HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 18 July 2018

VYAMA VYA UKOMBOZI BARANI AFRIKA VYATAKIWA KUINGIA KATIKA AWAMU YA PILI YA UKOMBOZI WA KIUCHUMI

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
VYAMA vilivyoshiriki kupigania ukombozi wa Bara la Afrika sasa vimetakiwa kuingia awamu ya pili ya ukombozi wa kiuchumi kwa ajili ya maendeleo ya Bara la Afrika huku vikitakiwa kukomesha rushwa, ufisadi na ubadhirifu.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Balozi Seif Ali Idd wakati anafunga mkutano wa siku mbili uliohusisha vyama vilivyokuwa mstari wa mbele kupigania ukombozi Kusini mwa Bara la Afrika.

"Awamu ya kwanza ilikuwa ni kupigania uhuru kwa nchi za Afrika na sasa uhuru tunao, hivyo vyama hivyo vinatakiwa kuingia awamu ya pili ya ukombozi wa kiuchumi.

"Kuna kila sababu ya kujifunza kutoka China ambapo wameendesha mapinduzi ya kiuchumi na  kuwakomboa wananchi wake wapatao bilioni  mbili,"amesema.

Amefafanua kama si China mambo yangekuwa mabaya na kama ingekuwa inatolewa Kombe la Dunia kwa nchi ambayo imefanikiwa kujenga uchumi imara basi kombe lingekwenda China.

Balozi Idd amesema China imekuwa ikitoa msaada kwa nchi mbalimbali za Afrika ikiwamo Tanzania ambayo imekuwa ikinufaika na misaada ya nchi hiyo na miradi mbalimbali ambayo imeacha alama isiyofutika akitolea mfano reli ya TAZARA.

Amesema kwa upande wa Zanzibar kuna miradi mingi ya maendeleo imefanyika ikiwamo pia ujenzi wa kiwanda cha sukari , viwanja vya kisasa vya mpira.

Akifafanua zaidi kuhusu mkutano huo, amesema ni vema yale ambayo wamekubaliana yakatekelezwa kwa vitendo na si maneno matupu.

"Mada zote zilizotolewa katika mkutano huo zilikuwa za wazi na zimejadiliwa kwa kina.Nitoe rai hakikisheni yale ambayo mmekubaliana basi yanatekelezwa kwa vitendo.

"Pia hakikisheni mnaongeza mapambano katika vita dhidi ya rushwa na ufisadi.Ni wakati muafaka sasa wa kuanza ukombozi wa kiuchumi kwa nchi za Afrika,"amesema Balozi Idd.

Amesisitiza CCM tangu kuazishwa kwake kimekuwa mstari wa mbele kupiga vita rushwa na chini ya Mwenyekiti wake Rais Dk.John Magufuli ameongeza pambano dhidi ya rushwa na ufisadi huku akiimarisha nidhamu katika utumishi kupitia kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu.

"Tunakipongeza Chama cha Kikomunisti cha China(CPC) kwa kuamua mkutano huu kufanyika nchini Tanzania ambapo pamoja na mambo mengine vyama vya Afrika vimepata nafasi ya kujadili mambo kwa kina na kufikia maazimio,"amesema.

Kwa upande wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa  kutoka CPC Xu Lyuping amesema mkutano huo umefanyika kwa mafanikio makubwa na pasipo shaka utakuwa na matokeo makubwa.

Amesema anaamini vyama vyote vilivyo shiriki wamepata uelekeo wa namna ya kwenda kupambana na ukombozi wa kiuchumi kwa maendeleo ya Bara la Afrika na watu wake.

"Cha msingi ni kuwekwa jitihada za kufkia malengo.CPC imekuwa madarakani tangu mwaka 1949 na msingi wa kukaa madarakani kwa muda mrefu ni kuwaletea maendeleo wananchi,"amefafanua.

POLEPOLE NA FAIDA ZA MKUTANO

Kwa upande wake Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole amesema mkutano huo wa kidunia umefanyika kwa mara ya kwanza Afrika na kwa mara ya kwanza Tanzania.

Amesisitiza vyama vyote ambavyo vimeshiriki kuna mambo kadhaa ambayo wamekubaliana kwa ajili ya maendeleo ya Bara la Afrika huku akitumia nafasi hiyo kutoa shukrani kwa CPC kwa uamuzi wake wa kutakaka mkutano huo kufanyika nchini.Amesema ni wakati muafaka kwa vyama vyote vilivyoshiriki kupigania ukombozi wa Bara la Afrika kuendelea kuweka misingi imara ya kuleta maendeleo ya wananchi wake.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa kutoka Chama cha Kikoministi cha China (CPC)  Xu Lyuping akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati wa kufungwa  kwa mkutano wa Vyama vya Kisiasa Barani Afrika na Chama cha Kikoministi cha China leo Jijini Dar es Salaam.. Wa pili kushoto ni Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Dr. Bashiru Ali Kapura, na Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara NPhilip Mangula.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiufunga mkutano wa Vyama vya Kisiasa Barani Afrika na Chama cha Kikoministi cha China ukiofanyika kwa siku mbili Jijini Dar es Salaam .
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa kutoka Chama cha Kikoministi cha China (CPC)  Xu Lyuping akitoa salamu za Chama cha Kikoministi wakati wa kufungwa  kwa mkutano wa Vyama vya Kisiasa Barani Afrika na Chama cha Kikoministi cha China leo Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Chama Kinachotawala Nchini Cape Vade Bwana Miguel Petro akitoa salamu za Chama hicho wakati wa kufungwa  kwa mkutano wa Vyama vya Kisiasa Barani Afrika na Chama cha Kikoministi cha China leo Jijini Dar es Salaam.
Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad