HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, July 17, 2018

NCAA yaweka mikakati kuijaza Dreamliner

Na Ripota Wetu- Arusha
WAKATI Rais Dk. John Magufuli akitoa maelekezo ya kufikia watalii milioni 5 hadi ifikapo mwaka 2020, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imeanza utekelezaji wa agizo hilo kwa kukutana na wawekeza katika sekta ya utalii.

Ili kuhakikisha mikakati hiyo inafikiwa Serikali tayari imeleta ndege kubwa Boeing 787 Dreamliner ambayo pamoja na mambo mengine itapanua wigo zaidi wa kubeba wageni wakiwamo watalii kutoka ndani na nje ya nchi.

Wakati mikakati hiyo ikiendelea kutekelezwa na Serikali, NCAA kwa upande wake nao imeanza utekelezaji huo wa kufikia watalii milioni 5 mwaka 2020 kupitia Jukwaa la Uwekezaji katika sekta ya utalii kwa eneo la Ngorongoro.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Jukwaa hilo lililofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), mjini Arusha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Japhet Hasunga alisema malengo hayo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Ilani ya Chama kinachoongoza Serikali imeelekeza hadi mwaka 2020 tuwe tumefikia watalii milioni 2.Lakini Rais Dk. John Magufuli na Mwenyekiti wa CCM Taifa alitoa maelekezo tena ya kufikia watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2020,” alisema Hasunga.

Alisema Jukwaa hilo lililoandaliwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), ikishirikiana na wawekezaji kutoka kampuni za mawakala wa utalii, wamiliki wa kambi na hoteli za kitalii kutafungua ushirikiano zaidi wa kufikia malengo waliyojipangia.

Hivi karibuni Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ilifanya ziara na wawekezaji kwenye baadhi ya vivutio na maeneo wanayotarajia kukaribisha wawekezaji lengo ni kupokea ushauri na maoni ya wawekezaji hao.
 Naibu Mhifadhi wa NCAA Dk. Maurus Msuha akiwasilisha mada wakati wa Jukwaa la Wawekezaji katika sekta ya utalii kuhusu vivutio vipya vya utalii na uwekezaji kwenye eneo hilo la Ngorongoro.
 Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji Tarafa ya Ngorongoro Edward Maura akizungumza wakati wa Jukwaa la Wawekezaji wa sekta ya Utalii lililoandaliwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro mjini Arusha. 
  Naibu Mhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Asangye Bangu akizungumza wakati wa Jukwaa la Wawekezaji katika Sekta ya utalii lilofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC). 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Japhet Hasunga katikati akifuatilia mada wakati wa Jukwaa la Wawekezaji wa Sekta ya Utalii mjini Arusha, kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo Dk. Aloyce Nzuki kulia ni Mwenyekiti wa TATO Will Chambulo. 
 Viongozi wa Chama cha Mawakala wa Utalii (TATO), kutoka kushoto Katibu wa TATO Cyril Ako na Makamu Mwenyekiti wa TATO Henry Kimambo wakifuatilia mada kwenye Jukwaa la wawekezaji katika sekta ya utalii lililoandaliwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
 Baadhi ya wawekezaji wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa kwenye Jukwaa la Wawekezaji wa Sekta ya utalii lililoandaliwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad