HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, 28 August 2018

PANITA, ASASI ZA KIRAIA WATOA USHAURI KWA SERIKALI KUHUSU NAMNA BORA KUBORESHA HALI YA LISHE NCHINI

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii.

SERIKALI kupitia Halmashauri imeshauriwa kujenga tabia ya kutenga fedha kupitia mapato yao ya ndani ili kuweka mfumo thabiti na endelevu katika kuboresha hali ya lishe na ambao utajengeka juu ya msingi bora unaowekwa na fedha za wafadhili pindi miradi hii itakapokwisha.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa PANITA Tumaini Mikindo kwa niaba ya Asasi za kiraia ambazo zimejikita katika masuala ya lishe nchini wakati wa kikao kati ya na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi) Suleiman Jaffo.

Lengo la kikao hicho kimekutana kwa ajili ya kuifanya tathimini taarifa ya utekelezaji wa mkataba wa lishe baina ya Makamu wa Rais, Wakuu wa Mikoa wa Tanzania Bara na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali.

Hivyo Mikindo ameshauri ni vema pia halmashauri ziweke vipaumbele kwenye afua za lishe ambazo zitaleta matokeo chanya kwa haraka. Pia Serikali iongeze bajeti ya lishe kutoka Sh.1,000 ya sasa kwa mtoto hadi kufikia Sh. 23,000 ambayo ni takribani dola 8.5 za kimarekani kwa mwaka kwa kila mtoto chini ya miaka mitano na iwapo wanalenga kufikia maazimio ya Baraza la Afya Duniani (WHA) kuhusu lishe kufikia 2025. 

"Baada ya maneno haya machache namshukuru Waziri Jafo kwa kutushirikisha katika kikao hiki adhimu cha kujadili utekelezaji wa mkataba wa lishe,"amesema Mikindo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa leo kuhusu kikao hicho cha tathimini.

Awali wakati anaanza kuzungumza Mikindo amesema asasi za kiraia zinatoa shukrani kwa Waziri Jaffo kwa kuwaalika kwenye mkutano huo na kwao ni fursa ya kutoa maoni yao kuhusu lishe nchini.

"Hii ni uthibitisho tosha Serikali ya Awamu ya tano chini ya Rais Dk.John Magufuli inavyothamini na kutambua mchango wa wadau ikiwemo Asasi za kiraia katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya taifa hili kuelekea uchumi wa kati kupitia viwanda ifikapo 2025.Waziri tunaomba utufikishie shukurani zetu za dhati kwa Rais,"amesema. 

Aidha amesema wanamshukuru Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kwanza kwa kukubali kuwa kinara wa lishe na pili kwa kutimiza ahadi aliyoitoa siku ya uzinduzi wa ripoti ya lishe ya dunia nchini Tanzania Julai 20 mwaka 2016 jijini Dar es Salaam.

"Naomba nirejee baadhi ya maneno aliyoyatamka siku hiyo. Ninanukuu, “…Ni kweli kwamba kwenye “Political will” jambo lolote linaweza likafanyika; kwa hiyo niseme kwamba na hili suala la lishe tutalipa msukumo mkubwa wa kisiasa ili kila mmoja wetu aimbe lishe na kupunguza Utapiamlo,"amesema wakati anatoa nukuu hiyo.

Pia amesema Mama Samia alisema wakati wa uzinduzi huo kuwa viongozi wa Serikali watahakikisha wanatoa ushirikiano stahiki ili kuwezesha lishe kupata msukumo wa kipekee katika ngazi zote za maamuzi.

Mbali ya kumnukuu Makamu wa Rais, Mikindo amesema katika hotuba ya bajeti kuu ya fedha ya Serikali ya mwaka 2018/19 iliyosomwa na Waziri wa Fedha Dk.Philip Mpango kwa mara ya kwanza Serikali imetambua lishe kama moja ya vipaumbele vya kitaifa katika kufikia uchumi wa viwanda na kuhahidi kutoa msukumo wa kipekee katika kuborsha hali ya lishe nchini.

"Baada ya maneno haya kwa moyo dhati kabisa nimpongeze Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na Rais Dk.Magufuli na Serikali yote kwa ujumla kwa kulisimamia jambo hili kikamilifu.Ndio maana tupo hapa leo katika kikao hiki kupata tathimini ya utekelezaji wa mkataba huu kwa miezi sita ya mwanzo toka uliposainiwa mbele yako mwezi Desemba mwaka 2017,"amesema.

Amefafanua kwa hiyo kikao chao hicho ni muhimu kupitia yaliyotekelezwa na kama kuna mafanikio watapongezana na kama kuna changamoto basi watazitafutia suluhu kwa pamoja ili waweze kufikia malengo tarajiwa ya kuboresha hali ya lishe nchini Tanzania.

Ametumia nafasi hiyo kuelezea mambo machache ambayo ni muhimu katika kuboresha hali ya lishe nchini Tanzania ambapo amesema Serikali imetenga fedha katika bajeti kwa mwaka wa 
2017/18 zipatazo Sh.bilioni 11 katika ngazi za mikoa na wilaya kwa kigezo cha Sh.1000 kwa mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano. 

Amesema jambo hilo ni jema na linapaswa kupongezwa. Aidha utekelezaji wa bajeti hiyo unaonesha mambo kadha yakiwamo ya sehemu kubwa ya bajeti hiyo inatoka kwenye Mfuko wa Afya wa Pamoja (Health Basket Fund) ikifuatiwa na ruzuku ya Serikali Kuu kwenda halmashauri na kwa kiwango kidogo toka kwenye mapato ya ndani ya halmashauri. 

"Kwa kiasi kikubwa fedha ambazo zimetumika ni zile zinazotoka kwenye Mfuko wa Afya wa Pamoja (Health Basket Fund) ikifuatiwa na ruzuku ya Serikali kuu kwa kiasi kidogo na pengine zile zilizotengwa toka mapato ya ndani ya halmashauri zisitolewe kabisa,"amesema Mikindo .

Aidha amesema sehemu kubwa ya mipango na bajeti za lishe kwa ngazi ya wilaya haizingatii afua za lishe ambazo zingeweza kuleta matokeo chanya kwa haraka.

Pia mikoa ambayo inapata fedha za wafadhili au wadau wa maendeleo imekuwa haiweki fedha za vyanzo vya ndani katika bajeti za lishe au zikiweka basi ni kwa kiwango kidogo sana. 

"Hii inamaanisha nini? Kwa kipindi cha kati tutapata matokeo chanya kwa sababu fedha za wafadhili zipo. Lakini mafanikio haya hayatakuwa endelevu pindi miradi ya wafadhili itapomaliza muda wake,"amesema.

Awali imeepezwa pia mkutano ulioandaliwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na UNICEF Tanzania ulikuwa na malengo mahususi ambayo ni kuwasilisha utekelezaji wa afua za lishe na viashiria vilivyo kwenye Mkataba wa Makubaliano wa Masuala ya Lishe baada ye Miezi sita ya utekelezaji. 

Pia kujenga uelewa wa pamoja wa utekelezaji wa Viashiria vilivyoko katika Mkataba wa Lishe,kuongeza msukumo wa usimamizi na uelewa wa Masuala ya Lishe ili kupunguza kiwango cha Udumavu na Utapiamlo nchini. Na jambo lingine ni kufafanua madhara na hasara ya Udumavu katika uchumi na maendeleo ya nchi.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad