HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, October 29, 2018

DAWASA Yawahakikishia Wakazi wa Dar es Salaam na Pwani Huduma Bora ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) imedhamiria kuendelea kuimarisha huduma zake katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano hasa katika ujenzi wa Viwanda kwa kuhakikisha kuwa huduma hiyo inafika maeneo ya Viwanda na kwa wananchi kwa kiwango kinachotakiwa.

Akizungumza katika kipindi cha mizani kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Afisa  Mtendaji mkuu wa Mamlaka hiyo Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema kuwa wamejipanga kuhakikisha kuwa maeneo yote yanafikiwa na huduma ya maji safi na salama yakiwemo ya Viwanda na maeneo ya pembezoni  mwa Jiji la Dar es Salaam ambapo tayari hatua zimechukuliwa katika kutekeleza azma hiyo.

 “Tumejipanga kuhakikisha kuwa  hata wananchi wasio na uwezo  wanafikiwa na huduma ya maji kwa njia ya mkopo ambapo tunawaunganishia maji na wanalipia kidogo kidogo hivyo mwananchi hatakuwa na sababu ya kukosa maji na hii ndiyo dhamira ya Serikali yetu;” Alisisitiza  Mhandisi Luhemeja.

Aliongeza kuwa Mamlaka hiyo pia ina miradi yakupeleka maji katika maeneo rasmi ya viwanda katika mkoa wa Pwani ambapo kuna miradi katika Wilaya za Kisarawe, Kibaha,Bagamoyo na Mkuranga ili kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Akifafanua Mhandisi Luhemeja amesema kuwa tayari  maeneo ya pembezoni yakiwemo Kiwalani, Ukonga, Salasala na Mbagala yameanza kunufaika na mpango wa kuhakikisha kuwa wananchi ambao hawajafikiwa na huduma hiyo wanafikiwa ili waweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi na uzalishaji.

Akitolea mafano wa hatua zinazochukuliwa katika  kuimarisha huduma ya maji katika Wilaya ya Kigamboni Mhandisi Luhemeja amesema kisima cha Gezaulole kimeshafungwa pampu na mtandao  wa mabomba utawekwa ili maji yatakayozalishwa yasambazwe katika eneo hilo ikiwa ni hatua mojawapo yakuondokana na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama

“ Upanuzi wa mfumo wa usambazaji maji kati ya Changanyikeni hadi Bagamoyo kwa ufadhili wa Benki ya Dunia unaendelea kwa kuongeza mtandao wa kusambaza maji ambao  utachangia kuondoa changamoto ya upotevu wa maji “,Alisisitiza Luhemeja.

Akizungumzia suala la watu binafsi kumiliki visima na kuuza maji Luhemeja amesema kuwa Mamalaka yake inachukua hatua madhubuti kuhakikisha kuwa maji hayo ni salama kwa matumizi ya wananchi  na si vinginevyo.

“Maji yanayosambazwa kwa wananchi lazima yakizi vigezo, DAWASA itapima maji hayo na kama hayakidhi vigezo basi visima husika vitafungwa ambapo kwa sasa tutasajili upya visima vyote vya watu binafsi wanaofanya biashara ya kuuza maji;’’Alisisitiza Luhemeja.
Kwa upande wa majitaka Mhandisi  Luhemeja amesema kuwa huduma hiyo inapanuliwa kwa kununua magari 20 ya kunyonya maji taka hali itakayopanua wigo wa huduma hiyo kwa wananchi na pia mifumo 9 ya majitaka imeanza kukarabatiwa ili kuweza kupokea na kutibu majitaka.

 Mamlaka hiyo imebuni mikakati mbalimbali ya kuimarisha utendaji  wake na huduma zake kwanza kwa kuanzisha kituo cha huduma kwa wateja, kuweka mikakati ya makusudi kuhakikisha kuwa wananchi wa pembezoni wanafikiwa na huduma ya maji, kuimarisha miundombinu, kuzuia uvujaaji wa maji, kuongeza mapato na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza maji kupitia katika Kampeni maalum itakayoendeshwa katika shule za mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ili kujenga utamaduni wa kulinda na kutunza maji na miundombinu.

DAWASA imekuwa ikiimarisha utendaji wake ili kuendana na azma ya Serikali kuhakikisha kuwa wananchi wanafikiwa na huduma ya maji safi na salama katika maeneo yao na kwa wakati.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad