikuwa mpango maalum? Kwanini hawakuchukua tahadhari? Yaani najiuliza maswali mengi mengi mnooo… Ndio maana nasema acha nikae kimya tu. Najua ipo Tume ambayo imeundwa kuchunguza ajali ya MV.Nyerere.Hata hivyo kwa nafasi yangu ninayo nafasi ya kujadili kama ambavyo wengine wanajadili. Kwani kuna ubaya gani? Naomba niseme tu siingilii  Tume inayochunguza ajali hiyo maana sijui wao wanauliza maswali ya aina gani. Wakiuliza kama yangu nayo si tatizo.

Sitaki kuzungumza. Naomba niwe mkweli tayari tumeelezwa kuwa uwezo wa Kivuko cha MV. Nyerere ilikuwa ni kubeba watu 101. Hivyo siku ambayo Kivuko hicho kimepinduka kulikuwa na idadi ya watu zaidi ya 265. Najuliza kwanini iwe hivyo? Huenda nikawa na jibu langu acha nawe msomaji uwe na jibu lako.


Ukweli utabaki kuwa kivuko hicho kilibeba idadi ya watu tofauti na uwezo wake. Hiki ni chanzo namba moja cha Kivuko hicho kupinduka. Najua watalaam wanayo nafasi ya kufanya uchunguzi wao na kuja na majibu halisi ya kilichosababisha ajali.
Rais wangu Dkt. Magufuli wakati anazindua Flyover ya Mfugale iliyopo makutano ya Tazara jijini Dar es Salaam amewaambia Watanzania kila mmoja kwa nafasi yake ajitafakari.

Nami kama Mtanzania nikaanza kuitafakari kauli ya Rais ya kututaka sote tujitafakari kuhusu ajali ya MV.Nyerere.Kuna somo la kujifunza kutokana na ajali ya MV. Nyerere. Hata hivyo swali la msingi la kujiuliza tumejifunza nini? Jibu la swali hili nadhani kila mmoja atakuwa na lake.

Kwangu mimi nilichojifunza kuna uzembe wa kusimamia Sheria, Kanuni na Taratibu kuhusu vivuko. Si vyote. Ni kwa hicho cha MV Nyerere. Sitaki ugomvi wala shari na mtu. Pia nimejifunza iko haja ya kuhakikisha Sheria, Kanuni na Taratibu zinaheshimiwa. Tukifuata sheria naamini tutakuwa salama na tutaepuka ajali.  Kwa kuwa kuna tume inachunguza acha hili nisiendelee kulizungumza. Tutafahamu ukweli wakati ukifika.

Binafsi maisha yangu ni Dar es Salaam. Kwa wanaoishi katika Jiji la Dar es Salaam wanafahamu changamoto za usafiri. Idadi ya abiria ni kubwa kuliko magari ya abiria yaliyopo. Juhudi za kuondoa changamoto ya usafiri zinaendelea kuchukuliwa. Ni jambo la kawaida siku hizi kuchagua unataka kupanda Daladala, Mabasi ya Mwendo kasi au Treni.

Pamoja na kuwa na usafiri huo kuna swali ambalo najiuliza na kutafakari. Inahusu idadi ya abiria ambao wanatumia vyombo hivyo vya usafiri. Ukweli ni kwamba mabasi ya mwendo kasi yanabeba idadi kubwa sana ya watu. Nafahamu kwamba basi moja linauwezo wa kubeba abiria kati ya 150 hadi 160.

Kwa ujinga wangu huwa najaribu kuangalia idadi ya watu inayokuwemo na kinachonijia ni kwamba idadi ya watu ni kubwa huenda kuliko uwezo wa Basi la Mwendo kasi. Watu wanajazana kiasi cha milango kushindwa kufunga hadi watu walazimishe kujibana. Tena kwa taabu.

Wananchi tupo...tunaona na wala hakuna anayekemea.Kila mmoja anawaza kurudi nyumbani au kwenda kazini.Hakuna anayefikiria kuhusu usalama wa maisha yake. Siombi yatokee lakini ni vema tukachukua tahadhari mapema. Ukienda kwenye kituo  cha mabasi ya mwendo kasi utakachoshuhudia ni namna ambavyo mamia ya wananchi wanakata tiketi na kuingia kituoni.

Nani anasimamia  wanaoingia kwenye basi? Hilo hakuna anayefikiria.Kwenye mwendo kasi hata basi likajaa vipi ukifanikiwa kukanyaga mguu basi unaoenda utafika.Ni hatari .Tena hatari sana .Hakuna anayezungumza sote tuko kimya. Tunasubiri litokee jambo baya ndio tuanze kusema. Tuanze kusema mapema kama sehemu ya tahadhari kwetu.

Nenda kwenye treni zinazotoa huduma ya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam. Watu wanajazana .Nikiri sina utalaam na sifahamu idadi ambayo inatakiwa katika Behewa moja. Lakini kwa ujina wangu au sijui ndio uoga huwa naona kabisa idadi ya watu inayobebwa ni kubwa mno.

Ni usafiri ambao ninautumia mara kwa mara. Naishi Gongo la Mboto. Hivyo angalau naujua usafiri wa Treni. Ni usafiri ambao ukiingia una uhakika wa kufika nyumbani kwa wakati. Hivyo umekuwa usafiri pendwa na matokeo yake watu tunajazaa. Yaani tunajaza haswaaa. Kwa kuwa tunakwenda na kurudi tumebaki kimya tu. Tunajiona tuko salama.

Achilia mbali Treni na Mwendo kasi. Nenda kwa wanaokaa Mbagala . Huko balaa. Kuingilia dirishani ni jambo la kawaida. Mlango wa kazi gani na huo unawahusu wenye nguvu. Kimbaumbau kama mie mbona mwendo wa dirishani tu. Hapo sifikiri kukaa kwenye siti a.k.a kiti.

Unaweza kusema napiga stori za uongo. Kwa wanaoishi maeneo ya Mbagala wanajua ninachokizungumzia. Hali ni mbaya. Namshukuru Rais wangu amezungumzia mikakati ya kuboresha usafiri kwa wakazi wa Mbagala kwa kujengwa kwa barabara ya mabasi ya Mwendo kasi. Yataanzia Gegerezani hadi Mbagala. Alau itapunguza ukubwa watatizo.

Pamoja na hayo ni vema katika dhana ile ile ya kutafakari ajali ya MV. Nyerere kama sehemu ya kujifunza basi kwa Dar es Salaam tutafakari kuhusu idadi kubwa ya abiria ambayo wanajazana kwenye vyombo vya usafiri.K una mambo mengi ya kuzungumza lakini niseme tu nadhani nimeeleweka. Kwanza nimechoka kuandika .


Najua nawe umechoka kusoma. Hata hivyo nihitimishe kwa kusema  Treni na Mabasi ya mwendo kasi ni janga jingine ambalo lazima tuchukue tahadhari mapema tubaki salama. Maisha matamu bwana asikwambie mtu. Hivi hata hiki nilichoandika unataka kutuma maoni.

Aya nipo kwenye
0713833822

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad