HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, October 29, 2018

MWIJAGE: VIWANDA VIDOGO, BIASHARA NDOGO VINA MCHANGO MKUBWA KATIKA UCHUMI, MAENDELEO, USTAWI WA NCHI

Na Stella Kalinga, Simiyu
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage amesema viwanda vidogo na vya kati vina mchango mkubwa katika uchumi, maendeleo na  ustawi wa nchi yoyote, kwa kuwa vinatoa ajira kwa watu wengi ikilinganishwa na viwanda vikubwa hivyo havipashwi kubezwa kwa namna yoyote.

Mhe. Mwijage ameyasema hayo Oktoba 28, 2018 wakati akihitimisha Maonesho ya Viwanda Vidogo Kitaifa yaliyofanyika Kitaifa kwa mara ya kwanza katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu kuanzia Oktoba 23.

“ Najua kuna watu wanapenda kubeza lakini napenda niwaeleze nafasi ya viwanda na biashara ndogo katika uchumi, maendeleo na ustawi ya nchi yoyote, Sisi Tanzania tangu uhuru mpaka leo tuna viwanda 54,000, lakini asilimia 99 ni viwanda vidogo, vidogo sana na vya kati; sisi siyo kilema kwenye viwanda nchi zote zipo hivyo, viwanda vyenye tija  na vinavyoajiri watu wengi ni viwanda vidogo, vidogo sana na vya kati” alisema Mwijage.

 Amesema pamoja na viwanda vidogo na vidogo sana kuwa na tija katika uchumi wa nchi viwanda hivyo pia ni shule na vinaweza kumilikiwa kirahisi huku akisisitiza kuwa lengo la Serikali ni kujenga uchumi jumuishi ambao nji rahisi ya kuufikia ni kupitia uchumi wa viwanda.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo(SIDO), Prof.Sylvester Mpanduji ametoa wito kwa Watanzania kuwa, ili waweze kushiriki katika Ujenzi wa Uchumi waViwanda hawana budi kuanza na viwanda vidogo ambavyo SIDO itakahakikisha vinakuwa endelevu.

Akizungumzia Maonesho ya Viwanda Vidogo Prof. Mpanduji amesema yamesaidia kuwaleta wajasiriamali pamoja kuonesha bidhaa zao na kubadilisha uzoefu katika teknolojia, usindikaji na masuala mengine yanayohusu bidhaa wanazozalisha kupitia viwanda vidogo na vya kati.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amesema mkoa huo umebeba ajenda ya Tanzania ya viwanda huku akibainisha kuwa  mwaka 2019 Simiyu imedhamiria Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli atakapotembelea mkoa huo afanye uzinduzi wa Falsafa ya Wilaya Moja Bidhaa Moja  kwa kufungua kiwanda katika kila wilaya.

Aidha, Mtaka amemhakikishia Waziri Mwijage kuwa Simiyu itaongeza uzalishaji wa malighafi ya viwanda hapa nchini mara mbili na kuomba wizara ya viwanda isaidie upatikanaji wa teknolojia za viwanda kuja nchini.

Akizungumzia dhamira ya kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika Ujenzi wa Uchumi wa viwanda Mkurugenzi Msaidizi wa UNDP anayeshughulikia miradi Amoni Manyama, amesema Shirika hilo liko tayari kushirikiana na Mkoa wa Simiyu na mikoa mingine nchini, katika nyanja ya kifedha na kitaalam kwa kufanya uchambuzi wa viwanda vinavyowezekana katika mikoa mbalimbali.

Maonesho ya Viwanda Vidogo ambayo yamefanyika Kitaifa kwa mara ya kwanza, chini ya kauli mbiu “PAMOJA TUJENGE VIWANDA KUFIKIA UCHUMI WA KATI” yameshirikisha wajasiriamali 515 kutoka mikoa 23 hapa nchini na nchi jirani za Burundi na Uganda, ambapo pia Mabalozi kutoka nchi za Nigeria na Angola walishiriki.
  Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akimkabidhi nakala ya Mwongozo wa Uwekezaji  wa Mkoa huo Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage wakati wa Kilele cha Maonesho ya Viwanda Vidogo (SIDO) yaliyofanyika Kitaifa  katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani humo,kuanzia Oktoba  23 na kuhitimishwa Oktoba 28, 2018(kulia) Balozi wa Nigeria nchini Tanzania, Mhe. Dkt. Shahabi Issa Gada.
 Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage akizungumza na wajasiriamali mara baada ya kutembelea mabanda yao katika Kilele cha Maonesho ya Viwanda Vidogo (SIDO) yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Simiyu katika Viwanja vya Nyakabindi,kuanzia Oktoba  23 na kuhitimishwa Oktoba 28, 2018.
 Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage akizungumza na baadhi ya viongozi wa World Vision na Halmashauri ya Wilaya ya Itilima alipotembelea banda lenye bidhaa za sabuni zinazozalishwa kupitiakiwanda kidogo kilichopo wilayani Itilima, katika Kilele cha Maonesho ya Viwanda Vidogo (SIDO) yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Simiyu katika Viwanja vya Nyakabindi, kuanzia Oktoba  23 na kuhitimishwa Oktoba 28, 2018.
 Viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage (mwenye tai) na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) wakiimba pamoja na Kwaya ya Walimu Bariadi, katika Kilele cha Maonesho ya Viwanda Vidogo (SIDO) yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Simiyu katika Viwanja vya Nyakabindi, kuanzia Oktoba  23 na kuhitimishwa Oktoba 28, 2018.
 Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera akiwasalimia wananchi wakati wa Kilele cha Maonesho ya Viwanda Vidogo (SIDO) yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Simiyu katika Viwanja vya Nyakabindi, kuanzia Oktoba  23 na kuhitimishwa Oktoba 28, 2018.  
 Kikundi cha Ngoma cha BASEKI kikitoa burudani katika Kilele cha Maonesho ya Viwanda Vidogo (SIDO) yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Simiyu katika Viwanja vya Nyakabindi, kuanzia Oktoba  23 na kuhitimishwa Oktoba 28, 2018.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad