HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 29 August 2018

ANAYEJENGA FLY OVER TAZARA AWEKA REKODI YA AINA YAKE

 Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan(JICA) Ofisi ya Tanzania Toshio Nagase akizungumza leo jijini Dar es Salaam ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mhandisi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania(Tanesco) Ilala, Dastani Ndamugoba  katikati akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar ees Salaam leo kuhusu mradi wa umeme uliopo Muhimbili. Kulia ni Meneja wa Tanesco Ilala Mhandisi Sotco Nombo.
 Jinsi barabara ya flyover ilivyo.
Baadhi ya wajumbe kutoka JICA wakifurahia kukamilika kwa ujenzi wa Fly over ya Tazara jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wakisikiliza maelezo kutoka kwa mwakilishi wa JICA.

*Atumia saa milioni 2.4 ya kazi bila kupata ajali.
*Mwakilishi JICA ataja vipaumbele miradi ya maendeleo

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
MWAKILISHI Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan(JICA) nchini Tanzania Toshio Nagase amesema Mkandarasi wa kijapani amefanikiwa kuweka rekodi ya usalama wakati wa ujenzi Fly over ya Tazara ambapo kwa zaidi ya saa milioni 2.4 ya kazi yamepita bila ajali.

Amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati anaelezea namna JICA wamekuwa wakishiriki katika kutoa misaada ya mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya miradi ya kimaendeleo.

Amefafanua JICA imekuwa inatekeleza miradi mbalimbali hapa nchini tangu mwaka 1963 na kwamba Watanzania 18,000 wamepata mafunzo Japan, wataalam 2,000 wa Japan wamekuja nchini.Pia watalaam wa kujitolea kutoka nchi hiyo 1600 wameletwa Tanzania kwa nyakati tofauti.

Hivyo wakati anazungumzia ujenzi wa Fly over hiyo amesema mkandarasi Japan ameweka rekodi kwani hadi sasa hakuna aliyepata ajali.

“Barabara ya juu ya kwanza yenye urefu wa mita 425 ambayo itakamilika Septemba mwaka huu.Msongamano wa magari kwenye makutano ya barabara yenye magari mengi hapa nchini utapungua kwa kiasi kikubwa.

“Muda wa kusafiri utapungua kwa takribani asilimia 40,”amesema Nagase.

Mbali na ujenzi huo wa Flyover amesema JICA wamefanikiwa kutoa misaada ya fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali nchini na kufafanua Tanzania ndio nchi inayoongoza miongoni mwa zile zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kupata misaada mingi kutoka Japani.

“Serikali ya Japani na JICA ina mipango tisa chini ya maeneo matatu ya kipaumbele na eneo la kwanza ni kukuza uchumi, kuendeleza kilimo, kuendeleza kilimo cha mpunga na kuendeleza viwanda.

“Eneo la maendeleo ya miundombinu na hasa usafirishaji na mipango ya nishati  na eneo la tatu uimarishaji wa huduma za jamii hasa utawala bora,utawala wa fedha za umma , afya na miradi ya maji,”amesema.

Pia JICA imeelezea mradi wa umeme katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam ambapo kukamilika kwa mradi huo umesaidia kuondoa changamoto mbalimbali zilizopo hospitalini hapo.

Akizungumzia mradi huo wa umeme Mkuu wa Idara ya Ufundi na Matengenezo Mhandisi Leonard Elizeusi amesema kukamilika kwa mradi huo kumeifanya Hospitali ya Muhimbili kuondokana na changamoto ya kukatika umeme.

“Hatuna tatizo la umeme katika hospitali ya Muhimbili.Tunao umeme wa uhakika na mahitaji yetu uniti 4 lakini umeme unaozalishwa hapa ni uniti 12,”amesema.

Amefafanua kabla ya kuwepo kwa kituo hicho cha umeme kulikuwa na changamoto ya kukatika umeme mara mbili kwa wiki na hivyo kwa mwezi kutumia gharama kubwa kununua mafuta kuendesha majenereta.

Pia amesema changamoto ya umeme ilisababisha wakati mwingine huduma kutofanyika na hivyo kusabibisha vifo lakini sasa hakuna matatizo ya umeme na hilo ni jambo la kujivunia.

1 comment:

  1. Ni usalama wa kiwango cha juu katika mradi mkubwa kama huo lakini hivi aloandika hii habari anajua masaa million 2.4 ni sawa na miaka mingapi.
    Tunatambua kazi ilofanywa lakini msitamke vitu ambavyo hamna uelewa navyo

    ReplyDelete

Post Bottom Ad