HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, August 22, 2018

WAKAZI WA KILAMBO MKOANI MTWARA WAOMBA KIWANDA CHA KUSINDIKA MAZAO YA KILIMO

Na Benny Mwaipaja, WFM, Mtwara
WAKAZI wa Kijiji cha Kilambo, Wilaya ya Mtwara, mkoani Mtwara, wameiomba Serikali iwasaidie kuwatafutia mwekezaji atakayejenga kiwanda cha kusindika matunda na mazao ya kilimo katika kijiji chao kutokana na kijiji hicho kuwa na matunda na mazao mbalimbali yanayokosa soko na kuwasababishia umasikini.

Wakazi hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilambo Bw. Mohamed Mkama, wametoa ombi hilo mbele ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, aliyefanya ziara ya kikazi katika Kituo cha Forodha cha Kilambo, kilichoko mpakani mwa Tanzania na Msumbiji, mkoani Mtwara,  kwamba kijiji chao kina fursa nyingi za kilimo zinazohitaji viwanda vya kuongeza thamani ya mazao yao na kutoa ajira kwa vijana.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilambo Bw. Mohamed Mkama, alisema kuwa Kijiji chao kinapakana na nchi ya Msumbiji ambako kuna mwingiliano mkubwa wa watu katika masuala ya biashara na uhusiano wa kijamii ikiwemo pande

mbili za nchi kuoleana hivyo kuwafanya wananchi wa Msumbiji waishio mpakani kutegemea bidhaa kwa wingi kutoka katika kijiji chao.

"Watu kutoka Msumbiji wananunua sana chakula na bidhaa nyingine kutoka kwetu lakini tunawauzia bidhaa bila kuongeza thamani hivyo uwepo wa kiwanda utakuza uchumi wa kijiji chetu na tunakuomba Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango, utusaidie kupata kiwanda ili nasi tuweze kunufaika" alisisitiza Mwenyekiti huyo wa Kijiji

Mkazi mwingine wa Kijiji hicho  Bw. Selemani Kumamba, alimweleza Waziri wa Fedha na Mipango kwamba Kijiji chao ni maarufu kwa kilimo cha matunda hivyo wanapendekeza kujengwa kwa kiwanda cha kusindika matunda ili juisi itakayozalishwa katika kijiji chao iwe na soko.

"Mhe. Waziri sisi ni wakulima wazuri wa matunda lakini matunda yetu wakati wa msimu yanakosa soka, yanaoza  na tunayatupa jambo linalotulazimu tukuombe utusaidie kuhamasisha wawezezaji waje wajenge kiwanda cha kusindika juisi katika kijiji chetu ili nasi tuondokane na umasikini" alisema mzee Selemani Kumamba

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, aliwaambia wakazi hao kwamba inabidi ufanyike utafiti wa kutosha ili kubaini wingi wa mazao yanayozalishwa na wakulima katika kijiji hicho na vijiji jirani ili kupata takwimu sahihi za uzalishaji wa mazao hayo yakiwemo matunda ili kuiwezesha Serikali kuwashawishi wawekezaji kujenga kiwanda katika eneo hilo na kuwapongeza wakulima hao kwa kufanya kazi kwa bidii na mawazo yao ya kujiletea maendeleo.

"Tukiwa na uhakika huo hata mwekezaji anayekuja tutamwambia kwa mwaka mmoja, kwa wastani, kijiji hiki na vijiji jirani vinazalisha maenbe kiasi fulani, kwa hiyo wazo la kutaka kuwa ni kiwanda ni  zuri lakini linahitaji kufanyiwa kazi zaidi" alisema Dkt. Mpango aliyeambatana na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Bw. Evod Mmanda

Aliwasahauri wanakijiji hao kuanzisha mashamba mapya ya matunda na kupanda mbegu za kisasa zinazozaa kwa wingi na kuushauri uongozi wa wilaya kuwasaidia wananchi hao kupata miche ya kisasa inayozaa kwa muda mfupi ili waweze kushawishi zaidi kupatikana kwa kiwanda kijijini hapo.

Dokta Philip Mpango, yuko mkoani Mtwara kwa ziara ya kikazi ambapo pamoja na mambo mengine amekutana na wafanyabiashara wa mkoa wa Kigoma pamoja na Kutembelea taasisi zilizochini ya Wizara hiyo.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kushoto), akitoka kukagua Kituo cha Forodha na Ushuru cha Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA katika Mpaka wa Tanzania na Msumbiji (Kilambo), alipofanya ziara na kuzungumza na wafanyakazi wa Kituo hicho, mkoani Mtwara.
Meneja wa Kituo cha Forodha na Ushuru cha Kilambo, mpakani mwa Tanzania na Msumbiji mkoani Mtwara Bw. Emmanuel William (wa tatu kulia), akitoa maelezo ya eneo jipya la ujenzi wa Ofisi za Kituo hicho katika Kijiji cha Kilambo, mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.
Meneja wa Kituo cha Forodha na Ushuru cha Kilambo, mpakani mwa Tanzania na Msumbiji mkoani Mtwara Bw. Emmanuel William (kulia), akitoa maelezo ya eneo jipya la ujenzi wa Ofisi za Kituo hicho katika Kijiji cha Kilambo, mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb),  akitembelea maeneo mbalimbali ya  Kituo cha Forodha katika Mpaka wa Tanzania na Msumbiji- Kilambo Mkoani Mtwara.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Bw. Evod Mmanda (kulia) akitoa maelezo kwa Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani) kuhusu uhitaji wa Ofisi za Kituo cha Forodha katika Mpaka wa Tanzania na Msumbiji- Kilambo, Mkoani Mtwara ili kurahisisha utendaji katika kudhibiti magendo na ukusanyaji wa mapato wakati wa ziara ya Waziri huyo alipokwenda kujionea hali halisi ya mpaka huo.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akisalimiana na Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilambo Bw. Mohammed Mkama, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mtwara kukagua pamoja na mambo mengine, Kituo cha Forodha na Ushuru cha Kilambo, kilichoko katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji.
Diwani wa Kata ya Tangazo Bw.(kushoto), akijadili jambo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), alipokutana na wakazi wa Kijiji cha Kilambo, akiwa katika ziara yake ya kukagua Kituo cha Forodha na Ushuru-Kilambo, kilichoko mpakani kwa Tanzania na Msumbiji.
Wazee wa Kijiji cha Kilambo wakimpongeza Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) kwa utendaji wake mzuri wa kazi, alipofanya ziara ya kutembelea Kituo cha Forodha katika Mpaka wa Tanzania na Msumbiji- Kilambo Mkoani Mtwara.
Mzee Seleman Kumamba (kushoto) akizungumza na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), ambapo alimuomba Waziri huyo kuangalia uwezekano wa kuweka kiwanda katika eneo hilo  kikiwemo cha kusindika matunda kwa kuwa watanufaika kutokana na soko la mazao yao lililopo nchi jirani ya Msumbiji.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akisalimiana na watumishi wa umma katika Mpaka wa Tanzania na Msumbiji- Kilambo Mkoani Mtwara alipofanya ziara na kukagua shughuli mbalimbali katika Mpaka huo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad