HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, July 21, 2018

DC MJEMA AZINDUA CHANGAMKA MWANAMKE WILAYANI ILALA

Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii

MKUU wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam Sophia Mjema amezindua rasmi semina ya wanawake wajasiriamali ijulikanayo kama Changamka Mwanamke ambayo imehusisha maonesho ya bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na vikundi vya akina mama katika Wilaya hiyo.

Akizungumza leo katika hafla hiyo Mjema amesema kuwa  jukwaa hilo lenye lengo na nia ya kuwakwamua wanawake linajitosheleza, hivyo hakuna mwanamke atakayebaki kama alivyo mara baada ya kumalizika kwa semina hiyo.

Amewahimiza  na kuwa na jitihada katika kuhakikisha malengo yao yanatimia. Ameeleza kuwa amefurahishwa na shughuli zinazofanywa na wanawake hao kwani wameanzisha viwanda vidogo ambapo serikali ya awamu ya tano ina mlengo huo.

Mjema amewahaidi kuwashika mkono na kushirikiana nao ili kuweza kufikia uchumi wa  kati. Pia amesema kuwa kuna mifuko 19 ya kuwawezesha wanawake katika kila sekta na amewataka wanawake kuwekeza katika sekta mbalimbali.

Ametaja baadhi ya sekta hizo ni ufugaji, uvuvi, kilimo na nyinginezo na mikopo ya asilimia 20 itatolewa kwa akina mama, 20 kwa vijana na asilimia 10 kwa wazee na hii ni katika kuhakikisha uchumi wa wanawake na taifa unakua imara.

Aidha amemuagiza Afisa tarafa kuhakikisha wanawake hao wajasiri katika kutafuta mali wanapatiwa uhakika wa masoko ya bidhaa wanazouza na kutatua suala la mashine ya malipo kwa njia ya mtandao (EFD's.)

Naye Mkurugenzi na mwanzilishi wa taasusi hiyo Maria Lucas ameeleza kuwa lengo lao ni kuelimishana katika masuala ya afya, malezi na kutoa mafunzo katika shughuli za kiuchumi na wananufaika na mafunzo hayo kwani hadi sasa wamekuwa na shughuli mbalimbali ambazo zinawapa kipato.

Kwa niaba ya taasisi hiyo amemwomba mkuu wa Wilaya kuwasaidia katika kutatua changamoto za mashine za EFD's ambazo imekuwa changamoto kwao sambamba na ukosefu wa mitaji.

Katika semina hiyo viongozi wa ngazi mbalimbali na wajasiriamali wanawake walihudhuria ambapo pia walipata nafasi ya kusajiliwa katika mfuko wa NSSF.Pia wamepata  hekari 2 za kulima pilipili huko kibiti kutoka kwa mdau wa shughuli zao.
 Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema akikagua moja ya bidhaa zinazotengenezwa na wanawake wajisiriamali katika uzinduzi wa semina hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema akipata maelezo ya namna bidhaa hizo zinavyozalishwa alipokuwa katika moja ya mabanda ya wajasiriamali hao.

 Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla ya uzinduzi wa semina ya wajasiriamali leo jijini Dar es salaam

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad