HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 2 August 2018

JENGENI DARAJA USIKU NA MCHANA- KWANDIKWA

Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa amemtaka Mkandarasi anayejenga Daraja la Magara linalounganisha Wilaya ya Babati na Mbulu kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha ujenzi wake unakamilika kwa haraka na ubora unaotakiwa ili kuwaondolea wananchi kero ya usafiri inayowakabili.

Akizungumza mara baada ya kukagua daraja hilo, Kwandikwa amesema tayari kiasi cha shilingi bilioni 1.4 kimelipwa kama malipo ya awali hivyo Mkandarasi aongeze kasi na kulimaliza daraja hilo pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa Kilomita 4.9 katika kipindi cha miezi 24.

“Daraja hili likikamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa litahamasisha shughuli za biashara na uzalishaji kati ya Mbulu na Babati na hivyo kuchochea uchumi wa wilaya hizo” amesema Kwandikwa.

Aidha amemtaka Mkandarasi China Railway Seventh Group (CRSG) anaejenga daraja hilo kutoa fursa za ajira kwa wakazi wa Wilaya za Mbulu na Babati katika kuharakisha ujenzi wake.

Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Manyara, Mhandisi Bashiri Rwesingisa amemhakikishia Naibu Waziri Kwandikwa kuwa ujenzi wa Daraja la Magala ni Sehemu ya Mkakati wa Serikali wa kuijenga barabara ya Kutoka Mbuyu wa Mjerumani hadi Mbulu kwa Lami ambapo tayari upembuzi yakinifu kwa ajil ya ujenzi huo umekamilika.

Mhandisi Rwesingisa amemhakikishia Naibu Waziri Kwandikwa kuwa pamoja na ujenzi wa daraja la Magala mkakati wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kutoharibu mazingira ili kuyawezesha maji kufuata mkondo na hivyo kupunguza adha wakati wa mvua unaendelea.

Naye Mhandisi Lusekelo Kijalo anaesimamia mradi huo amesisitiza kwamba ujenzi wa daraja la Magala na barabara unganishi zenye urefu wa Kilomita 4.9 utakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa.

Naibu Waziri Kwandikwa yuko katika ziara ya kukagua maendeleo ya miundombinu ambapo pamoja na mambo mengine amekagua eneo la Mwada-Mbuyu wa Mjerumani kitakapojengwa kituo cha pamoja cha ukaguzi wa magari kitakachohusisha mizani, polisi na huduma za kibiashara.
 Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Manyara, Mhandisi Bashiri Rwesingisa akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa (aliyevaa kofia) kuhusu hatua iliyofikia ya maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Mizani ya kudumu katika eneo la Mwada-Mbuyu wa Mjerumani, Wilayani Babati. Mkoani Manyara.
 Muonekano wa eneo la Mwada Wilayani Babati  itakapojengwa mizani na kituo cha pamoja cha ukaguzi wa magari mkoani Manyara.
 Muonekano wa mto Manyara ambapo linajengwa daraja la Magara lenye urefu wa mita 84, wilayani Babati Mkoani Manyara. Daraja hilo linatarajiwa kukamilika katika kipindi cha  miezi 24.
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa akitoa maelekezo kwa Uongozi wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mkoa wa Manyara kuhusu kuzingatia viwango katika ukarabati wa barabara sehemu ya mlima Magara kwa kiwango cha zege mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Mkoani Manyara.
 Mafundi wakindelea na ujenzi wa  barabara sehemu ya Magara kwa kiwango cha zege, Mkoani Manyara.
Muonekano wa barabara Magara-Mbulu ambayo inafanyiwa ukarabati na Wakala wa Barabara Nchini (TNAROADS) kwa kiwango cha zege,Mkoani Manyara.m

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad