NSSF YAVUNA WANACHAMA ELFU80 KAMPENI YA 'ZAMU YAKO' - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 21 June 2018

NSSF YAVUNA WANACHAMA ELFU80 KAMPENI YA 'ZAMU YAKO'

KAMPENI ya kitaifa ya kuhamasisha watu binafsi pamoja na walioko kwenye sekta isiyorasmi kujiunga na mfuko wa hifadhi ya jamii (NSSF) ya 'zamu yako', imeanza kutoa matokeo chanya baada ya zaidi ya watu elfu 80 kujiunga na mfuko huo hadi sasa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo kwenye kikao na viongozi wa vikundi vya wajasiriliamali na vyama vya ushirika mkoa wa Arusha, Mwenyekiti  wa kamati ya kuratibisha sera ya hifadhi ya jamii kwa sekta isiyo rasmi, Maryam Muhaji alisema kampeni hiyo ilianza Juni mosi mwaka huu katika Jiji la Dar es salaam.

Alisema  tangu kuanza kwa kampeni hiyo iliyoanzia katika mikoa ya Dar es salaam, Mwanza, Kagera, Mara na Arusha, tayari wanachama elfu 80 wamejiunga na mfuko wa NSSF na wameanza kupata huduma.

“Hii kampeni ya ‘Zamu Yako’ ni kampeni maalum ya kuhamasisha watu walioko katika sekta isiyo rasmi kujiunga na mfuko wa NSSF kwa kuwa katiba inamtaka kila mwananchi kujiunga na mfuko wa hifadhi ya jamii ni haki yake, hivyo baada ya kugawanywa kwa mifuko hii tumeanzisha kampeni hiui ili kutoa fursa kwa watu wote,”alisema.

Alisema  kwa kuwa lengo la Serikali ni kuwafikia wananchi wenye kipato cha chini kuweza kupata huduma muhimu, mfuko wa NSSF utaendelea na kampeni hiyo katika mikoa mbalimbali nchini na imepanga hadi kufikia Juni 2019 iwe imeshaandikisha wanachama laki 3.

Maryam alisema wanachama wanapaswa kujiunga na mfuko wa NSSF na kufaidika na mafao saba ya muda mrefu na muda mfupi yanayotolewa na mfuko huo ikiwemo pensheni, uzee, afya, uzazi, mazishi na kuumia kazini.

“Kwa kuanzia mtu anayetaka kujiunga na mfuko wa NSSF anapaswa kuchangia kiasi cha Tsh 20,000 kila mwezi ambapo pesa hiyo itamwezesha kupata huduma mbalimbali, kiwango hiki ni kidogo kulinganisha na huduma ambayo mwanachama ataipata, na hata atakapostaafu atapata mafao yatakayomwezesha kuendelea kuishi bila wasiwasi,”alisema.

Akifungua kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo aliwaagiza viongozi wote wa Wilaya ikiwemo maafisa ushirika kutambua vikundi vyote vilivyopo katika maeneo yao na kuviwasilisha katika ofisi za NSSF ili viweze kufikiwa na kuunganishwa na mfuko huo.

Kwa upande wake Meneja wa Saccos ya Kimandolu Utu Family, Charles Isaya aliipongeza NSSF kwa kuanzisha mpango huo wa kuandikisha wanachama kutoka sekta isiyorasmi na kudai kuwa atahakikisha wanachama wenzake wote wanajiunga ili kunufaika na huduma hiyo.

Hadi hivi sasa mfuko wa hifadhi ya jamii wa NSSF una wanachama laki2, wakati takwimu za serikali zinaonyesha kuwa sekta isiyorasmi ina zaidi ya watu milioni 18 ambao hawajajiunga na mfuko wowote wa hifadhi ya jamii jambo ambalo limekuwa likiwakosesha fursa mbalimbali za kupata mafao.

Mwenyekiti wa kamati ya kuratibisha sera ya hifadhi ya jamii katika sekta isiyorasmi  kupitia mfuko wa NSSF, Maryam Muhaji akizungumza na viongozi wa vikundi vya ujasiriamali na saccos mkoa wa Arusha katika ukumbi wa NSSF Arusha kuhamasisha kujiunga na mfuko huo.

Washiriki wa kikao cha semina kwa viongozi wa vikundi vya wajasiriamali na  vyama vya  ushirika mkoa wa Arusha wakimsikiliza Mwenyekiti wa kamati ya kuratibisha sera ya hifadhi ya jamii katika sekta isiyorasmi kupitia mfuko wa NSSF Maryam Muhaji (hayuko pichani) wakati wa ufunguzi wa kikao hicho.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad