HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, 28 August 2018

Waziri Mwakyembe akutana na Wamiliki wa Televisheni nchini

Na Immaculate Makilika na Bushiri Matenda- MAELEZO
Serikali imesema kuanzia septemba 5, mwaka huu visimbuzi vitaanza kuonesha channeli zote za ndani bila kutoza gharama yoyote kwa mtazamaji.

Akiwaeleza waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, kuhusu yaliyozungumzwa katika kikao kati ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe na wadau na wamiliki wa televisheni nchini, Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa serikali imefikia uamuzi huo baada ya visimbuzi vya AZAM, ZUKU na DSTV kutoonesha channeli za ndani, kulingana na aina ya leseni zao.

“Ningependa watanzania wafahamu kwamba kuanzia septemba 5 mwaka huu, visimbuzi vya TIN, Starmedia, Continental na Digtek vitaonesha takribani channeli 34 za ndani bure, ili kutoa fursa ya kila mwananchi kuwa na haki ya kupata taarifa” alisema Dkt. Abbasi

Aidha, alielezea kuwa wadau hao na wamiliki wa televisheni wameonesha kuridhishwa na hatua hiyo ya kwa vile Serikali imetengeneza miundombinu itanayoruhusu channeli zao kuonekana nchi nzima.

Dkt. Abbasi, alisisitiza kuwa “nchi imeandaa mfumo, ambao unaweza kufanyakazi bila kutegemea kampuni kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuonesha channeli za ndani au matangazo, kwa hivyo wadau au wamiliki wa vyombo vya habari wasihofu kuhusu hilo”

Kikao kati ya Waziri Mwakyembe na wadau na wamiliki wa televisheni nchini, kimefanyika kwa lengo la kuwa na majadiliano ya pamoja baina serikali na wadau hao ili kupata muafaka kuhusu kutooneshwa kwa chaneli za ndani katika visimbuzi vilivyokiuka masharti ya leseni zao.

Aidha, kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Injinia James Kilaba, pamoja na wataalamu wake.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe (katikati) akizungumza na wawakilishi wa wamiliki wa televisheni nchini (hawapo pichani) wakati alipokutana nao mapema hii leo jijini Dar es Salaam ili kusikiliza matatizo ya visimbuzi, kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), Mhandisi James Kilaba na kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi (kushoto) akizungumza na wawakilishi wa wamiliki wa televisheni nchini (hawapo pichani) wakati Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe (katikati) alipokutana nao mapema hii leo jijini Dar es Salaam ili kusikiliza matatizo ya visimbuzi, kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), Mhandisi James Kilaba.

Baadhi ya wawakilishi wa wamiliki wa televisheni nchini wakimsikiliza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe (hayupo pichani) wakati alipokutana nao mapema hii leo jijini Dar es Salaam ili kusikiliza matatizo ya visimbuzi.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad