HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, 28 August 2018

TRC WADHIBITI WIZI WA MAFUTA KATIKA UJENZI RELI YA KISASA

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania(TRC) Masanja Kadogosa akizungumza kabla ya kuanza ziara ya kutembelea mradi wa reli ya kisasa iliyofanyika leo Augusti 28,2018 kuanzia Shaurimoyo  mpaka Kilosa mjini morogoro.
 Meneja Mradi mradi wa reli ya kisasa ya standard gauge, Injinia Maizo Mgedzi akizungumza kabla ya kuanza ziara ya kutembelea maradi wa Reli ya kisasa ambayo itaanzia Dar es Salaam mpaka morogoro na baadae kuanzia Morogoro mpaka Dodoma. Ziara hiyo iliyohusisha wakurugenzi wa bodi ya wakurugenzi wa shirika la reli Tanzania leo Augusti 28,2018.
 Wajumbe wa Bodi ya wakurugenzi wa shirika la Reli Tanzania wakisikiliza maelezo ya mradi kabla ya kuanza ziara ya kutembelea mradi wa Reli ya kisasa.
 Meneja Mradi mradi wa reli ya kisasa ya standard gauge akitoa maelezo ya mradi wa Reli ya kisasa jijini Dar es Salaam leo mara baada ya kuanza ziara ya kutembelea mradi wa reli ya kisasa leo Augusti 28,2018.
 Reli ya kati ambapo reli ya kisasa.
Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi, Profesa John Kondoro akizungumza wakati ziara ikiendelea leo Augusti 28,2018 ya kutembelea ujenzi wa reli ya kisasa.
  Baadhi ya maeneo ambayo reli ya kisasa yatapita chini ya ardhi.
 Ujenzi wa reli ya kisasa ukiendelea

 Mradi mradi wa reli ya kisasa ya standard gauge ulipofikia baadhi ya maeneo.

 Mataaluma yakiwa tayari kwaajili ya kwenda kuwekwa kwenye maeneo ambayo reli ya kisasa itapita.

Maeneo yanayoendelea kujengwa reli ya kisasa eneo la Mlandizi.
Picha na Avila Kakingo, Globu ya jamii.

*Mkurugenzi Mtendaji Kadogosa asema ujenzi umekamilika kwa asilimia 22

*Wajumbe Bodi ya Wakurugenzi washuhudia kasi ya ujenzi kuanzia Dar 

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii.
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania(TRC) Masanja Kadogosa amesema kwa sasa wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti wizi wa mafuta huku akieleza kuna baadhi ya madereva wamefukuzwa kazi kutokana na tuhuma hizo.

Kadogosa amesema hayo leo katika eneo la Soga mkoani Pwani ambapo kuna kambi ya wafanyakazi wanaojenga Reli ya Kisasa ambapo ameelezea namna ambavyo wamedhibiti wizi wa mafuta kwa kuimarisha ulinzi kwa kushirikiana na mamlaka za ulinzi na usalama.

Sababu za kuelezea hayo ni baada ya baadhi ya waandishi waliokuwa kwenye ziara ya Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRC  wakiongozwa na Mwenyekiti wao Profesa John Kondoro kutaka kufahamu hali kutokana na kuwepo kwa taarifa za uwepo wa wizi wa mafuta.

"Tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti wizi wa mafuta katika mradi huu.Ni tofauti na hapo awali, tumeimarisha ulinzi na sasa tumefanikiwa kudhibiti wizi huo.

"Kuna watu 30 wamekamatwa kwa tuhuma za wizi wa mafuta na tayari wamefunguliwa kesi.Pia katika kukomesha vitendo vya wizi kuna baadhi ya madereva ambao tumewafukuza,"amesema Kadogosa.


VIPI KUHUSU UJENZI WA RELI?
Akizungumzia ujenzi wa reli hiyo ya kisasa ambayo awamu ya kwanza ni kutokea Dar es Salaam hadi Morogoro, Kadogosa amewaeleza wajumbe wa bodi hiyo  kwamba ujenzi umekamilika kwa asilimia 22.

Amesema katika ujenzi wa reli hiyo kuna hatua mbalimbali za ujenzi zinazoendelea na kila eneo kwa asilimia tofauti na eneo jingine lakini kwa ujumla wake ujenzi umefikia asilimia 22 na ujenzi unaendelea kwa kiwango cha kuridhisha.

Ameongeza ujenzi wa madaraja unaendelea na tayari zimeanza kuwekwa , ujenzi wa tuta nao unaendelea na maeneo maeneo mengine wameanza kuweka kokoto kwa ajili ya kuanza kutandika mataluma.

"Kasi ya ujenzi wa reli ya kisasa inakwenda vizuri, ratiba ya ujenzi huu unatakiwa kukamilika Novemba mwaka 2019, hivyo kazi inaendelea na ujenzi unafanyika usiku na mchana na sisi TRC muda wote tumekuwa tukifuatilia tena hatua kwa hatua,"amesema Kadogosa.

Ametumia nafasi hiyo kusisitiza wanafanya kazi kwa saa 24 kwani changamoto ya mvua ilisababisha kutofanyika kazi za ujenzi na hivyo wamemua kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati.


UNAZUNGUMZIAJE UJENZI STESHENI YA DAR?
Kadogosa amefafanua kwamba ujenzi wa stesheni ya Dar es Salaam na maeneo mengine ya mradi huo yamezingatia uhalisia wa Mtanzania na kwamba kabla ya kuanza ujenzi huo walimtaka mtalaamu kuonesha ramani ya majengo atakayojenga.

Amesema hata baada ya kuangalia walimtaka ajenge majengo ambayo yataonesha uhalisia wa nchi yetu.Pia amesema maeneo ya Stesheni baada ya kukamilika mbali ya kuwa sehemu ya abiria yatakuwa na maeneo ya mahitaji yote muhimu.

"Kwa Stesheni ya Dar es salaam kutakuwa na eneo kwa ajili ya abiria, kutakuwa na hoteli, kutakuwa na maeneo ya maduka makubwa ya kisasa na na maduka ya kawaida.Kutakuwa na ofisi mbalimbali za watumishi pamoja na kumbi za mikutano.

"Tunataka maeneo ya Stesheheni hata kama kutakuwa hakuna treni basi shughuli nyingine za kiuchumi ziendelee,"amesema Kadogosa na kufafanua katika maeneo mengine ya vituo vya treni kutakuwa na majengo yanayofanana na nyumba za kabila la Wamasai na Wagogo na yote hiyo ni katika kuonesha uhalisia.


MAANDALIZI YAKOJE?
Kuhusu maandalizi, Kadogosa amesema kuna mikakati mbalimbali inayoendelea ikiwamo ya kuandaa watalaam wataokaofanya kazi ya kuendesha treni hiyo baada ya ujenzi wake kukamilika.

Amesema kuna baadhi ya watalaam wa TRC ambao wameanza kupatiwa mafunzo kwa ajili ya kuusimamia mradi huo na baadhi yao watakwenda kujifunza nje ya nchi na hasa katika nchi ambazo wanao uzoefu wa kusimamia treni za aina hiyo.

Pia amesema kuna watalaam ambao watakuja nchini kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa watalaam wazawa huku akielezea kuwa kuna vijana 160 kutoka vyuo vikuu hapa nchini wameanza kupewa mafunzo ya nadharia na kisha watapewa mafunzo kwa vitendo.

"Tunataka mradi huu utakapoanza basi tuwe na watalaam wetu ambao watasimamia shughuli mbalimbali .Hivyo tumeedelea kujieandaa na tunakwenda vizuri sana,"amesema Kadogosa.


HALI IKOJE KWA WAZAWA?
Katika hilo Kadogosa amesema kwamba kwa mujibu wa mkataba uliopo unaeleza wazi kwamba katika ujenzi wa reli hiyo ushiriki wa Watanzania ni asilimia 80 na iliyobaki ni ya wageni.

Amesema hadi sasa ujenzi huo ukiwa umekamilika kwa asilimia 22 idadi ya Watanzania ambao wanashiriki katika ujenzi wa reli hiyo ni asilimia 92 na asilimia iliyobakia ni wageni.

"Katika kila eneo la ujenzi wazawa ni wengi kuliko wageni.Hivyo tumevuka lengo ambalo lipo kwenye mkataba wetu.Wazawa wanashiriki kikamilifu,"amesema Kagogosa wakati anatoa maelezo ya ujenzi huo kwa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa TRC.

TUMESHAWAHI KUJENGA RELI KWA FEDHA ZETU?
Katika hilo Kadogosa amesema kuwa ujenzi wa reli hiyo ya kisasa ni wa kihistoria kwani kama Taifa ndio ujenzi wa reli ambayo unafanywa na Watanzania wenyewe kupitia fedha zao.

"Hii ndio reli yetu ya kwanza kuijenga kwa fedha zetu kama Taifa.Reli ambayo tunatumia ilijengwa na wakoloni miaka ya nyuma lakini hatimaye Taifa la Tanzania limeamua kujenga reli ya kisasa tena kwa fedha zake.Hili ni jambo la kujivunia,"amesema Kadogosa wakati anazungumzia ujenzi wa reli hiyo.


NINI MAONI YA PROF.KONDORO?
Akizungumza baada ya kukagua ujenzi huo kuanzia Shaurimoyo jijini Dar es Salaam hadi Soga mkoani Pwani Profesa Kondoro amemetoa maoni yake kuwa ameridhishwa na kasi ya ujenzi huo.

Amesema kuwa lengo la ziara yao ambayo ni ya kawaida ni kutoaka kuona kwa uhalisia shughuli za ujenzi huo na kwamba inawapa nafasi ya kuangalia ripoti ambazo wanazo kwenye makaratasi na uhalisia wa ujenzi huo.

"Kwetu sisi wajumbe wa bodi tumeridhika na kasi ya ujenzi wa reli hii.Kwa matamanio ambayo tunanayo tunatamani mradi huu ungekabidhiwa jana lakini kwasababu ujenzi ni mambo ya kitalaam basi tunaacha utalaalam uchukue nafasi yake,"amesema Profesa Kondoro.

Ameongeza ujenzi huo upo katika hatua tofauti na kuna baadhi ya maeneo yanachangamoto zake kutokana na reli inakopita lakini wameridhishwa na maelezo ya wataalam wanaosimamia ujenzi wa reli hiyo.

2 comments:

Post Bottom Ad