HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, 31 July 2018

UWANJA WA NDEGE WA TERMINAL III KUANZA KUTUMIKA MWEZI MEI MWAKANI

Na Ripota wetu, Globu ya Jamii
Waziri wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano Mhandisi Isack Aloyce Kamwelwe leo amefanya ziara ya mafunzo na ukaguzi wa Jengo la tatu la abiria katika Kiwanja cha  kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).

Akizungumza na waandishi wa habari katika ziara hiyo Waziri Kamwelwe amesema amefurahishwa na hatua ya ujenzi iliyofikiwa na kwamba anaamini akifika kwa awamu ya pili mambo yatakua mazuri zaidi. Amesema kuwa kufikia mwakani mwezi mei abiria wataanza kutumia uwanja wa Terminal 3.

"Nimefurahishwa sana na hatua ambayo ujenzi umefikia, kiwanja hiki kimejengwa kwa ubora wa kimataifa na miundombinu pamoja na vifaa vitatakavyo tumika katika jengo hili vitakua ni vya kisasa zaidi ambavyo viwanja vyote vya kimataifa hutumia", alisema Waziri Kamwelwe.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha JNIA Mhandisi Paul Rwegasha ameeleza kuwa kukamilika kwa jengo la tatu la abiria kunakuja na faida nyingi za kiuchumi kwa Taifa na mwananchi mmoja mmoja.

"Ukamilishwaji wa jengo hili la tatu la abiria katika Kiwanja Cha Kimataifa cha Julius Nyerere kutafungua milango mingi ya kiuchumi, serikali itaweza kupata mapato kupitia kodi za huduma mbalimbali zitakazo tolewa katika jengo hili, wananchi watapata ajira, wawekezaji wataongezeka na watalii pia", alisema Bwana Rwegasha.

Katika hatua nyingine Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha JNIA ameweka wazi kwamba, tayari mchakato wa kumpata mzabuni kwa ajili ya maandalizi ya kuhamia katika jengo la tatu la abiria na wazabuni kwa ajili ya upangaji wa maeneo ya huduma zitakazo patikana ndani ya jengo unaendelea.

"Tayari mchakato wa kuwapata hao wazabuni umeanza ambapo hatua ya awali imekamilika, hatua inayofuata ni kuwashindanisha wazabuni kwa wazabuni, ambapo tunatarajia kwamba tutampata mzabuni kwa ajili ya kufanikisha uhamaji wa baadhi ya huduma kutoka jengo la pili kwenda jengo la tatu la abiria na pia mzabuni ambae atafanya mpangilio wa huduma zitakazo patikana katika jengo hilo na kutoa ushauri kwamba huduma ipi ipatikane eneo lipi ", alieleza Bwana Rwegasha.
Aidha Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mhandisi Julius Ndyamukama akitoa taarifa ya ujenzi kwa Waziri Kamwelwe ameeleza kuwa hatua ya ujenzi wa Jengo la tatu la abiria unaendelea vizuri na wanatarajia kumaliza ndani ya muda uliopangwa.

Ujenzi wa jengo hili unaendelea vizuri ambapo mpaka sasa ujenzi wa eneo la maegesho ya magari umekamilika kwa asilimia 85 na ujenzi wa jengo la abiria umekamilika kwa asilimia 78 na kama ujenzi utaendelea kwa mwendo huu kufikia mwezi mei mwaka 2019 Kiwanja kitakabidhiwa kwa TAA kwa ajili ya matumizi, alisema Ndyamukama.

Katika ziara hiyo Waziri akiongozana na Kaimu Mkurugenzi wa JNIA Bw, Paul Rwegasha, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mhandisi Julius Ndyamukama, msimamizi wa mradi wa ujenzi huo Wolfgang Marshick wa BAM International contractors, Mhandisi Mshauri Moharram kutoka Misri, wahandisi wasaidizi na waandishi wa habari ameweza kujionea sehemu mbalimbali za jengo hilo kuanzia upande ambao abiria wanaosafiri kwenda sehemu mbali mbali wataingia na sehemu ambayo abiria wanaowasili watatokea.

Sehemu nyingine ambazo Waziri amezikagua ni sehemu ya maegesho ya magari, sehemu ya kukagua mizigo, sehemu ya kuingilia watu muhimu, sehemu ya maduka na eneo la kujenga hoteli ya nyota nne kwa ajili ya abiria wanaowasili nyakati za usiku na ambao wanabadilisha ndege.

Mchakato wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria ulianza kufuatia ongezeko la abiria wanao ingia na kutoka kupitia uwanja wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) ambapo takwimu zilionyesha kwamba kufikia mwaka 2025 idadi ya abiria itakua Milioni 8 kwa Mwaka ukilinganisha na Jengo la pili la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka.
Gharama za ujenzi wa jengo la tatu la abiria zinakadiriwa kufikia Euro Milioni 254 sawa na bilioni 560 za Tanzania, aidha jengo la tatu la abiria litakua na uwezo wa kuhudumia abiria 2800 kwa saa, eneo la kuegesha magari mchanganyiko 2075, eneo la mita za mraba 227,000 kwa ajili ya maegesho ya ndege nyingi kwa wakati mmoja na maeneo mengine.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isaack Kamwelwe akizungumza na viongozi wanaosimamia mradi wa ujenzi wa jengo jipya  la III  la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakati wa ziara yake aliyoifanya uwanjani hapo leo.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isaack Kamwelwe akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Julius Ndyamukama wakati wa ziara ya kutembelea mradi wa ujenzi wa jengo jipya  la III  la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere(JNIA), Paul Rwegasha akizungumza kuhusu usimamzi wa kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Julius Nyerere wakati wa ziara ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isaack Kamwelwe alipotembelea mradi wa ujenzi wa jengo jipya  la III  la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Mkandarasi wa mradi wa jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Wolfgang Marschick akitoa maelezo kuhusu ujenzi wa jengo jipya  la III  la abiria wakati wa ziara ya kwanza ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isaack Kamwelwe katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) leo jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isaack Kamwelwe akizungumza wakati alipokuwa anatembelea mradi wa ujenzi wa jengo jipya  la III  la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) ili kujionea ujenzi unavyoendelea.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Julius Ndyamukama(katikati) akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isaack Kamwelwe(wa pili kushoto) wakazi wa ziara ya kutembelea  mradi wa ujenzi wa jengo jipya  la III  la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isaack Kamwelwe akikagua ujenzi wa jengo jipya  la III  la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) ili kujionea  ufanisi pamoja kujua changamoto wanazozipata wakati wa ujenzi huo.

Mwonekano wa ujenzi wa jengo jipya  la III  la abiria linaloendelea kujengwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isaack Kamwelwe akitoka kukagua ujenzi wa jengo jipya  la III  la abiria linalojengwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)  leo Jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isaack Kamwelwe akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza ziara ya kutembelea katika mradi wa ujenzi wa jengo jipya  la III  la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) leo Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad